Wanawake warembo kwenye soka Bongo

Muktasari:
- Agosti 22, 2021, Rais Samia Suluhu Hassan alizungumza kuhusu mwonekano wa wachezaji wa kike wa mchezo wa mpira wa miguu kujaribu kuondoka kwenye asili yao na kutaka kujifananisha na wanaume, akiwataka wabaki kwenye haiba yao ya kike, kwa sababu kuna maisha ya baadaye kwa sababu nao watahitaji kuwa na wenza wao kwa ajili ya kuanzisha familia kwa maana ya kufunga nao ndoa
Mtazamo uliojengeka kwa watu ni kuwa binti anapojihusisha na mchezo wa mpira wa miguu, ambao asili yake ni wa kiume, basi asibadili mwonekano wake kuanzia mavazi,nywele,mwendo pamoja na sura kujifananisha na wanaume, bali abaki kwenye haiba yake ya kike.
Agosti 22, 2021 Rais Samia Suluhu Hassan alizungumza kuhusu mwonekano wa wachezaji wa kike wa mchezo wa mpira wa miguu kujaribu kuondoka kwenye asili yao na kutaka kujifananisha na wanaume, akiwataka wabaki kwenye haiba yao ya kike, kwa sababu kuna maisha ya baadaye kwa sababu nao watahitaji kuwa na wenza wao kwa ajili ya kuanzisha familia kwa maana ya kufunga nao ndoa.
Hilo limeanza kuwaingia akilini baadhi ya wachezaji wa kike wa mchezo wa soka hapa nchini, ambao wameamua kubaki kwenye mvuto na mwonekano wa kike bila ya kujali wanajihusisha na mpira wa miguu unaohitaji mwili na ushupavu ndani ya uwanja.
Kocha wa Simba Queens, Mussa Hassan 'Mgosi' anasema mabadiliko ya wachezaji katika timu yake yanayoonekana kwa sasa ni jitihada zilizofanywa kwa makusudi kwa ajili ya kuwataka mabinti kutochagua kuonekana kama wanaume kwa kuwa wanacheza soka na badala yake wabaki kuwa na mwonekano wenye kuvutia kama ilivyo kwenye asilia ya mwanamke.
“Niliweka nidhamu ya kuhitaji wachezaji wabaki katika mwonekano wa kike, nilikataza unyoaji wa kihuni na kuvaa kama wanaume na wale waaliokuwa wanakaidi maagizo niliwarudisha nyumbani na uongozi wa klabu ilikuwa inafahamu hilo.”
Anasema hali hiyo ilimvutia kocha wa timu ya Taifa ya soka ya wanawake Tanzania, Twiga Stars, Bakari Shime kwa kuunga mkono harakati za kuwabadili wachezaji hao, licha ya kwamba kulikuwa na wachache walioonyesha ugumu katika kubadilika ili kuwa na mwonekano wa kike.
Mgosi anasema binti anayehusisha na soka anapaswa kujitambua kwamba yeye bado jinsi yake ni ya kike, hivyo kujaribu kujibadilishe awe kwenye mwonekano wa kiume kitu kinacholeta taswira mbaya kwenye jamii inayowazunguka.
“Haya mambo yaliwafanya hata wachezaji waliokuwa wanakuja kutoka nje wakawa wanaiga maisha ya wenzao wa hapa, lakini nilipokataza wakabadilika na sasa wanaonekana kama wanawake na hata kwenye mitandao yao ya kijamii wanaweka picha zao zenye mvuto na kuwatambulisha kwa mwonekano wa kike,” anasema.
Mwananchi lilifanya mazungumzo na baadhi ya wanasoka wa kike wanaofanya vizuri kwenye mchezo huo, ambao wamekuwa na mwonekano wa kuvutia kama mabinti licha ya kujihusisha na mchezo wa kandanda unahitaji purukushani, ukakamavu na nguvu nyingi ndani ya uwanja.
Aisha Masaka
Binti huyo anayemudu vyema nafasi ya ushambuliaji anacheza soka la kulipwa katika klabu ya BK Hacken ya Sweden, ambapo kwa siku za karibuni ameamua kukacha ule mwonekano wake wa zamani wa kutupia mavazi ya kiume na sasa amekuwa akitinga viwalo vya kike vinavyomfanya kuwa na mvuto mkubwa.
Mrembo Aisha anasema zamani ndoto zake zilikuwa kujishughulisha na masuala ya mitindo, hivyo alipofika Sweden aliona ni vyema akaanza kuishi ndoto zake kuwa kwenye mwonekano wa mitindo ya mavazi ya kike.
“Nilipenda kuwa mwanamitindo, lakini nilipoingia kwenye soka nikakutana na mazingira tofauti ambayo yalinifanya nitembee na mdundo huo niliokutana nao,” anasema.
Mrembo Aisha anasema ilifika wakati hata vazi aina ya gauni hakuwa nalo, lakini kila kitu kilibadilika baada ya kwenda Sweden, ambapo alibadilika na kujiweka kwenye mwonekano wa kike kama ilivyo asili.
"Si rahisi kubadilika, lakini nilijikuta naanza kubadilisha mtazamo kutokana na marafiki niliokuwa nao huku Sweden na ninapenda na nimeamua kusuka kabisa ili kubadilika."
Opah Clement
Mshambuliaji wa kimataifa wa soka la wanawake Tanzania, Opah Clement, anayekipiga kwenye klabu ya Besiktas ya Uturuki, naye ameingia kwenye orodha ya mabinti ambao wameamua kufanya mwonekano wao kuwa wa kike licha ya kukipiga kwenye mchezo wa mpira wa miguu.
Hivi karibuni, mrembo Opah aliposti picha zake kwenye mitandao ya kijamii zinazomwonyesha akiwa kwenye kivazi cha gauni, huku akirembwa uso wake kitu ambacho kiliwavutia mashabiki wake wengi walipovutiwa na kuamua kujiweka kwenye asili na mwonekano wake wa kike.
Opah aliwahi kusema kwenye mahojiano “Wakati mwingine mwonekano unaweza kusababishia changamoto wakati wa kucheza kutoka kwa timu pinzani ili kukutoa mchezoni.”
Irene Kisisa
Staa wa Yanga Princess, Irene Kisisa, moja ya wanasoka wa kike wenye mwonekano wa kuvutia na wanaojiweka kwenye haiba ya kike bila ya kujali kwamba wanajihusisha na mchezo wa mpira wa miguu ambao zama kwa zama ulikuwa ukichezwa na jinsi ya kiume.
Mrembo Irene anafichua kwamba yupo kwenye soka, lakini jambo hilo halijawahi kumfanya afikirie kubadili mwonekano wake ili awe kama mwanamume na badala yake amebaki kama alivyo kwa sababu anajiamini kwenye jinsi yake alivyo.
“Napenda mwonekano wangu wa kike na sijawahi kujibadilisha hata wazazi hawawezi kufikiria tofauti kwa sababu walizoea kuniona na muonekano huu nilionao,” anasema.
Anasema amekuwa akifuatilia wachezaji wa nje na hakuwahi kuwaona wakibadili mwonekano wao kwa sababu ya kucheza mpira hivyo wanazidi kumhamasisha na kuamini kuwa kucheza mpira hakuzuii mitindo.
Hata hivyo anaendelea kusisitiza kuwa kubadilisha mwonekano katika uvaaji hakumaanishi kuwa mtu huyo anajua mpira kuliko wanaovaa kike kwani wapo wanaovaa kike na kufanya vizuri.
Kisisa anapenda kuwaangalia wachezaji wa nje,wasanii na watu maarufu katika uvaaji na vazi lake pendwa ni suruali za kuachia ‘Boyfriend jeans’ kwa kuwa hapendi nguo za kubana.
Protasia Mbunda
Mchezaji wa Fountain Gate Princess, mrembo Protasia Mbunda anasema kinachomfanya aendelee kuhamasika kuvaa mavazi ya kike ni kupenda kwake urembo na aina ya mavazi yanayovuma kwa kipindi husika.
“Kila ninachokifanya katika maisha yangu najali mwonekano wangu kwanza na hii inanifanya nijivunie kuwa mwanamke licha ya kufanyakazi za kiume,” anasema.
Anasema amekuwa akiwaangalia wasanii kama Vanessa Mdee,Frida Amani na Dk Robin B katika masuala mazima ya mwonekano na kwa upande wa wachezaji wa nje amekuwa akimtazama zaidi, staa wa timu ya wanawake ya Aston Villa, Alisha Lehmann, ambaye amekuwa na mwonekano matata kwelikweli na kujiweka kama mwanamke licha ya kucheza soka.
Kutokana na mwonekano wake wa kujiweka kike alibahatika kuwa balozi wa taulo za kike kitu ambacho ameendelea kujivunia nacho katika maisha yake ya soka na kujitofautisha na wachezaji wengine.
Mrembo Protasia ametoa ushauri kwa wazazi kuwaamini mabinti zao na kuwasaidia wanapohitaji msaada kwa kuwa mpira wa miguu ni ajira kama ilivyo nyingine.
“Soka halimfanyi mtoto wa kike kubadili mwonekano hivyo anaweza kucheza na akabaki kuwa mrembo endapo hataiga tabia za wengine,” anasema.
Fatma Issa (Fetty Densa)
Kama umekuwa na kawaida ya kuitazama Simba Queens ikicheza, pale kwenye kiungo yao kumekuwa na binti anayecheza akiwa na uchungi, basi huyo ndiye Fatma Issa maarufu kama Fetty Densa.
Licha ya kujihusisha na mchezo wa soka, mrembo Fatma hakutaka kabisa kuachana na mitindo yake ya mavazi ya kuhakikisha anavaa ushungi hata kama akiwa kwenye jezi na kupambania timu yake ndani ya uwanja. Fetty Densa ni mmoja wa wanasoka wa kike walionyesha kwamba hijabu haiwezi kuwa kikwazo katika kutimiza majukumu yake ndani ya uwanja.
Inawezekana akawa ni mfano wa kuigwa kwa wachezaji wenzie kwani aliamua kufungua biashara zake ambazo zinamuingizia kipato kwa kupitia mavazi ambayo ni ya jinsia zote.
“Juhudi ufanya ndoto ziwe kweli sasa hakuna kukata tamaa kwenye jambo lolote lile pambana mpaka mwisho,” maneno ambayo huyatumia Fetty Densa kwenye mitandao ya kijamii.