Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Soka letu lipo kwa ajili ya Simba na Yanga

Niliwahi kuongea na mmoja wa wajumbe wa kamati ya saa 72 wakati wa utawala Jamal Malinzi.

Jamaa akaniambia ile kamati siyo ya kusimamia na kuendesha ligi kuu, ni ya kupigania maslahi ya Yanga na Simba kwenye ligi kuu.

Ndani ya vikao vyake ubishani ni kuhusu Yanga na Simba tu, kama vijiwe vya masokoni au maskani fulani hivi ya wana.

Usiombee mezani kuwe na hoja ya Yanga au Simba kufanya makosa, kanuni huwa zinawekwa pembeni na kuanza kubishana kwa hisia.

‘Mbona Mkude hakuoneshwa kadi kwa faulo kama ile, mbona Yondani hakufungiwa kwa kosa kama lile’.

Watu watabishana kwanza hadi wachoke, halafu ndiyo warudi kwenye kanuni.

Haijawahi kutokea mtu akapigania maslahi ya timu zingine mule zaidi ya Simba na Yanga.

Hizi timu zingine kanuni huachwa zifanye kazi barabara...lakini Yanga na Simba hutumia busara zaidi, kanuni kidogo!

Anasema wakati wa sakata la kadi tatu za njano za Mohamed Fakhi wa Kagera Sugar mwaka 2017, ndiyo kulikuwa na balaa.

Hadi Rais wa Shirikisho aliweka mkono kupigania maslahi ya klabu fulani ambayo haikuwemo moja kwa moja kwenye sakata lakini ilikuwa inafaidika na maamuzi.

Mbaya zaidi akasema kumbe hata Kelvin Yondani wa Yanga naye alikuwa na kadi tatu wakati ule ule, lakini kamati iliogopa kuchafua hali ya hewa.

‘Ingeonekana tuna malengo mabaya na Yanga. Yaani kama tunawatafutia sababu ili kuweka mzani sawa.’

Lakini anasema kulikuwa na malumbano makubwa sana kwenye hilo.

Sasa hii ni kamati moja kati ya kamati kibao za mamlaka zinazotakiwa kutenda haki.

Na wajumbe wake ni moja kati ya watendaji wengi ndani ya mamlaka tunaotarajia watutendee haki.

Tutafikaje nchi ya ahadi kwenye hali kama hii


Tatizo huanzia hapa

Mfumo wa mpira wa Tanzania unazalisha mashabiki wa aina mbili tu, Simba au Yanga.

Hawa ndiyo wakiwa watu wazima wanaingia kwenye taasisi zetu za kuongoza mpira.

Matokeo yake ndiyo haya...kuongoza kwa hisia.

Katika hali kama hii tutabaki na tatizo hili miaka na mikaka.

Moja ya sababu ya vilabu vingine kukosa mashabiki au kutozalisha mashabiki wa kutosha ni kuishi maisha mafupi.

Klabu ya mpira ili ivune mashabiki wake ni lazima kwanza ivae uwakilishi wa watu na kisha ikae muda mrefu ili iwe sehemu ya hao watu.

Ukiangalia msimamo wa ligi zetu za madaraja yote, utakuta takribani nusu ya timu hazikuwepo misimu mitano tu iliyopita.

Ukirudi nyuma misimu 20, utakuta zaidi ya robo tatu ya timu hazikuwepo kabisa...yaani zilikuwa hazijaanzishwa.

Tunaanzisha timu mpya kila uchao, kama bendi za siku kuu.

Tunatakiwa tuwe na ligi yenye timu za kudumu ambazo kila msimu zipo.

Msimu unapoanza, watu wanatakiwa wakae kwa kutulia kusubiri timu wanazozijua kuona zimebadilikaje kutoka msimu uliopita.

Hatuwezi kuzalisha mashabiki kwa timu zetu kuwa mpya kila siku.

Ushabiki ni hisia inayojengwa muda mrefu kutokana na kuguswa.


Suluhisho

Kila kitu kinachoonekana kinaenda vizuri basi kilifanyiwa jitihada za makusudi huko nyuma.

Na sisi tufanye jitahada za makusudi sasa kubadilisha hii hali.

Tuwe na sheria ngumu kwa timu kushiriki ligi, hasa za kulipwa.

Lazima timu iwe na vigezo hasa, siyo hivi vya sasa.

Tufanye kama Marekani wanavyofanya. Ili timu ipate nafasi ya kushiriki ligi, lazima iwe na uwezo wa kifedha, uwanja wa uhakika wa mechi na mazoezi na akiba kwenye akaunti yake inayoweza kulipa mishahara hata miezi mitatu mbele.

Kama timu haina hivyo vigezo, isiruhusiwe kushiriki ligi.

Ni bora tuwe na ligi zenye timu chache zenye uwezo kuliko kuwa na ligi zenye timu nyingi dhoofu-li-hali.

Kwa mfano tuwe na ligi zenye timu zisizozidi 12 kwa kila daraja, kuanzia ligi kuu hadi daraja la nne.


Ligi Kuu timu 8

Championship timu 10

First Division timu 12

Second division timu 12

Ligi za timu chache zitakuwa rahisi kudhaminika na kuzifanya timu zigawane keki kubwa kubwa hivyo kuwa na uwezo wa kushinda hasa.

Hizi hela za Azam TV, bilioni 12 kwa mwaka zinaweza kudhamini ligi zote na kuzifanya ziwe na hela nzuri.

Timu zikiwa na hela nzuri zitadumu muda mrefu na kuzalisha mashabiki wake hivyo kufanya mgao wa mashabiki kuwa na mizania.

Mgao wa mashabiki ukiwa na mizania, maana yake sasa tutapata watu wenye hisia na timu mbalimbali kwenye vikao vya maamuzi.

Lakini kwa sasa vikao vya maamuzi ni sawa na Bunge la Makaburu wakati wa ubaguzi wa rangi Afrika Kusini.

Yaani anakuwepo mbunge mmoja mzungu ambaye kazi yake ni kuwawakilisha watu weusi.

Yaani kuna wajumbe wa Yanga na Simba kazi yao ni kuviwakilisha vilabu vingine.

Hatuwezi kwenda!