Wajumbe wagomea matokeo uchaguzi TOC, ulinzi waimarishwa
Kutoka kushoto, Anthony Mtaka, Henry Tandau na Leonard Thadeo waliokuwa wakichuana kusaka urais wa TOC.
Muktasari:
- Uchaguzi huo uliahirishwa mara tatu kufuatia kuenguliwa kwa baadhi ya wagombea akiwamo Mtaka, kabla ya makubaliano ya TOC, Serikali na Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) kuwarejesha wiki iliyopita na kuamuliwa uchaguzi ufanyike leo Julai 5, 2026.
Dar es Salaam. Hali ya sintofahamu imeibuka kwenye uchaguzi w Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) baada ya mwenyekiti wa uchaguzi kutangaza matokeo yaliyogomewa na wajumbe.
Awali mchuano mkali kwenye nafasi ya urais ulikuwa kwa ulikuwa kwa Antony Mtaka, mkuu wa mkoa wa Njombe na Henry Tandau aliyekuwa makamu mwenyekiti wa TOC.
Hata hivyo sintofahamu ilitokea baada ya Leonard Thadeo kutangazwa ndiye mshindii, huku zogo likisikika ndani ya chumba cha uchaguzi.
Wakati wa kutangaza matokeo, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Uchaguzi huo, Ibrahim Mkwawa aliwafukuza waandishi wa habari na kueleza kwamba mkutano huo ni wa wajumbe wa TOC huku polisi sita, wawili wakiwa na silaha za moto wakiimarisha ulinzi.
Waandishi wakiwa nje, Mkwawa na makamu wake, Maharagwe Mchungahela walitoka kwenye chumba cha mkutano na kuondoka, kabla ya wajumbe kuanza kupiga kelele wakidai kilichotangazwa si kile ambacho wao wamekichagua.
Wajumbe hao walitoka nje na kusimama vikundi vikundi, wakihoji uhalali wa Thadeo ambaye wakati wa kuhesabu kura alionekana kupata kura moja kutangazwa ndiye mshindi.
Waliokuwa mawakala wa wagombea walidai Thadeo alipata kura moja, Tandau kura Saba na Mtaka kura 29, lakini wakati wa kutangaza imekuwa kinyume nyume.
Mkwawa alipoulizwa na Mwananchi kuhusu matokeo hayo, alisema kuna simu ya muhimu anazungumza nayo na kutokomea kusikojulikana.
Huku ulinzi wa polisi wenye silaha za moto ukiwa umeimarishwa, baadhi ya viongozi wa TOC wanaomaliza muda wao nao waliondoka, huku rais wa TOC anayemaliza muda wake, Gulam Rashid akishangaa kilichotokea.
"Nilitoka nje wakati matokeo yanatangazwa, mwanzo nilisikia Mtaka ndiye ameshinda, lakini nimerudi nasikia Thadeo ndiye ametangazwa, nini kimetokea," alihoji Gulam.
Thadeo baada ya matokeo kutangazwa alitoka nje ya ukumbi akiwa kama anaongea na simu na kutamka neno moja tu kwamba huo ndiyo uchaguzi na kuondoka eneo la uchuguzi.
Baada ya sintofahamu hiyo, utaratibu wa kuapishwa washindi haukufanyika huku wajumbe wakikaa vikundi vikundi wakipinga matokeo hayo wakidai hawayatambui.
Walidai hawajawahi kuona uchaguzi wa aina hiyo, na kudai kuna namna.
Mwanamichezo wa zamani, Suleiman Nyambui amesema kilichofanyika ni uhuni.
"Thadeo wakati kura zinahesabia alishakubali matokeo na kukiri kura hazijatosha, sababu alipata kura moja tu, imekuwaje ndiye atangazwe mshindi," alihoji Nyambui.
Mpiga kura kutoka Zanzibar, Mohamed Salim alidai hawajakubaliana na matokeo yaliyotangazwa.
"Uchaguzi gani mshindi hajaapa, ametangazwa kisha kamati ikatokomea na yeye hakaondoka, huu uchaguzi sisi kama wapiga kura hatujakubaliana na matokeo.
Uchaguzi huo uliahirishwa mara tatu kufuatia kuenguliwa kwa baadhi ya wagombea akiwamo Mtaka, kabla ya makubaliano ya TOC, Serikali na Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa (IOC) kuwarejesha wiki iliyopita na kuamuliwa uchaguzi ufanyike leo Julai 5, 2026.