TRA yaikaba koo tena TFF

Mtendaji Mkuu wa TFF, Angetile Osiah
Muktasari:
Kutokana na hali hiyo, TFF ilipewa muda wa kuhakikisha wanalipa madeni yao jambo ambalo hata hivyo halikutekelezwa kama maelezo ya TRA yalivyotaka.
Dar es Salaam. Mamkala ya Mapato Tanzania (TRA), imeendelea kulibana Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), na safari hii imelikata kuanza mara moja kulipa deni la Sh573 milioni ambalo ni mjumuisho wa kodi mbalimbali.
Fedha hizo ni deni la miaka mitatu ya nyuma, ambazo ni kodi na mapato yatokanayo na viingilio vya mechi mbalimbali, kwa mujibu wa taarifa za ndani ilizozipata Mwananchi.
Taarifa zaidi zimeeleza kuwa, TRA tayari wameshaandika barua TFF kuitaarifu juu ya uamuzi huo na hatua zitakazochukuliwa iwapo watashindwa kutekeleza maelekezo hayo.
Barua hiyo inaitaka TFF kuanza kulipa limbikizo la deni hilo Jumatatu wiki ijayo, ingawa alipoulizwa Mtendaji Mkuu wa TFF, Angetile Osiah alisema hawajapata barua hiyo.
Kwa mujibu wa chanzo hicho cha habari, TRA ilibaini deni hilo kutokana na ukaguzi wa hesabu walioufanya TFF mwaka huu na kukuta kuna madeni ya kodi (PAYE) na ongezeko la thamani (VAT).
Kutokana na hali hiyo, TFF ilipewa muda wa kuhakikisha wanalipa madeni yao jambo ambalo hata hivyo halikutekelezwa kama maelezo ya TRA yalivyotaka.
Kwa mujibu wa habari hizo za ndani, TRA imeitaka kulipa madeni yake kama maelekezo yanavyotaka na kwamba, kinyume na agizo hilo itatumia wakala wa udalali kukamata mali za TFF na kuzipiga bei.
“Wameambiwa wasipofanya hivyo katika muda waliopewa, basi TRA watawatumia madalali wa Majengo kwenda kukamata mali za shirikisho hilo na kuzipiga bei kufidia deni hilo,” alisema mtoa habari huyo.
Hii siyo mara ya kwanza kwa TRA kuibana TFF kuhusu ulipaji wa kodi, kwani mwaka jana taasisi hiyo ya kukusanya kodi ilizuia akaunti za TFF ikiitaka kulipa kodi.
Hatua ya kuzuia akaunti hizo ilikuja baada ya TRA kutaka kulipwa kiasi cha Sh157 milioni ambazo ni makato katika mishahara ya makocha wa timu ya taifa, yaani Taifa Stars.
Makato hayo ni tangu wakati Kocha raia wa Brazil, Marcio Maximo ambaye alikuwa wa kwanza kuletwa na Serikali, kabla ya kumaliza mkataba na kisha kuja Kim Poulsen.
Kutokana na hali hiyo, TFF iliomba msaada wa Serikali ambao kimsingi ndiyo walikuwa na jukumu la kulipa kodi hiyo kwa vile ndiyo pia walikuwa walipaji wa mishahara ya makocha.
Naibu Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, Amos Makala aliwahi kusema kuwa suala hilo limefikia pazuri baada ya kupelekwa ngazi nyingine ya uamuzi.
Mwananchi ilimtafuta Ofisa Uhusiano wa TRA, Oliver Njunwa kuhusu suala hilo na alisema: “Sifahamu lolote kuhusu habari hiyo na hata kama ningefahamu kitu, sina mamlaka ya kuzungumza ila bosi wangu.”