Timu 31 zatua anga la Simba

Muktasari:

  • Al Ahly ya Misri ndio mabingwa wa kihistoria wa mashindano ya Ligi ya Mabingwa wakiwa wametwaa taji hilo mara 10 wakifuatiwa na Zamalek iliyotwaa ubingwa mara tano

Timu 31 zimeungana na Simba kutinga hatua ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu ambayo itatoa washindi 16 watakaofuzu hatua ya makundi ya mashindano hayo.

Kuhitimishwa kwa raundi ya awali ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika jana kumefanya kutimia kwa idadi ya timu 32 zitakazosaka fursa muhimu ya kutinga hatua inayofuata ambayo imekuwa ni ndoto ya idadi kubwa ya klabu barani Afrika

Kati ya timu hizo 32, kumi ikiwemo Simba zilifuzu moja kwa moja hadi raundi ya kwanza kwa kubebwa na idadi kubwa ya pointi ilizokusanya kutokana na ushiriki mzuri kwenye mashindano ya klabu Afrika huku nyingine 22 zikitinga hatua hiyo baada ya kupenya katika raundi ya awali.

Timu 10 ambazo zilifuzu moja kwa moja ni Simba, Al Ahly na Zamalek (Misri), Wydad na Raja Casablanca (Morocco), Esperance na Etoile Du Sahel (Tunisia), Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini), TP Mazembe (DR Congo) pamoja na Horoya (Guinea)

Ukiondoa hizo zilizopenya moja kwa moja, nyingine 22 ambazo zimetinga hatua hiyo baada ya kupata matokeo mazuri katika mechi za hatua iliyopita ni ES Setif na CR Belouizdad za Algeria, Al Hilal na Al Merrikh (Sudan),Petro de Luanda na Sagrada Esperanca (Angola), Amazulu (Afrika Kusini), Tusker (Kenya), Gendarmarie (Niger), Zanaco (Zambia)  na Stade Malien (Mali)

Mbali na hizo pia kuna APR(Rwanda), AS Maniema (DR Congo), Jwaneng Galaxy (Botswana), Rivers United (Nigeria), AS Otoho (Congo), Nouadhibou (Mauritania), Royal Leopards (Eswatni), Al Ittihad (Libya) na LPRC Oilers (Liberia)