Utu Kwanza Tribe yaanzisha matembezi, mbio kwa ajili ya misaada ya kisheria
Mwenyekiti wa Utu Kwanza, Shehzada Walli (kushoto) akizungumza na Mgeni wa heshima katika hafla hiyo, aliyekuwa Rais wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), Ibrahim Razza.
Muktasari:
- Kwa mujibu wa waandaaji, ushiriki katika matembezi na mbio za Utu Kwanza Tribe ni bure, huku wananchi wakihimizwa kujitokeza kwa wingi na kuwa sehemu ya harakati za kuunganisha afya, utu na maendeleo ya jamii.
Dar es Salaam. Taasisi ya Utu Kwanza imezindua rasmi programu mpya ya matembezi na mbio ijulikanayo kama Utu Kwanza Tribe, yenye lengo la kuhamasisha afya, mshikamano wa jamii na kukusanya fedha za kusaidia huduma za misaada ya kisheria kwa wananchi wasio na uwezo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa programu hiyo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Utu Kwanza, Shehzada Walli, amesema kuwa mpango huo utakuwa ukifanyika kila Jumamosi asubuhi na utawakutanisha wananchi kutoka makundi mbalimbali ya kijamii, taasisi, kampuni binafsi, vilabu vya riadha na jumuiya za kidini.
Walli amesema Utu Kwanza Tribe siyo klabu ya kawaida ya matembezi au mbio, bali ni jukwaa la kuunganisha watu kwa ajili ya kutanguliza utu na kusaidia wananchi wanaohitaji msaada wa kisheria kupitia madawati ya huduma yaliyopo katika Mahakama ya Kisutu, Mahakama za Wilaya na Mahakama za Mwanzo.
“Lengo letu ni kuileta jamii pamoja na kueneza ujumbe wa utu. Kila mtu anayeshiriki matembezi au mbio hizi anakuwa amechangia kwa namna moja au nyingine kusaidia mwananchi anayehitaji msaada wa kisheria,” amesema Walli.
Ameeleza kuwa programu hiyo imevutia wadhamini mbalimbali wa fedha na huduma, akiwemo mdhamini mkuu Shehzada Walli mwenyewe pamoja na kampuni za Skylink Tanzania, Advent Construction na Ron Thornton ambazo zimechangia fedha za kuendesha shughuli hizo.
Walli amesema matembezi na mbio za kwanza zitafanyika Juni 13 mwaka huu zikianzia Hoteli ya Crowne Plaza kuanzia saa 12 asubuhi, huku washiriki wakipewa uchaguzi wa kutembea au kukimbia kilomita tano au nane kulingana na uwezo wao.
“Kila Jumamosi kutakuwa na mandhari maalumu ya shughuli husika. Tunataka washiriki wasifurahie tu mazoezi bali pia wapate nafasi ya kujifunza, kuburudika na kujenga mitandao ya kijamii na kikazi,” amesema.
Katika uzinduzi huo, viongozi na wanachama wa vilabu mbalimbali vya riadha walihudhuria kuonesha mshikamano wao. Miongoni mwao ni wawakilishi wa Goba Runners, Runners Tanzania, Running Lovers na makundi mengine yanayojihusisha na michezo ya kukimbia na kuendesha baiskeli.
Walli amesisitiza kuwa Utu Kwanza Tribe haiji kushindana na vilabu vya riadha vilivyopo bali kushirikiana navyo katika kuendeleza utamaduni wa mazoezi na kuchangia maendeleo ya jamii.
Mbali na matembezi ya kila wiki, taasisi hiyo pia imeendelea kuandaa mbio za masafa marefu za Utu Kwanza Run ambazo zimefanyika kwa miaka mitatu mfululizo. Awali mbio hizo zilikuwa zikifanyika kutoka Bagamoyo hadi Dar es Salaam kwa umbali wa kilomita 60.
Mwaka huu, mbio hizo zinatarajiwa kufanyika Zanzibar Septemba 6, ambapo washiriki watakuwa na chaguo la kukimbia kilomita 60, 30, 10 au tano kulingana na uwezo wao.
Walli amesema hatua ya kuhamishia mbio hizo Zanzibar inalenga kuunga mkono juhudi za Serikali za kuendeleza utalii wa michezo na kuitangaza Zanzibar kimataifa kama kitovu cha matukio ya michezo.
“Tumeingia ubia na Skylink Tanzania ambao kwa kushirikiana na FCM Travel wataisaidia kuitangaza Utu Kwanza Run duniani kote. Tunataka kuvutia washiriki kutoka ndani na nje ya nchi huku tukichangia ukuaji wa utalii wa michezo,” amesema.
Mgeni wa heshima katika hafla hiyo, aliyekuwa Rais wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), Ibrahim Razza, ameipongeza Utu Kwanza kwa kuanzisha mradi huo akisema utasaidia wananchi wengi wanaokumbana na changamoto za kisheria na kijamii.
Razza amesema si kila Mtanzania ana uwezo wa kumudu gharama za uwakili au kupata ushauri wa kisheria kwa wakati, hivyo uwepo wa taasisi kama Utu Kwanza ni hatua muhimu katika kuhakikisha haki inapatikana kwa wote.
Ametoa wito kwa wadau mbalimbali kuendelea kuunga mkono jitihada hizo ili wananchi wengi zaidi wanufaike na huduma za misaada ya kisheria huku wakihamasishwa kujenga afya kupitia michezo na mazoezi.
Kwa mujibu wa waandaaji, ushiriki katika matembezi na mbio za Utu Kwanza Tribe ni bure, huku wananchi wakihimizwa kujitokeza kwa wingi na kuwa sehemu ya harakati za kuunganisha afya, utu na maendeleo ya jamii.