Wadau wanavyomkumbuka Hans Pope

Muktasari:

  • Wafanyabiashara na wadau wa michezo wamemzungumzia mdau mwenzao, Zacharia Hans Poppe, aliyefariki dunia juzi usiku wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salam.

Dar es Salaam. Wafanyabiashara na wadau wa michezo wamemzungumzia mdau mwenzao, Zacharia Hans Poppe, aliyefariki dunia juzi usiku wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salam.

Mkurugenzi wa Taasisi Binafsi Tanzania (TPSF), Francis Nanai alisema jumuiya ya wafanyabiashara na wawekezaji, imepoteza mtu muhimu ambaye anapaswa kuenziwa kwa mazuri aliyokuwa akiyafanya.

“Sisi wafanyabiashara na wawekezaji tunaungana na Watanzania wengine kumuombea apumzike kwa amani. Sisi watu wa sekta binafsi tumepoteza mwekezaji mkubwa, lakini kwa Wanasimba wamepoteza mwanachama na shabiki kindakindaki,” alisema Nanai.

Alisema namna nzuri ya kumuenzi Hans Poppe ni ndugu na washirika wake wa kibiashara, kuhakikisha biashara zake zinaendelea; zisife kwa kuwa ameondoka.

“Biashara alizoziacha zimetoa ajira, zinategemewa na watu wengi na zinalipa kodi kwa Serikali,” alisema.

Mkuu wa operesheni wa Chama cha Wasafirishaji (TAT) Hussein Wandwi, alisema kifo cha Hans Poppe ni pigo kubwa kwa sekta yao, kwa kuwa alikuwa anayajua vyema masuala ya mafuta na usafirishaji.

“Alikuwa Rais wetu na mwanzilishi wa TAT mwenye maono ya mbali,” alisema Wandwi na kuongeza kuwa wadau wa sekta ya uchukuzi watamkumbuka sana.

Msemaji wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tatoa) Raheem Dosa, alisema wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kuondokewa na mwanachama wao, ambaye yeye kwa kiasi kikubwa alikuwa akisafirisha mafuta kwenda nchi za Zambia, Burundi, Rwanda DR Congo na ndani ya nchi.

“Wanachama wa Tatoa wote kupitia makundi mbalimbali wamesikitishwa na kifo cha mwenzao huyu, ambaye ni miongoni mwa wasafirishaji wakubwa hapa nchini; alikuwa ni mtu mwema sana,” alisema Dosa akimuelezea Hans Poppe, ambaye alikuwa na mamia ya malori yaliyokuwa yakifanya shughuli za usafirishaji.

Dosa alisema wakati wa uhai wake, Hans Poppe alikuwa kinara wa kupaza sauti pindi alipokuwa akiona mambo hayaendi vizuri.

‘‘Alikuwa msema kweli bila kuogopa jambo lolote, alikuwa mtu mahiri sana aliyekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya chama chetu,’’ alisema.

Naye mfanyabiashara Mohammed Dewji (Mo) alimzungumzia Hans Poppe, akisema kuwa amefanya naye kazi kwa miaka mingi, na kila siku alikuwa akitanguliza mbele maslahi ya Simba.

“Kaka yangu ulikuwa na wema wa kipekee, na ulikuwa wa kwanza na ulinyooka linapokuja suala la kuilinda Simba, hukuwa na maslahi binafsi. Ulikuwa rafiki wa marafiki wa Simba, na ulikuwa tofauti na wasioitakia mema Simba, Nitakukumbuka sana,” aliandika Mo katika ukurasa wake wa Twitter.

Aliongeza kusema kuwa moyo wake una maumivu makali na bado ni vigumu kwake kukubali kwamba Hans Pope amefariki, huku akitoa pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na wanachama wa klabu ya Simba.

“Kaka yangu, umetangulia nasi tutafuata. Nitakukumbuka sana kaka yangu. Natoa pole sana kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki, pamoja na wanafamilia wote na mashabiki wa Simba kwa kumpoteza ndugu yetu...” aliandika Mo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba.


Simba yasikitika

Baada ya taarifa za kufariki kwa Hans Poppe, uongozi wa klabu ya Simba ulitoa taarifa ya kuelezea masikitiko yake kufuatia msiba huo, huku ikisema wamepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za kifo cha mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi.

“Ninamfahamu kwa miaka mingi akiwa ni mwana-Simba mahiri, mwenye msimamo na ukweli. Ni mtu aliyependa umoja na kupata mafanikio kwa jumla. Siku zote alikubali kutumikia klabu kwa moyo wake wote bila kujali muda wake, mali au hasara,” alisema Mwenyekiti wa klabu hiyo, Murtaza Mangungu.

Klabu ya Yanga nayo ilituma salamu za rambirambi kwa uongozi wa TFF, Simba, familia, mashabiki, ndugu, jamaa na wanamichezo wote nchini.

“Uongozi wa klabu ya Yanga umepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha mjumbe wa Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji TFF na kiongozi wa Simba SC, ndugu Zacharia Hans Poppe,” ilieleza taarifa ya Yanga.