Uongozi Man United wamtega Erik ten Hag
Muktasari:
- Mdachi huyo yupo kwenye presha kubwa huko Old Trafford baada ya kuwa na mwanzo wa hovyo wa msimu huu wa 2024-25.
England. Kimenuka, Kocha, Erik ten Hag ameripotiwa kupewa mechi mbili tu za kuokoa kibarua chake Manchester United.
Mdachi huyo yupo kwenye presha kubwa huko Old Trafford baada ya kuwa na mwanzo wa hovyo wa msimu huu wa 2024-25.
Msimu wa Man United unatoka kwenye hali mbaya na kuwa taabani baada ya kipigo cha mabao 3-0 nyumbani uwanjani Old Trafford kwenye mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Tottenham Hotspur, juzi Jumapili.
Mashabiki wengi waliokuwapo uwanjani Old Trafford waliimba nyimbo za kumtaka Ten Hag afukuzwe, wakati wakishuhudia timu yao ikishuka hadi nafasi ya 12 kwenye msimamo wa Ligi Kuu England baada ya kuvuna pointi saba kwenye mechi sita.
Lakini, ripoti zinafichua kocha huyo wa zamani wa Ajax ataendelea kubaki kwenye kikosi hicho hadi wikiendi, akiwa na kazi ya kuiongoza Man United kwenye mechi ya Europa League dhidi ya FC Porto na Aston Villa kwenye Ligi Kuu England.
Man United itakipiga na miamba hiyo ya Primeira Liga, Porto - Alhamisi. Iliangusha pointi kwenye mechi ya kwanza ilipotoa sare na FC Twente kwenye mchezo wao wa kwanza wa Europa League uliofanyika uwanjani Old Trafford.
Baada ya mechi hiyo, Man United itakipiga na Aston Villa ugenini kwenye uwanja wa Villa Park, Jumapili - mechi ya lazima kushinda.
Na mbaya zaidi kwenye mechi hiyo, Ten Hag hatakuwa na huduma ya nahodha wake Bruno Fernandes na kiungo Kobbie Mainoo.
Fernandes alionyeshwa kadi nyekundu ya moja kwa moja juzi baada ya kumchezea rafu James Maddison, wakati alipoteleza na kumkanyaga kwenye ugoko.
Wakati huo, kiungo mwenzake, Mainoo alilazimika kutolewa uwanjani kwenye kipindi cha kwanza kutokana na kuwa majeruhi.
Ten Hag alikiri baada ya mechi hiyo ana wasiwasi wa kuhusu majeraha ya Mainoo, aliposema: “Siwezi kusema kitu kwa sasa. Nasubiri kupata majibu, kwa sababu mchezaji anapotoka uwanjani wakati wa mapumziko akiwa majeruhi lazima uwe na wasiwasi.”
Kocha huyo Mdachi aliulizwa kama ana wasiwasi wowote wa sasa wa kuhusu kupoteza ajira yake huko Man United kutokana na timu kupata matokeo mabovu, akajibu kwamba bado yupo yupo sana Old Trafford.
Alisema: “Sifikirii hilo. Sote tulifanya uamuzi kwenye majira ya kiangazi ya kuwa pamoja kuanzia mmiliki na viongozi. Tulifanya uamuzi pia namna tunavyoweza kuboresha timu na vile tunavyotaka kujenga kikosi chetu. Tunafahamu wazi hilo linahitaji muda, usajili umekwendaje, baadhi ya wachezaji wamechelewa kama (Manuel) Ugarte. Pia ni lazima tuboreshe idara zetu muhimu, bado tuna majeruhi, tunahitaji muda. Sote tunasafiri kwa jahazi moja, mmiliki, uongozi na wachezaji. Hivyo sina wasiwasi.”
Lakini, pointi saba kwenye mechi sita amefikiria kwenye rekodi za hovyo kama kilivyokuwa kipindi cha makocha David Moyes na Ole Gunnar Solskjaer na kufutwa kazi, walipokuwa na mwanzo mbaya kwenye kikosi hicho tangu mwaka 1989.
Na wakati Ten Hag akisisitiza kwamba wala hana wasiwasi wa kufutwa kazi, mastaa wa zamani Gary Neville, Rio Ferdinand, Ashley Young na Jamie Redknapp hawakutaka kupepesha macho na kuanza kukosoa kiwango cha Man United cha ndani ya uwanja.
Neville, ambaye ni nahodha wa zamani wa Man United alisema timu hiyo inashangaza na imekuwa ya hovyo, aliposema: “Kipindi cha kwanza kilikuwa hovyo. Hii ilikuwa siku ya kushangaza, hovyo kabisa. Hii ni mbaya sana kwa Ten Hag. Hakika wamenishangaza kwa namna wanavyokwenda chini.”
Kiungo wa zamani wa Liverpool na Tottenham, Redknapp alikiri kumwonea huruma Ten Hag kutokana na udhalilishwaji aliokutana nao kwenye mechi hiyo.
“Inafikia wakati unamwonea huruma kocha. Alionekana kuishiwa mbinu kabisa, alishindwa kabisa kuwahamasisha wachezaji wake kupambana. Man United na Ten Hag inarudi nyuma kwa kasi. Huwezi kuelezea zaidi, amepata mabeki wote aliotaka, amepewa wachezaji wa kutosha - hana cha kujitetea.
“Wanaonekana kujichimbia chini. Huoni atakwenda wapi kutoka hapa. Wamekuwa hovyo kwa namna ninavyowaona Man United wakicheza.
“Ni aibu sana. Klabu yenye hadhi kama hii haiwezi kucheza kwa kiwango kile.”
Staa wa zamani wa Man United, Ashley Young aliongeza: “Man United haikujitoa kwa kila kitu uwanjani. Hawakuwa na jitihada.”
Mshindi mara tano wa Ligi Kuu England, Rio Ferdinand alitumia chaneli yake ya YouTube na kuzungumzia kiwango cha Man United, akisema: “Hakika ni kiwango cha hovyo sana, niwe mkweli. Walikuwa hovyo, hawajui wafanye nini na hawapambani. Kipindi cha pili walijaribu kupambana hapa na pale, lakini hawakuwa na ubora kabisa.”