Utamu wa namba Kombe la Dunia 2026
Ufunguzi rasmi wa Fainali za Kombe la Dunia 2026 unatarajiwa kufanyika Alhamisi, Juni 11, 2026 kwa mechi baina ya wenyeji wenza, Mexico dhidi ya Afrika Kusini.
Mchezo huo umepangwa kuchezwa katika Uwanja wa Azteca jijini Mexico City, saa 4:00 usiku kwa muda wa Afrika Mashariki.
Zikiwa zimebaki siku tatu tu ili tukio hilo kubwa la soka duniani lianze, Spoti Mikiki inakuletea namba zinazobeba dondoo mbalimbali muhimu kuhusu nchi, timu, makocha na wachezaji mbalimbali ambao watashiriki mashindano hayo mwaka huu.
Ni mara ya tatu kwa Mexico kuandaa Fainali za Kombe la Dunia na hivyo inaweka rekodi ya kuwa nchi iliyoandaa mara nyingi zaidi mashindano hayo.
Kabla ya mwaka huu ambao Mexico ni muandaaji mwenza, nchi hiyo pia imewahi kuandaa mwaka 1970 na 1986.
Nchi iliyoshiriki mara nyingi zaidi fainali za Kombe la Dunia ni Brazi ambayo mwaka huu itakuwa inashiriki kwa mara ya tatu.
Inayofuatia ni Ujerumani ambayo hii ni mara ya 21 kwake kushiriki Kombe la Dunia na nafasi ya tatu ipo Argentina inayoshiriki mara ya 19.
Qatar na Saudi Arabia ndizo timu zenye idadi kubwa zaidi ya wachezaji wanaocheza katika ligi za ndani za nchi zao, zikiwa na wachezaji 25 kila moja.
Wachezaji pekee wanaocheza nje ya nchi katika vikosi vyao ni beki wa kushoto wa Qatar, Homam Ahmed, anachezea Cultural Leonesa ya Hispania na beki wa kulia wa Saudi Arabia, Saud Abdulhamid, anayeitumikia RC Lens ya Ufaransa.
Nchi za Cape Verde, DR Congo, Ivory Coast, Curaçao, Senegal na Uruguay hazina hata mchezaji mmoja anayechezea klabu ya soka iliyoko ndani ya mipaka ya nchi zao.
Kiungo mshambuliaji wa Panama, Cesar Yanis, ndiye mchezaji mfupi zaidi akiwa na kimo cha mita 1.60.
Anafuatiwa na mshambuliaji wa Curaçao, Jeremy Antonisse, mwenye kimo cha mita 1.64.
Kipa wa Austria, Florian Wiegele, mwenye kimo cha mita 2.05, ndiye mchezaji mrefu zaidi kuwahi kujumuishwa katika kikosi cha Kombe la Dunia.
Rekodi hiyo hapo awali ilikuwa ikishikiliwa na kipa wa Uholanzi, Andries Noppert, mwenye kimo cha mita 2.03, katika fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Qatar 2022.
Wachezaji wengine warefu zaidi katika fainali za Kombe la Dunia 2026 ni beki wa England Dan Burn (mita 2.01), kipa wa Colombia Alvaro Montero (mita 2.01), na beki wa kati wa Bosnia na Herzegovina Stjepan Radeljic (mita 2.01).
Lionel Messi, Guillermo Ochoa na Cristiano Ronaldo watashiriki Kombe la Dunia kwa mara ya sita, jambo ambalo ni rekodi mpya.
Hapo awali walikuwa wakishiriki rekodi ya kucheza matoleo matano ya Kombe la Dunia pamoja na Antonio Carbajal, Lothar Matthäus, Gigi Buffon, Rafa Márquez na Andrés Guardado.
Kwa upande mwingine, Luka Modrić, Yuto Nagatomo na Manuel Neuer watakuwa wakishiriki Kombe la Dunia kwa mara ya tano katika fainali za sasa.
Messi na Ronaldo watakuwa wachezaji wa kwanza kuwahi kucheza katika mechi za Kombe la Dunia katika matoleo sita tofauti, tofauti na Ochoa ambaye alishindwa kucheza hata mechi moja katika Kombe la Dunia la Ujerumani 2006 na Afrika Kusini 2010 licha ya kujumuishwa kwenye kikosi cha timu yake.
Gilberto Mora ndiye mchezaji mwenye umri mdogo zaidi katika Fainali za Kombe la Dunia 2026 akiwa na umri wa miaka 17.
Ni mchezaji wa sita kuwahi kucheza mashindano hayo akiwa na umri mdogo wa miaka 17 ambapo anafuata nyayo za Pele, Salomon Olembe, Femi Opabunmi, Samuel Eto’o na Norman Whiteside.
Manchester City, ikiwa na wachezaji 19, ndiyo klabu yenye uwakilishi mkubwa zaidi katika Kombe la Dunia 2026.
Wachezaji wa klabu hiyo wamejumuishwa katika vikosi vya Algeria, Ubelgiji, Croatia, Misri, England, Ufaransa, Ghana, Uholanzi, Norway, Ureno, Hispania na Uzbekistan.
Klabu zinazofuatia kwa kuwa na idadi kubwa ya wachezaji katika mashindano hayo ni Bayern Munich (wachezaji 18), Arsenal (16), PSG(16), Barcelona (15), Al Hilal (12), Atletico Madrid (12), Crystal Palace (12), Manchester United (12), Borussia Dortmund (11), Galatasaray (11) na Liverpool (11).
Kati ya wachezaji watakaoshiriki Kombe la Dunia mwaka huu, Lionel Messi ndio mchezaji mwenye mabao mengi zaidi katika mashindano hayo akiwa amepachika mabao 13.
Anafuatiwa na Kylian Mbappe (12), Harry Kane (8), Neymar (8) na Cristiano Ronaldo (8).
Ikumbukwe mchezaji anayeshikilia rekodi ya kufunga idadi kubwa zaidi ya mabao kwenye Kombe la Dunia ni Miloslav Klose ambaye aliwahi kuifungia Ujerumani mabao 16.
Kipa wa Scotland mwenye umri wa miaka 43, Craig Gordon, ndiye mchezaji wa pili mwenye umri mkubwa zaidi kuwahi kushiriki Kombe la Dunia.
Mchezaji pekee aliyekuwa na umri mkubwa zaidi kuliko yeye ni kipa wa Misri, Essam El Hadary, ambaye alikuwa na umri wa miaka 45 wakati wa Kombe la Dunia lililofanyika Russia mwaka 2018.