Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sababu Sopu kutemwa Stars akimpisha Gomez

Muktasari:

  • Selemani Mwalimu anayeichezea Simba kwa mkopo akitokea Wydad Casablanca ya Morocco, amefunga bao moja katika kikosi cha Simba msimu huu.

Dar es Salaam. Benchi la ufundi la timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' chini ya Miguel Gamondi, limefanya mabadiliko ya kumtoaa mshambuliaji wa Azam FC, Abdul Suleimani 'Sopu' kutokana na jeraha na kumchukua mshambuliaji wa Simba, Selemani Mwalimu 'Gomez'.

Mabadiliko hayo yamebainishwa leo Jumamosi Desemba 13, 2025 na TFF, ikiwa ni siku nane kabla ya kuanza kwa Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 huko Morocco.

"Kocha Miguel Gamondi amemuita mshambuliaji Selemani Mwalimu kwenye kikosi cha Taifa Stars cha wachezaji 28 watakaocheza AFCON 2025 Morocco kuchukua nafasi ya Abdul Suleiman “Sopu” ambaye ameumia," imesema taarifa ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) bila kubainisha aina ya jeraha.

Mwalimu anayeitumikia Simba kwa mkopo akitokea Wydad Casablanca alikuwa miongoni mwa wachezaji 55 ambao walikuwemo kwenye kikosi cha awali cha wachezaji 55 wa Taifa Stars kilichowasilishwa kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Kwa mujibu wa kanuni za Fainali za AFCON 2025, mchezaji ambaye jina lake lipo kwenye kikosi cha awali ndiye atapaswa kuchukua nafasi ya mchezaji aliyeumia katika kikosi cha mwisho cha wachezaji 28 wanaoshiriki AFCON.

Hata hivyo, fursa ya mchezaji mwingine kuchukua nafasi ya mchezaji aliyeumia, inatolewa kabla ya mchezo wa kwanza wa timu ya mchezaji husika aliyeumia.

Mwalimu hadi sasa ameifungia Simba bao ambalo alilipata katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Namungo FC ambayo ilimalizika kwa ushindi wa mabao 3-0 ambao timu yake iliupata katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Kwa sasa, Taifa Stars ipo nchini Misri ikijiandaa na Fainali za AFCON 2025 ambazo zitafanyika Morocco kuanzia Desemba 21 mwaka huu hadi Januari 18, 2026.

Katika fainali hizo, Taifa Stars imepangwa kundi C na timu za Tunisia, Nigeria na Uganda.

Taifa Stars itaanza kwa kuikabili Nigeria, Desemba 23 kisha Desemba 27 itakabiliana na Uganda na mechi ya mwisho ya hatua ya makundi itakuwa ni Desemba 30 dhidi ya Tunisia.