Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Uviko-19 ilivyokatisha safari ya Mpepo kwenda Ulaya

Mshambuliaji wa KMC, Eleuter Mpepo.

Muktasari:

  • Mpepo ambaye alianza kupenda soka tangu mdogo, alicheza katika vituo kadhaa vya kukuza vipaji jijini Mbeya

Dar es Salaam. Ni fahari kwa Taifa kuwa na nyota wengi wanaokipiga ligi za Ulaya. Lakini haikuwa bahati kwa mshambuliaji wa KMC, Eleuter Mpepo ambaye safari yake ilikatishwa ukingoni baada ya kuibuka kwa ugonjwa wa Uviko-19.

Akizungumza na Mwananchi, Mpepo alithibitisha jambo hilo kuwa ni miongoni mwa changamoto ambayo hawezi kuisahau katika safari yake ya soka.

“Changamoto zipo nyingi, nakumbuka wakati nipo Zambia nikawa nimepata timu Ureno nikasaini mkataba wa miaka mitano kupitia Shadaka Sports Management lakini nikapelekwa kwa mkopo Msumbiji maana ilikuwa dirisha dogo kwa hiyo ikabidi nimalizie miezi sita kwenye timu inaitwa Costal do sol ndio walikuwa mabingwa kule.

“Kwa kuwa nafasi yangu kuna mchezaji ndio alikuwa anamaliza mkataba, nikawa nafanya vizuri sana kwenye ile timu ghafla COVID-19 ikaharibu kila kitu, ilikuwa noma sana aise kichwa kilikuwa kinauma,” alisema Mpepo.

Mshambuliaji huyo hakuishia hapo kwani alitaja changamoto nyingine ambayo ilimfanya akae nje ya uwanja kwa miezi sita jambo ambalo pia lilimfanya apate wakati mgumu.

“Changamoto yingine nikuchana nyama ya paja nikiwa Angola ile ilikuwa mbaya sana iliniweka nje miezi sita nikaamua kurudi home ‘nyumbani’,” alielezea kwa masikitiko.

Mshambuliaji wa KMC, Eleuter Mpepo.


Kujiunga KMC

Mpepo aliyetamba na timu mbalimbali za Ligi Kuu Bara ikiwamo Mtibwa Sugar, baada ya kukaa nje kwa miezi sita akiuguza majeraha alijiunga na Singida Black Stars katika dirisha dogo la Januari 2025, akitokea Trident ya Zambia.

Hata hivyo, mshambuliaji huyo hakuweza kudumu kwenye kikosi cha Walima Alizeti hao wa Singida kutokana na ushindani mkubwa wa namba uliopo na hivyo ikambidi aondoke na kujiunga KMC.

Mpepo alisema licha ya kuwa aliwekewa ofa na timu tatu za Ligi Kuu lakini mwenyewe aliamua kutua KMC kutokana na shauku ya kufanya kazi na aliyekuwa kocha wa timu hiyo Abdallah Bales.

“Nikiwa niko nyumbani baada ya kuomba kuondoka Singida mwezi wa kumi nilipigiwa simu yakuwa inatakiwa nijiunge KMC kutoka kwa baadhi ya viongozi kupitia kwa kaka zangu Gidion na Shiraz.

“Ingawa nilikuwa na ofa nyingine tatu hivi, shauku yangu zaidi ilikuwa ni mwalimu Abdallah Bales ndio sababu kubwa sikujali nafasi waliopo kwakuwa niliamini juu ya uwezo wangu yakuwa ntaongeza nguvu na wenzangu waliokuwepo tangu mwanzo pengine tunaweza kufanya jambo kubwa pamoja,” alisema mshambuliaji hoyo.

Mshambuliaji wa KMC, Eleuter Mpepo wakati alipokuwa Singida Black Stars


Alichokisema kuhusu Singida BS

Akiwazungumzia waajili wake wa zamani Singida Black Stars, mshambuliaji huyo alisema, Singida ni timu nzuri yenye wachezaji bora lakini licha ya kutopata nafasi ya kutosha bado alijifunza kitu kutoka kwao.

“Ni timu nzuri sana nilitegemea kwenda kufanya vizuri kwakuwa timu ina mchanganyiko wa wachezaji bora wazawa na wageni lakini mpira ulivyo nitofauti tunavyouzungumza, sikuweza kupata muda wa kucheza navingine havikuwa sawa ikanibidi niombe kuondoka.  

“Nilichojifunza kutokana nao nikuwa kunanyakati utapata pesa hutopata gametime (muda wa kucheza) na kunawakati utapata gametime na hutopata pesa lakini pia unaweza usipate vyote yani usipate nafasi ya kucheza na pesa usipate, ndio safari ya mpira ilivyo”, alisema Mpepo kwa kicheko cha maskitiko.

Mshambuliaji wa KMC, Eleuter Mpepo wakati alipokuwa Singida Black Stars


Alivyopambania nafasi akiwa nje

Mpepo aliyecheza pia Tanzania Prisons, Singida United na Mbeya Kwanza zote za Tanzania, lakini pia alitaja ugumu aliopitia alipokuwa akicheza soka nje ya nchi ambapo alichezea Vilabu vya Buildcon ya Zambia, Cape Umoya United ya Afrika Kusini na Interclube ya Angola.

Katika safari yake akiwa nje ya nchi kupambania ndoto zake, mshambuliaji huyo alisema kuwa mbali na nyumbani kulimpa nguvu ya kupambana licha ya kukutana na magumu ya hapa na pale lakini alihakikisha anavuka na kwenda hatua nyingine.

“Kuwa mbali na nyumbani kunakupa nguvu ya kupambana kwa kuwa hakuna atakaye kuonea huruma pia nafasi yako ni dhahabu kila mtu anaitaka huna budi kuikumbatia kwa hali na mali.

“Kucheza nje kumenisaidia ushindani na uimara kupambana na changamoto tofauti tofauti zinazohusu kazi hii ya mpira lakini pia kuwa bora kwenye maeneo mengi ndani ya uwanja,” alisema nyota huyo wa KMC huku akiongezea kwa kuonyesha utofauti wa ligi ya Tanzania na ligi nyingine ambazo amewahi kucheza. Anasema;

“Nje ya Tanzania watu hawajali wageni wanajali sana watu wao tofauti na Tanzania tunawajali wageni kuliko wazawa, makosa ya mzawa yanashadadiwa wakati ya mgeni yanafichwa fichwa, nje ni tofauti mgeni ukikosea kazi unayo, mzawa anabebwa kwa kuwa wanamuhitaji national team (timu ya Taifa) hawahitaji kuharibu saikolojia yake kivyovyote vile,” alieleza Mpepo.

Mpepo ambaye alianza kupenda soka tangu mdogo, alicheza katika vituo kadhaa vya kukuza vipaji jijini Mbeya kama anavyoeleza mwenyewe;

Mshambuliaji wa KMC, Eleuter Mpepo wakati alipokuwa akijaribu kuwapita wachezaji wa Simba kwenye mechi ya Ligi Kuu.

“Ukuaji wangu mzima umekuwa niwakupenda soka. Shule ya msingi nimekuwa mchezaji bora, secondary mpaka chuo. Nimekulia friends ranger chini ya kocha Herry Mzozo.

“Mbeya kwanza ikaniendeleza safari chini ya kocha Shiraz Batchu, kisha Tanzania prisons chini ya kocha Abdallah Bales ikanitambulisha Ligi kuu kupitia juniors team ‘timu ya vijana, ‘ alisema mshambuliaji huyo alipokuwa akielezea maisha ya ukuaji wake wa soka.

Nje ya uwanja, kitu kingine anachopenda kukifanya Mpepo ni biashara pamoja na kuigiza.

“Napenda kufanya biashara na nafanya biashara, pia napenda kuwa actor ‘muigizaji’ kwani maranyingi niko karibu na Mliro napenda sana kufanya ile kazi, “ alieleza Mpepo.

Tangu ajiunge na KMC bado mshambuliaji huyo ajabahatika kutikisa nyavu katika Ligi Kuu huku akiwa na kibarua cha kuisaidia timu yake isishuke daraja kwani hadi sasa inaburuza mkia katika msimamo wa Ligi Kuu Bara.