Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tenga, Karia wabebeshwa zigo la AFCON 2027

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia (kulia) akiwa na Rais wa zamani wa TFF, Leodgar Tenga.

Muktasari:

  • Fainali za AFCON 2027 zitashirikisha idadi ya timu za Taifa 28 na zitafanyika Kenya, Tanzania na Uganda zitakazoandaa kwa pamoja.

Dar es Saalam. Rais wa zamani wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Leodgar Tenga ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ndani ya Maandalizi na Uratibu (LOC) ya Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.

Wakati Tenga akiteuliwa kuwa Mwenyekiti wa kamati hiyo, Rais wa sasa wa TFF, Wallace Karia ameteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo.

Uteuzi huo ambao umefanywa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda na Waziri wa wizara hiyo Zanzibar, Dk. Riziki Pembe, umetangazwa leo, Jumatano, Aprili 15, 2026.

Katibu wa kamati hiyo atakuwa ni Neema Msitha na Msaidizi wake atakuwa ni Said Kassim Marine.

Kamati hiyo inaundwa na idadi ya wajumbe 28 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar ambao wanatumikia kada tofauti kama za utawala, michezo, masoko, biashara, utalii, ulinzi na usalama na habari.

Ukiondoa Tenga, Karia, Msitha na Marine, wajumbe wengine ni Suleiman Jabir, Boniface Tamba, Ameir Makame, Profesa Madundo Mtambo, Rona Lyimo na Hamad Abdallah.

Pia kuna Naima Shaame, Nehemia Mchechu, Oscar Milambo, Mwalim Mwalim, Patrick Kahemele, Baraka Shelukindo, Maximilian Iraghe na Joseph Muya.

Pia Meshack Anyingisye, Gerard Kihinga, Dk. Erasto Sylvania, Mhandisi Ngwisa Mpembe, Abel Phillip, Simon Patrick na Sixtus Mapunda.

Haya ndio majukumu ya LOC

Kamati ya Uratibu wa Maandalizi ya AFCON ni kama moyo wa mashindano hayo.

Majukumu ya kamati hiyo ni kama yanavyoainishwa hapa chini.

1. Kutumika kama kituo cha mawasiliano kwa Kamati Ndogo za LOC na kutoa msaada wa kitaalamu katika utekelezaji wa shughuli zilizopangwa za LOC.

2. ⁠Kuratibu na Kamati Ndogo za LOC kuhusu matokeo yanayotarajiwa (deliverables) yanayozingatia viwango vilivyowekwa.

3. ⁠Kufuatilia utekelezaji wa kazi chini ya Kamati Ndogo kwa kuzingatia mpango wa LOC na ramani ya CAF.

4. ⁠Kushiriki katika mikutano ya Kamati Ndogo ili kufuatilia maeneo muhimu ya matokeo.

5. Kusimamia, kuongoza na kutathmini wafanyakazi walio chini ya usimamizi ili kuhakikisha utekelezaji wa shughuli zilizopangwa kwa wakati.

6. ⁠Kusaidia Kamati Ndogo husika kuhakikisha mipango na uratibu wa kutosha kwa ajili ya matukio ya mashindano ili kuhakikisha mafanikio na uzoefu wa kukumbukwa kwa washiriki wote na watazamaji/mashabiki.

7. ⁠Kutumika kama kiunganishi na Kamati Ndogo husika katika kutekeleza taratibu za usalama na kuhakikisha uzingatiaji wa kanuni za afya na usalama.

8. ⁠Kushiriki katika mchakato wa upangaji na uandaaji wa bajeti kwa Sekretarieti.

9. ⁠Kuweka viwango vya utendaji na viashiria muhimu vya utendaji ili kutathmini mara kwa mara kiwango cha mafanikio na kubaini maeneo yanayohitaji kuboreshwa kwa LOC na Kamati zake Ndogo.

10. Kuhifadhi kumbukumbu sahihi za shughuli zote za uendeshaji, ikiwemo ratiba za timu, ripoti za mechi na mahudhurio ya wajitolea.

11. ⁠Kutumika kama kituo cha mawasiliano kwa timu, maafisa na wadau wengine kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati.

12. ⁠Kusimamia maandalizi na matengenezo ya viwanja pamoja na hali ya uwanja na miundombinu ya uwanja wa michezo.

13. ⁠Kusimamia mipango ya usafiri, malazi na usimamizi wa maeneo ya matukio.

14. ⁠Kusaidia Kamati Ndogo husika katika kuajiri, kutoa mafunzo na kusimamia wajitolea kusaidia katika majukumu mbalimbali kama msaada wa siku ya mechi, usimamizi wa vifaa na ukarimu.

15. ⁠Kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vinavyofanya kazi na vilivyo katika hali nzuri, ikiwemo mipira ya mechi, nguzo za magoli na vifaa vya tiba, miongoni mwa vingine.

16. ⁠Majukumu mengine yoyote yatakayopewa na CAF.