Uraia wawakwamisha Akpan, Okwa kuingia Dubai

Muktasari:

  • Okwa alisema si kama amebaki Dar, kuna jambo lingine linaweza kuendelea dhidi yake bali ameshindwa kuingia Dubai kutokana na kuna shida ya mambo ya kisiasa hadi raia wa Nigeria kuzuiliwa kuingia.

KIKOSI cha Simba kinaendelea na mazoezi jijini Dubai kwenye kambi ya wiki moja ya kujiandaa na mechi za Ligi Kuu Bara, Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho (ASFC), huku nyota wake wawili kutoka Nigeria, Nelson Okwa na Vincent Akpan wakikwama kuambatana na msafara wa timu.
Okwa na Akpan wameshindwa kuondoka na timu kwa sababu ya marufuku iliyowekwa Dubai dhidi ya raia wa Nigeria, huku beki wa kati Henock Inonga akishindwa naye kuondoka na timu hiyo kwa vile yupo kwao DR Congo anakojiuguza jeraha alilopata katika mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Prisons.
Umoja wa Falme za Kiarabu, uliwekwa sheria miezi miwili iliyopita wa kuzuia raia yeyote kutoka Nigeria kupata viza, kitu kilichowakwamisha nyota hao ambao wamepewa programu maalumu ya kujifua jijini Dar es Salaam, wakati wenzao wakijifua Dubai kabla ya kuungana mara timu itakaporejea toka kambi hiyo ya wiki moja Umangani.
Kocha wa viungo kutoka Sauzi, Kelvin Mandla ndiye aliyewapa programu maalumu ya mazoezi wanayotakiwa kufanya kazi hadi timu ikirejea wakitakiwa kufanya mazoezi kwa siku, kukimbia kwenye lami pamoja na yale ya gym ili wawe sawa utimamu wa mwili na kama wenzao wa Dubai.
Okwa alisema si kama amebaki Dar, kuna jambo lingine linaweza kuendelea dhidi yake bali ameshindwa kuingia Dubai kutokana na kuna shida ya mambo ya kisiasa hadi raia wa Nigeria kuzuiliwa kuingia.
"Timu ikirejea nitaungana na wenzangu kwa ajili ya maandalizi mengine ila wakati huu kocha wa viungo kuna ratiba ya mazoezi ametuachia tunafakiwa kufanya asubuhi na jioni ili mwili kuendelea kuwa sawa kwenye hali ya ushindani," alisema Okwa, huku Akpan akisema; "Shida aliyokutana nayo Okwa ndio hiyo hiyo ipo upande wangu, ila nikuhakikishie nipo Simba na wala sitakwenda kokote kwa wakati huu."