Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sare za Simba zawaponza Boban,Nyosso

Haruna Moshi 'Boban'

*Mmoja asimamishwa, mwingine aenda timu ‘B’
SARE mfululizo zilizomchefua Kocha Milovan Cirkovic, zimezua jambo baada ya jana uongozi wa Simba kumsimamisha kiungo Haruna Moshi 'Boban' kwa utovu wa nidhamu, huku beki wa kati Juma Nyosso akishushwa heshima na kupelekwa kikosi ‘B’ ili kujirekebisha tabia.

Habari za uhakika zilizonaswa na gazeti hili na kuthibitishwa na uongozi wa klabu, zimesema kwa kiasi kikubwa wachezaji hao wanahusika timu kukosa ushindi.

Habari zinasema, Boban amesimamishwa kwa madai ya kutoa taarifa za uongo kwamba anaumwa na hivyo kukosa mchezo dhidi ya Coast Union.
"Boban alidai anaumwa hivyo hakwenda Tanga, lakini cha kushangaza alionekana akicheza mechi za 'ndondo' Upanga," alisema kiongozi mmoja.

"Amekuwa akifanya matukio mengi ya utomvu wa nidhamu na mara kadhaa uongozi umekuwa ukimpa onyo, lakini imekuwa kinyume chake," aliongeza.
"Hebu fikiria, mchezaji (Boban) anafahamu mechi yetu na Coastal ilivyokuwa ngumu, anadanganya kwa daktari anaumwa lengo likiwa kwenda mchangani."

"Boban huyuhuyu anafahamu tuna mdhamini na kuna mavazi maalumu kambini, lakini yeye anakuja na nguo zake za ovyo na ndala, akiulizwa anasema amegawa, apewe nyingine. Sasa mtu unagawaje kifaa chako cha kazi?" alihoji mtoa habari huyo.

"Kwenye mazoezi wachezaji wote wanatakiwa wapande basi moja, lakini yeye anakuja na gari lake, hataki kupanda basi. Kwa ufupi ni mtovu mkubwa wa nidhamu na uongozi umenawa mikono."

Alisema uongozi umeamua kumsimamisha kwa muda, na jana alitarajiwa kupewa barua yake.
Kwa upande wa Nyoso ameondolewa kikosi cha kwanza na kupelekwa kikosi chini ya miaka 20 ili ajirekebishe na kupandisha kiwango chake.

"Nyoso amekuwa mzembe, mechi tatu amepewa kadi za njano tatu. Kutokuwa kwake makini, kumesababisha kugawa magoli kwa wapinzani wetu," alisema.
"Mfano mechi dhidi ya Kagera Sugar alisababisha timu kufungwa magoli ambayo naweza kusema hayakuwa na ulazima.

"Imependekezwa arudi kikosi ‘B’ ili akajifunze tabia pia kupandisha kiwango chake."
Pamoja na sare nne tangu kuanza ligi, Simba bado inaongoza msimamo. Ilitoka sare ya 1-1 na Yanga, 2-2 Kagera Sugar, bila kufungana na timu za Coastal Union na JKT Mgambo zote za Tanga.

Wakati huohuo, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakaria Hanspope amesema muda wa klabu yake kutumia uungwana ili kulipwa Dola 32,000 wanazomdai beki wa Yanga, Mbuyu Twite umekwisha na kitachofuata ni kumkamata.

Hanspope alisema uamuzi huo ni wa lazima, na ikibidi hata ngumi, mateke na pingu kutumika ili kumfikisha mahakamani.

Kitisho hicho cha Hanspope kimekuja baada ya Yanga kushindwa kutekeleza agizo la Kamati ya Nidhamu, Maadili na Hadhi za Wachezaji zilizoitaka klabu hiyo ya Jangwani kuilipa Simba ndani ya siku 21.

Akizungumza juzi, Dar es Salaam, Hanspope alisema, klabu imefikia uamuzi wa kuchukua hatua hiyo kwa kile wanachodhani Shirikisho la Soka Tanzania(TFF) limeshindwa kuishinikiza Yanga kulipa pesa hizo.

Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah akizungumzia sababu za kutoichukulia Yanga hatua ikiwamo kuikata fedha kupitia mapato ya viingilio vya mechi zake alisema: "Hakuna kanuni inayotupa sisi mamlaka ya kuikata Yanga fedha kupitia mapato ya viingilio ukuzingatia kwamba Simba haikufuata kanuni katika kumsajili Twite kwani hawakuwasiliana na FC Lupopo.

"Isitoshe Simba walikiri kutofuata taratibu, ndiyo maana wakataka uungwana utumike na hata kikao cha klabu hizo na kilikuwa ni 'fair play' tu, zaidi ya hapo kamati haikutupa maelekezo ya nini tufanye endapo Yanga itashindwa kulipa fedha hizo ndani ya muda huo vinginevyo tusubiri kama itatupa maelekezo mengine."