Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wakala akanusha tetesi za timu mpya, Salah akiondoka Liverpool

Muktasari:

  • Ameisaidia timu kushinda mataji makubwa ikiwemo Ligi Kuu England mara mbili, Ligi ya Mabingwa Ulaya, Kombe la Dunia la Klabu, Kombe la FA na makombe mengine.

Liverpool, England. Wakala wa nyota wa Liverpool, Mohamed Salah, amevunja ukimya kufuatia tangazo la mchezaji huyo kuondoka klabuni hapo mwishoni mwa msimu huu, akikanusha vikali taarifa zinazodai kuwa tayari ameshachagua timu atakayochezea msimu ujao.

Salah, mwenye umri wa miaka 33, amethibitisha kuwa ataondoka Anfield baada ya kuitumikia Liverpool kwa miaka tisa, licha ya kusaini mkataba mpya wa miaka miwili wenye thamani ya takribani Pauni 400,000 (Sh1.4 bilioni) kwa wiki.

Uamuzi huo unamaanisha kuwa nyota huyo ataondoka kama mchezaji huru, hatua inayovutia vilabu mbalimbali duniani vinavyoweza kuwania saini yake.

Kupitia mitandao ya kijamii, wakala wake Ramy Abbas amesema wazi kuwa hakuna anayejua hatima ya Salah kwa sasa.

Nyota wa Liverpool, Mohamed Salah (kushoto), akiwa pamoja na Wakala wake, Ramy Abbas. Picha na Mtandao

“Hatufahamu Mohamed atacheza wapi msimu ujao, na hiyo pia ina maana hakuna mtu mwingine anayejua,” ameandika, akiwataka watu kupuuza taarifa zisizo na uthibitisho.

Kwa mujibu wa taarifa, vilabu kadhaa tayari vinaonesha nia ya kumsajili mshambuliaji huyo, zikiwemo timu kutoka Mashariki ya Kati na Marekani.

Mwaka 2023, klabu ya Al-Ittihad iliwahi kutoa ofa ya Pauni 150 milioni (Sh516 bilioni) kwa ajili ya kumsajili, huku uwezekano wa kuhamia ligi ya Marekani (MLS) au kubaki barani Ulaya ukiendelea kujadiliwa.

Katika ujumbe wake wa kuaga, Salah ameelezea kwa hisia kubwa jinsi Liverpool ilivyobadilisha maisha yake, akisema klabu hiyo si tu timu bali ni familia.

Nyota wa Liverpool, Mohamed Salah ambaye ametangaza kuondoka Anfield mwishoni mwa msimu huu. Picha na Mtandao

“Kuondoka si jambo rahisi. Hii klabu imenipa kipindi bora zaidi cha maisha yangu,” amesema.

Ametoa shukrani kwa mashabiki kwa sapoti waliompa katika nyakati zote, akiahidi kuwa ataendelea kubeba kumbukumbu hizo maisha yake yote.

Katika kipindi chake Anfield, Salah ameandika historia kubwa akiwa mfungaji wa tatu bora wa muda wote wa klabu hiyo kwa mabao 255 katika mechi 435. Ameisaidia timu kushinda mataji makubwa ikiwemo Ligi Kuu England mara mbili, Ligi ya Mabingwa Ulaya, Kombe la Dunia la Klabu, Kombe la FA na makombe mengine.

Licha ya mafanikio hayo, msimu huu haukukosa changamoto, ambapo kulikuwa na taarifa za kutofautiana na kocha Arne Slot, ikiwemo kukaa benchi mara kadhaa jambo ambalo lilizua mjadala mkubwa kuhusu mustakabali wake klabuni hapo.

Nyota wa Liverpool, Mohamed Salah. Picha na Mtandao

Hata hivyo, inaelezwa kuwa hali ilirejea kuwa nzuri kati yake na benchi la ufundi, na sasa nyota huyo wa Misri anatarajiwa kupewa heshima kubwa na mashabiki wakati atakapocheza mechi zake za mwisho Anfield.

Liverpool imesema kuwa uamuzi wa Salah kutangaza mapema umefanywa kwa heshima kwa mashabiki, huku ikisisitiza kuwa mchezaji huyo bado anaendelea kujitoa kuhakikisha anamaliza msimu kwa mafanikio kabla ya kuaga rasmi.

Kuondoka kwa Salah kunaashiria mwisho wa enzi muhimu katika historia ya Liverpool, huku macho yakielekezwa kuona atachagua wapi kuendelea na safari yake ya soka baada ya msimu huu.