Takwimu zinambeba Saido Ntibazonkiza
Muktasari:
- Juzi Simba ilitangaza kuachana na Saido akiwa ni mchezaji wa pili baada awali kumuaga John Bocco, pia wakafuata Shaaban Chilunda, Luis Miquissone na Kennedy Juma.
Dar es Salaam. Klabu ya Simba juzi iliachana rasmi na aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa timu hiyo Mrundi, Saidi Ntibazonkiza 'Saido' baada ya mkataba wake kumalizika huku nyota huyo akiondoka na rekodi tamu tangu alipoanza kucheza Ligi Kuu Bara.
Juzi Simba ilitangaza kuachana na Saido akiwa ni mchezaji wa pili baada awali kumuaga John Bocco, pia wakafuata Shaaban Chilunda, Luis Miquissone na Kennedy Juma.
Nyota huyo kwa mara ya kwanza alitua nchini Oktoba 12, 2020, aliposajiliwa na mabingwa wa Ligi Kuu Bara, Yanga akitokea Vital'O FC ya kwao Burundi na kukitumikia kikosi hicho kwa misimu miwili kisha kuachana nacho rasmi Julai Mosi, 2022.
Katika misimu miwili aliyoichezea Yanga, alicheza jumla ya michezo 18 ya Ligi Kuu Bara akihusika katika mabao 10 ambapo alifunga saba na kutoa pasi tatu za mabao. Baada ya hapo akajiunga na kikosi cha Geita Gold ambapo alicheza michezo 11 ya Ligi Kuu Bara huku akihusika katika jumla ya mabao 10, alifunga manne na kutoa pasi sita za mabao kiwango ambacho kiliwavutia mabosi wa Simba na kumsajili Desemba 29, 2022.
Kiwango Simba
Usajili wake wa kwenda Simba uliwashtua wadau wengi huku baadhi yao wakionekana kuukosoa kwa kile walichoeleza kiwango chake kushuka ingawa baadaye aliwafunga midomo kutokana na ubora wake.
Msimu wake wa kwanza wa 2022/2023, licha ya kuingia dirisha dogo la Januari alicheza jumla ya michezo 12 ya Ligi Kuu Bara ambapo alihusika katika mabao 19, baada ya kufunga 13 wastani wa bao moja kila mchezo na kuchangia sita huku akiwa kinara kwa upande wa Simba.
Msimu huo ulimfanya kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara baada ya kufunga jumla ya mabao 17, ambapo manne aliyafunga akiwa na Geita Gold na 13 akiichezea Simba. Saido alikuwa mfungaji bora sambamba na aliyekuwa nyota wa Yanga Mkongomani, Fiston Mayele aliyetua Pyramids FC ya Misri.
Nyota huyo aliendeleza moto wake ndani ya kikosi hicho ambapo msimu uliopita wa 2023/2024, alicheza jumla ya michezo 26 ya Ligi Kuu Bara akihusika katika mabao 14, kwenye timu hiyo baada ya kufunga 11 na asisti tatu akiibuka tena kinara kwenye timu hiyo.
Hii ina maana kuwa kwa misimu miwili mfululizo Saido ndiye amekuwa mfungaji bora wa Klabu ya Simba lakini akimaliza kwenye nafasi ya pili msimu mmoja nyuma na ya tatu msimu uliopita kwenye ligi.
Aibeba Simba kimataifa
Msimu uliopita Saido pia alikuwa kinara wa ufungaji kwenye Klabu ya Simba katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya timu hiyo kufunga mabao tisa hatua ya makundi, lakini Mrundi huyo akahusika kwenye mabao manne baada ya kufunga mawili na kutoa pasi mbili za mabao akilingana na Pacome Zouzoua wa Yanga.
Hii ina maana kwamba kiungo huyo mshambuliaji aliwazidi mastaa wengine wote wa timu hiyo kwenye michuano hiyo kwenye eneo la kuhusika na mabao.
Hii ina maana kwamba baada ya Simba kuachana na staa huyo, inawalazimu kutafuta mchezaji ambaye atakuwa bora kuliko Mrundi huyo ili aweze kufikia kiwango chake kuepuka kurudia makosa ya kumuacha Jean Baleke na Moses Phiri ambao walikuwa wanafanya vizuri kwenye eneo la ufungaji na kuwasajili Fred Michael na Pa Omary Jobe ambao walishindwa kufikia kiwango chao.
Akizungumza na Mwananchi, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema, wachezaji wote wanaoachana nao haina maana hawana umuhimu ila wanachotaka kukifanya kwa sasa ni kutengeneza timu imara na yenye ushindani msimu ujao.
"Mashabiki wasiwe na presha, kila mchezaji ambaye tumeachana naye ana umuhimu mkubwa, lakini jambo tunalotaka kwa sasa ni kutengeneza timu mpya imara na yenye ushindani zaidi," alisema Ahmed.
Namba zake zinambeba
Kiujumla nyota huyo tangu atue hapa nchini akizichezea Yanga, Geita Gold na baadaye Simba, amecheza jumla ya michezo 67 ya Ligi Kuu Bara na kuhusika katika mabao 53, baada ya kufunga 35 na kuchangia mengine 18.
Wachezaji wa zamani wafunguka:
Mchezaji na kocha wa zamani wa Simba, Abdallah 'King' Kibadeni alisema, kuachwa kwa wachezaji ndani ya timu hiyo kwake halimshtui sana kwa sababu viongozi wanatambua wanafanya hivyo kwa lengo la kutengeneza kikosi kizuri chenye ushindani.
"Kwangu sioni shida ila unapoacha mchezaji ni lazima ufanye tathimini ya kina juu ya maamuzi unayochukua, wao wanajua vizuri kutokana na jinsi mipango yao walivyoipanga kwa msimu ujao, hivyo ngoja tusubiri matokeo yake mbeleni," alisema.
Kwa upande wa nyota wa zamani wa kikosi hicho, Mtemi Ramadhan alisema, suala sio tu kuacha wachezaji isipokuwa ni jinsi gani unaweza kupata mbadala sahihi wa atakayeziba nafasi yake kwani wengi wao wamekuwa wakifeli na kujutia aliyeondoka.
"Unapoacha mchezaji mwenye namba nzuri kama Saidi Ntibazonkiza 'Saido' ni lazima kwanza ufanye tathimini ya kutosha kwa sababu uwezo wake unajieleza, sasa isije ikatokea ukaleta mtu ambaye watamkumbuka aliyetoka yaani hapo utakuwa umefeli."