Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Takwimu bora za michuano ya Euro 2024

Muktasari:

  • Mechi nyingine ya hatua hiyo kati ya England dhidi ya Uholanzi itapigwa Jumatano ijayo kwenye Uwanja wa Berlin.

Munich, Ujerumani. Michuano ya Euro inaendelea kesho kwenye uwanja wa Munich Arena wakati Hispania itakapovaana na wababe Ufaransa.

Mechi nyingine ya hatua hiyo kati ya England dhidi ya Uholanzi itapigwa Jumatano ijayo kwenye Uwanja wa Berlin.

Hispania ilifuzu hatua hii baada ya kuwatupa nje wenyeji Ujerumani, huku Ufaransa yenyewe ikiwaondoa kwenye mashindano hayo Ureno ambayo ilikuwa inapewa nafasi kubwa zaidi ya kwenda hatua ya nusu fainali.

Mchezo wa juzi uliishuhudia England ikitinga hatua hii muhimu kwa kuichapa Uswis kwa mikwaju ya penalti 5-3 baada ya sare ya dakika 120 za mchezo.

Kwa upande wa Uholanzi yenyewe ilipata tiketi ya nusu fainali baada ya kupita miaka mingi kwa ushindi wa dakika tisini, ikiwa ndiyo timu pekee ambayo imefuzu nusu fainali bila kwenda kwenye dakika za nyongeza kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya wabishi Uturuki.

Katika michezo ya nyuma ambayo timu hizo zimewahi kukutana, Hispania ilishinda michezo 16, imetoka sare saba na kupoteza dhidi ya Ufaransa mara 13.

Kwa upande wa England imewahi kushinda mara sita dhidi ya Uholanzi, imetoka sare mara tisa na kupoteza michezo saba, hivyo huu hauwezi kuwa mchezo rahisi kwa timu zote.

Sasa mashabiki wanasubiri kwa hamu kubwa kuona ni timu gani inaweza kuibuka na ushindi kwenye michezo ya nusu fainali ili itinge hatua ya fainali kati ya kesho na keshokutwa.

Hata hivyo, tayari kuna dondoo kadhaa ambazo zimetengenezwa na timu pamoja na wachezaji kwenye michuano hii mikubwa Ulaya ambayo fainali yake itafanyika Jumapili, Julai 14.


Dakika hatari za mabao

Michuano ya Euro imeonekana kuwa na mabao machache yakiwa ni 108 mpaka sasa, tofauti na jinsi ilivyokuwa ile iliyopita na dakika ambazo zimeonekana kuwa yamefungwa mengi hadi sasa ni 16-30, ambapo kwenye dakika hizi yamefungwa mabao 20.

Dakika ya 46-60, yamefanikiwa kufungwa mabao 17 ukiwa ndiyo muda unaoshika nafasi ya pili kwa mabao mengi zaidi kufungwa kwenye michuano hii msimu huu.

Dakika 61- 75, inafuata ikiwa na mabao 16, 76-90 mabao 15, dakika za nyongeza baada ya tisini kumalizika zina mabao 12 huku dakika ya 1-15, zikiwa na mabao 14.

Dakika 30 za nyongeza ndiyo zimeshuhudia mabao machache baada ya kufungwa mawili tu.


Timu yenye mabao mengi

Ujerumani pamoja na kwamba imetupwa nje hatua ya robo fainali lakini ndiyo inaongoza kwa kufunga mabao mengi ikiwa nayo 12, inafuatiwa na Hispania ambayo imefunga 11, huku Uholanzi ambayo imefuzu nusu fainali ikiwa imefunga tisa. Hii ndiyo timu pekee ambayo imefuzu kwenye hatua hii ikiwa na mabao mengi.


Timu iliyoongoza kwa kumiliki

Ureno ndiyo imeshikilia usikani kama timu iliyomiliki mpira kwa asilimia kubwa ikiwa na wastani wa 64.2, Ikifuatiwa na Ujerumani 58.6 huku England ambayo imefuzu hatua ya nusu fainali ikiwa na 58.6, Hispania inashika nafasi ya nne ikiwa na 57.2.


Bila kuruhusu

Ufaransa ambayo imefuzu nusu fainali ndiyo kinara hapa ikiwa imecheza michezo minne bila kuruhusu bao lolote, ikifuatiwa na Ureno ambayo imecheza michezo tatu ni Uholanzi ambayo ina mechi mbili.


Vinara wa mabao

Wachezaji watatu wamefungana kwenye chati ya juu ya kupachika mabao ambapo George Mikautdze wa Georgia, Jamal Masiala wa Ujerumani , Cody  Gakpo wa Uholanzi kila mmoja tayari ana mabao matatu.

Huku Gakpo akiwa na nafasi nzuri ya kuongeza mabao yake kwa kuwa bado yupo kwenye mashindano, lakini atakuwa akipambana na Jude Bellingham wa England ambaye ana mabao mawili na timu yake imefuzu nusu fainali hivyo ana nafasi ya kufunga zaidi.


Vinara wa asisti

Lamine Yamal wa Hispania ndiye kinara hapa akiwa nazo tatu, huku akiwa na nafasi ya kuongeza nyingine kwa kuwa timu yake bado ipo kwenye mashindano.

Nafasi ya pili inashikwa na Arda Guler wa Uturuki, Simons wa Uholanzi, na Fabian Ruiz wa Hispania ambao kila mmoja ana pasi mbili za mabao.


Mashuti yaliyolenga lango

Staa wa Ujerumani ambaye hakuwa na nyota sana na mashabiki wa timu hiy o Kai Havertz akiwa amepiga mashuti 11, Cristiano Ronaldo anafuata hapa akiwa na tisa, Cody Gakpo wa Uholanzi na Kylian Mbappe wa Ufaransa kila mmoja ana mashuti manane yaliyolenga lango wakiwa bado timu zao zipo.