Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Stars mambo magumu Kombe la Dunia

Dar es Salaam. Taifa Stars imepoteza matumaini ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia mwaka 2026, baada ya kulala kwa bao 1-0 dhidi ya Niger kwenye mchezo uliopigwa Uwanja wa Amaan Zanzibar.

Stars ilikuwa inatakiwa kuhakikisha inapata ushindi kwenye mchezo huu ili kufikisha pointi 13 ambazo zingefufua matumaini yake ya kucheza hatua ya mchujo wa michuano hiyo, lakini mambo yakawa magumu nyumbani.

Siku chache zilizopita pia Stars ilishindwa kuwika ilipovaana na vibonde Congo Brazaville na kutoka sare ya bao 1-1 ugenini.

Bao pekee la Niger ambayo ilionyesha kiwango kizuri kwenye mchezo huu liliwekwa kimiani na Daniel Sosah katika dakika ya 58 ya mchezo, baada ya kumalizia krosi iliyopigwa na kuwapita mabeki watatu wa Stars na kumkuta mfungaji.

Baada ya bao hilo, Stars ilibadili aina ya kucheza na kushambulia kwa nguvu kubwa lakini bado ilishindwa kuuweka mpira kimiani pamoja na kupata nafasi kadhaa za wazi za kufunga.

Dakika ya 79, Niger ilipata pigo baada ya beki wake wa kati Boureima Katokore kupewa kadi nyekundu, hata hivyo bado haikuisaidia Stars kusawazisha bao.

Matokeo haya yamefifisha kwa asimilia 90 matumaini ya Stars kucheza hatua ya mchujo baada ya kubaki nafasi ya pili na pointi 10, moja mbele ya Niger huku Morocco ikiwa imeshafuzu kwenye fainali zijazo baada ya kufikisha pointi 21.

Sasa itacheza mchezo wa mwisho wa makundi nyumbani mwezi ujao, itakapovaana na Zambia ambayo inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi sita kwenye msimamo.

Hata hivyo, Stars ambayo ilifika robo fainali ya Michuano ya Kombe la Mataifa Afrika kwa Wachezaji wa Ndani CHAN 2024 mwezi uliopita, hii ndiyo mara ya kwanza timu hiyo inakusanya pointi nyingi zaidi kwenye michuano ya kufuzu Kombe la Dunia baada ya kufikisha kumi, rekodi ya nyuma inaonyesha waliishia kwenye pointi nane.