Stars na mfupa mgumu AFCON 2025
Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars ipo Misri katika maandalizi ya mwisho kabla ya kwenda Morocco kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON 2025) zitakazoanza Desemba 21, 2025 hadi Januari 18, 2026.
Fainali hizo zinafanyika Morocco kwa kushirikisha timu 24, Taifa Stars ni miongoni mwa washiriki ikiwa ni mara ya nne inakwenda kucheza AFCON baada ya 1980, 2019 na 2023.
Kocha Miguel Gamondi ana mtihani wa kuhakikisha Taifa Stars safari hii inatoboa kwenda 16 bora baada ya mara zote kuishia makundi tena kwa aibu.
Ilishuhudiwa mwaka 1980 katika Fainali za AFCON nchini Nigeria, Taifa Stars ikimaliza mkiani mwa kundi A ikikusanya pointi moja, kisha mwaka 2019 zilipofanyika nchini Misri, ikamaliza tena mkiani mwa kundi C bila ya pointi, huku 2023 katika fainali zilizochezwa Senegal mwaka 2024, Stars ikamaliza mkiani mwa kundi F bila ya pointi.
Kumaliza bila ya pointi mara mbili za mwisho, ni mtihani wa kwanza anaokabiliana nao Gamondi, pia kuivusha Stars kwenda hatua ya 16 bora kwa mara ya kwanza, ni mtihani wa pili.
Fainali hizo zinaanza kuchezwa wikiendi hii kwa wenyeji Morocco kufungua dimba dhidi ya Comoros kwenye Uwanja wa Prince Moulay Abdellah uliopo katika Mji wa Rabat.
Mwanzo mpya wa Gamondi
Gamondi ameshafanya vizuri katika soka la Tanzania akiwa na klabu ya Yanga kwa msimu mmoja na nusu ambapo alishinda Ligi Kuu Bara, Kombe la FA, Ngao ya Jamii na kuifikisha timu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika misimu miwili mfululizo akianza 2023-2024 ambapo alikwenda nayo hadi robo fainali na 2024-2025 aliposhindwa kuiongoza katika makundi, mkataba wake ulisitishwa kabla hatua hiyo haijaanza kuchezwa.
Alipohamia Singida Black Stars msimu huu, Gamondi ameendeleza makali yake kwa kuifikisha timu hiyo hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, ikiwa ni mara ya kwanza kwa klabu hiyo kufika hapo. Pia ameshinda Kombe la Kagame akiwa na Singida Black Stars.
Kukabidhiwa mikoba ya kuiongoza Taifa Stars akichukua nafasi ya Hemed Suleiman ‘Morocco’ aliyekubaliana na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kukaa pembeni baada ya kufanikisha timu kufuzu AFCON 2025, Gamondi anaanza maisha mengine upande wa timu ya taifa.
Tangu akabidhiwe kikosi cha Taifa Stars akiwa kaimu kocha mkuu, Gamondi amekiongoza katika mechi moja ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Kuwait iliyochezwa Novemba 15, 2025 na kupoteza kwa mabao 4-3.
Desemba 3, mwaka huu, Gamondi aliita kikosi cha awali cha AFCON chenye wachezaji 53, kisha ukafanyika mchujo na kubaki majina 28 ya nyota waliokwenda kambini Misri Desemba 8, mwaka huu kujiandaa na fainali hizo.
Akizungumzia namna alivyoita kikosi, Gamondi anasema: “Ilikuwa ngumu kuchagua, sio wachezaji 55, lakini ngumu zaidi ni baada ya kuchagua wachezaji 28.”
Ugumu wa kundi
Taifa Stars imepangwa kundi C na timu za Tunisia, Nigeria na Uganda.
Mechi ya kwanza itakuwa dhidi ya Nigeria itakayochezwa Desemba 23, mwaka huu. Takribani wiki moja kutoka sasa.
Baada ya hapo, Desemba 27 ni dhidi ya Uganda, kisha Desemba 30 itamaliza hatua ya makundi kwa kukabiliana na Tunisia.
Katika viwango vya FIFA vilivyotoka Novemba 20, 2025, wapinzani wa Tanzania wapo juu zaidi kulinganisha na nchi yetu iliyopo nafasi ya 112 duniani na 27.
Nigeria inakamata nafasi ya tano Afrika na ya 38 dunia, Tunisia ya sita Afrika na 40 duniani, huku Uganda ikiwa ya 17 Afrika na 85 duniani.
“Tanzania tutajitahidi, tutajitahidi hata zaidi kuiwakilisha nchi vyema ili kujaribu kufanya jambo la maana,” anasema Gamondi.
“Sizungumzii matokeo, bali taswira ya soka la Tanzania na dhamira ya kutetea bendera ya Tanzania hasa katika wakati huu muhimu. Tunaishi Tanzania, tunahitaji kuonyesha kitu.
“Nadhani umoja ndio ujumbe mzuri kwetu na kukaa pamoja kuandaa timu hii kushindana. Kundi ni gumu sana, lakini hakuna kinachoshindikana.
“Tunahitaji kuwa na ndoto, tunatakiwa kuwa na imani na kikosi. Kazi yetu ni kujiandaa zaidi ya kimwili, kiufundi na kiakili wachezaji kuwa tayari kutoa kiwango cha juu na kutoa utendaji mzuri.
“Natumai Watanzania wanaweza kutuelewa na kutuunga mkono na kuwafanya wachezaji wajisikie vizuri katika mashindano haya makubwa.”
Wapinzani sio wanyonge
Katika kundi hili, unaweza kusema Taifa Stars ni wanyonge kuanzia ushiriki hadi mafanikio.
Ukiitoa Uganda ambayo haina rekodi ya kubeba ubingwa kama ilivyo Taifa Stars, lakini imecheza fainali ya AFCON 1978 ikipoteza mbele ya wenyeji Ghana.
Pia Uganda inakwenda kushiriki AFCON mara ya nane, wakati Tanzania ni ya nne.
Kwa upande wa Tunisia, imetwaa ubingwa mara moja mwaka 2004 ilipokuwa mwenyeji. Inakwenda kushiriki kwa mara ya 22.
Nigeria ndiyo yenye mafanikio zaidi katika kundi hili, imebeba ubingwa mara tatu ikiwamo 1980 ilipokuwa mwenyeji, pia mwaka 1994 nchini Tunisia na 2013 pale Afrika Kusini.
Vikosi
Kocha Miguel Gamondi jeshi lake litakuwa hivi; Makipa: Yakoub Suleiman (Simba), Hussein Masalanga (Singida BS) na Zuberi Foba (Azam)
Mabeki: Bakari Mwamnyeto (Yanga), Shomari Kapombe (Simba), Lusajo Mwaikenda (Azam), Mohamed Hussein (Yanga), Nickson Kibabage (Singida BS), Wilson Nangu (Simba), Pascal Msindo (Azam), Haji Mnoga (Salford City, England), Dickson Job (Yanga) na Ibrahim Abdullah (Yanga)
Viungo: Novatus Dismas (Göztepe FC, Uturuki), Kelvin Nashon (Pamba Jiji), Alphonse Mabula (Shamakhi, Azerbaijan), Habibu Iddi (Singida BS), Tarrryn Allouche (Rochdale AFC, England), Charles Mombwa (Floriana FC, Malta), Morice Abraham (Simba), Kibu Denis (Simba), Feisal Salum (Azam) na Iddi Selemani (Azam).
Washambuliaji: Mbwana Samatta (Le Havre, Ufaransa), Seleman Mwalimu (Simba), Kelvin John (Aalborg BK, Denmark) na Simon Msuva (Al-Talaba, Iraq)
Kocha Mkuu: Miguel Gamondi
Kwa upande wa Uganda, Kocha Mkuu, Paul Put ameita wachezaji 30, lakini wanaotakiwa kushiriki mashindano ni 28, huku kikosi hicho kikiwa tayari kimefika Morocco tangu Desemba 7 mwaka huu kikiweka kambi kusubiri kuanza kwa fainali hizo.
Kikosi cha Uganda kipo hivi; Makipa: Salim Omar Magoola (Richards Bay), Denis Onyango (Mamelodi Sundowns), Alionzi Nafian (Defence Forces), Charles Lukwago (KCCA)
Mabeki: Toby Sibbick (Burton Albion), Elio Caprodossi (Universitatea Cluj), Jordan Obita (Hibernian), Rogers Torach (Vipers), Abdu Azizi Kayondo (Slovan Liberec), Isaac Muleme (Viktoria Žižkov), Timothy Awany (FC Ashdod), David Owori (SC Villa), Hilary Mukundane (Vipers)
Viungo: Kenneth Semakula (Al-Adalah), Khalid Aucho (Singida Black Stars), Ronald Ssekingada (APR), Bobosi Byaruhanga (Oakland Roots), Baba Alhassan (Steaua București)
Washambuliaji: Allan Okello (Vipers), Melvyn Lorenzen (Muangthong United), Travis Mutyaba (CS Sfaxien), Denis Omedi (APR), Mato Rogers (FK Vardar), Reagan Mpande (SC Villa), Jude Ssemugabi (Jamus), Uchechukwu Ikpeazu (St. Johnstone),
Steven Mukwala (Simba), James Bogere (Masaka Sunshine), Ivan Ahimbisibwe (KCCA) na Shafik Nana Kwikiriza (KCCA)
Kocha Mkuu: Uganda
Kocha Mkuu wa Tunisia, ami Trabelsi, ameita kikosi kinachoundwa na Makipa: Aymen Dahmen (CS Sfaxien), Bechir Ben Saïd (Espérance), Sabri Ben Hassen (Étoile) na Noureddine Farhati (Stade Tunisien)
Mabeki: Yan Valery (Sheffield Wednesday), Mohamed Ben Ali (Espérance), Dylan Bronn (Servette FC), Montassar Talbi (FC Lorient), Yassine Meriah (Espérance), Adem Arous (Kasimpasa), Nader Ghandri (Akhmat Grozny), Mortadha Ben Ouanes (Kasimpasa), Ali Abdi (Nice) na Ali Maaloul (CS Sfaxien)
Viungo: Ferjani Sassi (Al Gharafa), Ellyes Skhiri (Frankfurt), Houssem Tka (Espérance), Mohamed Hadj Mahmoud (FC Lugano), Ismael Gharbi (Augsburg), Hannibal Mejbri (Burnley FC), Naim Sliti (Al Shamal) na Mohamed Ali Ben Romdhane (Al Ahly)
Washambuliaji: Elias Saad (Augsburg), Elias Achouri (FC Copenhagen), Hazem Mastouri (Dinamo Makhachkala), Sébastien Tounekti (Celtic), Firas Chaouat (Club Africain) na Seifeddine Jaziri Zamalek)
Kocha Mkuu:
Kwa upande wa Nigeria, kocha mkuu wa timu hiyo, Eric Chelle ameita jeshi la watu 28 linaloundwa na Makipa: Stanley Nwabali (Chippa United), Amas Obasogie (Singida Black Stars), Francis Uzoho (Omonia)
Mabeki: Calvin Bassey (Fulham), Semi Ajayi (Hull City), Bright Osayi-Samuel (Birmingham City), Bruno Onyemaechi (Olympiacos), Chidozie Awaziem (Nantes), Zaidu Sanusi (Porto), Igoh Ogbu (Slavia Prague), Ryan Alebiosu (Blackburn Rovers)
Viungo: Alex Iwobi (Fulham), Frank Onyeka Brentford), Wilfred Ndidi (Besiktas), Raphael Onyedika (Club Brugge), Tochukwu Nnadi (Zulte Waregem), Fisayo Dele-Bashiru (Lazio), Ebenezer Akinsanmiro (Pisa), Usman Muhammed (Ironi Tiberias)
Washambuliaji: Chidera Ejuke (Sevilla), Akor Adams (Sevilla), Ademola Lookman (Atalanta), Samuel Chukwueze (Fulham), Victor Osimhen (Galatasaray), Moses Simon (Paris), Paul Onuachu (Trabzonspor), Cyriel Dessers (Panathinaikos), Salim Fago Lawal (Istra 1961)