Yaliyojili CHAN 2024
Muktasari:
- Kila mechi imetoa wastani wa mabao mawili (2.05), tofauti na msimu uliopita huko Algeria ambako kulikuwa na wastani na wastani 1.9 wakati Senegal ikitwaa ubingwa wa mashindano hayo.
Mashindano ya mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) 2024 yametamatika kwa kishindo juzi, Jumamosi kwenye uwanja wa Michezo wa Kimataifa wa Moi, Nairobi huku yakiacha matumaini makubwa kwa wenyeji, Tanzania, Kenya na Uganda ambao kwa Pamoja pia watandaa fainali za mataifa ya Afrika AFCON 2027.
Mashindano hayo yametamatika kwa Morocco ambayo iliing'oa Tanzania kwenye hatua ya robo fainali kwa bao 1-0, ikitwaa ubingwa wa tatu baada ya kuichapa Madagascar mabao 3-2, hivyo kuwa timu iliyotwaa mataji mengi zaidi ya CHAN, ikiizidi kete, DR Congo.
Katika mashindano hayo ambayo kwa mara ya kwanza yamefanyika ukanda wa Afrika Mashariki yalishuhudiwa yakifungwa jumla ya mabao 90 katika mechi 44 ambazo zilichezwa kwenye viwanja vitano, ikiwemo viwili vya Tanzania, Benjamini Mkapa na Amaan.
Kila mechi imetoa wastani wa mabao mawili (2.05), tofauti na msimu uliopita huko Algeria ambako kulikuwa na wastani na wastani 1.9 wakati Senegal ikitwaa ubingwa wa mashindano hayo.
Rekodi
Mshambuliaji Oussama Lamlaoui, alionekana tena kama mkombozi kwa Morocco, akifunga mabao mawili kwenye mechi hiyo ya fainali, ikiwemo bao la kuvutia kutoka umbali wa mita 40 na kumalizia kama kinara wa mabao wa mashindano akiwa na mabao sita.
Ushindi huo uliifanya Morocco kupata medali za dhahabu pamoja na zawadi ya fedha ya dola 3.5milioni (zaidi ya 8.6bilioni), huku Madagascar ikipata medali za fedha kwa kuwa washindi wa pili na dola 1.2 milioni (zaidi ya sh2.8bilioni).
Mechi hiyo ya fainali, Madagascar ilikuwa ya kwanza kupata bao la kuongoza mapema dakika ya tisa kupitia Felicite Manohantsoa, Morocco ilijibu mapigo kupitia Youssef Mehri kabla ya Lamlaoui kuiweka Morocco mbele kwa bao la pili.
Madagascar hawakukata tamaa. Wakati mchezo ukielekea katikati ya kipindi cha pili, Toky Rakotondraibe alisawazisha, akitumia nafasi ya makosa ya ulinzi. Hata hivyo, Lamlaoui aliibuka tena na kufunga bao la kikatili akiwa karibu na katikati ya uwanja.
Licha ya Madagascar kupoteza mechi hiyo ya fainali, imeweka rekodi kwa kuwa taifa la kwanza kutoka kisiwani kufika fainali ya CAF.
Nyota wa mashindano
Nahodha wa Morocco,Mohamed Rabie Hrimat ndiye mchezaji bora wa mashindano ya CHAN PAMOJA 2024.
Hrimat alikuwa kiongozi wa timu tangu hatua ya makundi hadi fainali, akifunga mabao mawili, kutoa pasi za kufunga mbili.
Mafanikio ya Morocco yalifanikishwa si tu kwa vipaji vya nyota wanaounda kikosi hicho, bali pia kwa uzoefu na utulivu wa wachezaji. Akiwa na miaka 31, Hrimat alionesha sifa hizo, akiongoza wenzake kupitia nyakati ngumu hasa timu inapoelemewa jambao ambalo liliwasaidia na kufanya vizuri katika mechi nyingi ukiondoa moja tu ambayo walipoteza katika hatua ya makundi dhidi ya Kenya kwa bao 1-0.
Sauti ya kinara wa mabao
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mashindano hayo na kutwaa kiatu cha ufungaji bora akiwa na mabao sita, Oussama Lamlioui anasema; "Ninawashukuru sana mashabiki wa Morocco. Tuliwaambia waamini katika timu yetu, na sasa tumethibitisha kuwa tulistahili imani hiyo.”
Bao lake la pili lililofungwa dakika ya 80 liliihakikishia Morocco ubingwa wa tatu baada ya ushindi wa awali wa 2018 na 2020. Lamlioui pia anasisitiza mchango wa wenzake:
“Hii ni kutokana na jitihada za wenzangu. Bila wao, pengine tusingefika hatua hii. Tumeingia katika historia baada ya kushinda mataji matatu ya CHAN. Tunamkabidhi taji hili Mheshimiwa Mfalme Mohammed VI.”
Nyanda la boli
Marc Philippe Arona Diouf wa Senegal, ameteuliwa kuwa kipa bora wa CHAN 2024, akitambuliwa kwa mchango wake muhimu katika kuiongoza timu ya Simba wa milima ya Teranga kupata medali ya shaba.
Katika mechi ya mshindi wa tatu dhidi ya Sudan, Diouf alionyesha kiwango bora. Baada ya Sudan kupata bao la mapema kupitia Mohamed Tia Asad, Seyni Ndiaye alisawazisha kwa Senegal na kufanya mechi hiyo kufika katika mikwaju ya penalti.
Diouf aliokoa penati ya pili ya Sudan, jambo lililobadilisha mwelekeo wa mchezo na kuisaidia Senegal kushinda 4-2.
Diouf alianza kila mechi ya Senegal katika mashindano haya, akithibitisha kuwa muhimili wa timu hiyo ambayo asilimia kubwa iliundwa na vijana chini ya kocha Souleymane Diallo.
Katika mashindani hayo Senegal, ilitunukiwa tuzo ya 'Fair Play' yani timu yenye nidhamu, uadilifu na heshima.
Wenyeji walitisha
Tofauti na namna ambavyo ilikuwa ikifikiriwa pengine kabla ya kuanza kwa mashindano ya CHAN, mataifa wenyeji waliweka rekodi ya kutinga wote hatua ya robo fainali ya mashindano hayo.
Kenya iliyokuwa kundi A, iliwashangaza wengi kwa kuichapa Morocco kwa bao 1-0 na kumaliza hatua hiyo ikiwa kinara ikiwa na pointi 10.
Taifa Stars ikiwa kundi B yenye ilikuwa gumzo zaidi kwa kuweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza katika mashindano hayo kufuzu robo fainali huku ikiwa na mchezo mmoja mkononi, ilikusanya pointi tisa baada ya kuzifunga Burkina Faso (2-0), Madagascar (2-1) na Mauritania (1-0), mechi dhidi ya Afrika ya Kati (0-0) ilikuwa ni kwa ajili ya heshima tu.
Licha ya Uganda kuanza vibaya mashindano hayo kwa kuchapwa mabao 3-0 dhidi ya Algeria ilizinduka katika mechi zilizosalia, jambo ambalo liliwafanya nao kumaliza kinara wa kundi C ikiwa na pointi saba.
Mafanikio
Mashindano ya CHAN 2024 yalishuhudia mafanikio makubwa kwa upande wa kiufundi, maandalizi na ushirikiano wa wadau mbalimbali.
Kuanzia hatua ya makundi hadi fainali, mechi zilizochezwa zilionekana kuwa na kiwango kizuri cha kiufundi huku viwanja vitano vilivyochaguliwa, vikiboreshwa.
Wadau wa mashindano, wakiwemo viongozi wa serikali, walihakikisha kila kitu kilikuwa kipo kwenye mstari sahihi. Utaratibu wa kiusalama na usimamizi wa mashindano ulisimamiwa kwa makini na kuipa taswira nzuri timu za kigeni na mashabiki wa kimataifa waliotembelea.
Pamoja na mafanikio haya, mashindano pia yalitumia teknolojia na mbinu za kisasa katika usimamizi wa mechi, ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji wa takwimu za wachezaji, mfumo wa VAR na kamera za kuripoti matukio muhimu. Hii imesaidia kuongeza uwazi na uadilifu katika mashindano.
Kwa ujumla, mafanikio ya CHAN 2024 yameacha taswira chanya kwa mataifa ya Afrika Mashariki, wakionyesha uwezo wa kibiashara, kiufundi, na kuandaa mashindano ya kimataifa. Hii ni hatua kubwa kuelekea michuano ya AFCON 2027, ambapo Tanzania, Kenya na Uganda zitakuwa wenyeji.
Hapa haikuwa sawa
Hata hivyo, mashindano haya yalikuwa na changamoto kadhaa. Tanzania na Kenya zilikumbana na rungu la CAF kutokana na ukiukwaji wa kanuni za usalama, jambo lililoathiri baadhi ya mechi na usimamizi wa mashindano. Changamoto hizi ziliibua umuhimu wa kufanya maboresho ya kiusalama mapema kabla ya mashindano makubwa.
Baadhi ya masuala muhimu yalihusisha upatikanaji wa vifaa muhimu, usimamizi wa mashabiki na mafunzo ya maafisa wa usalama.
Changamoto nyingine ni ushirikiano kati ya wadau wa mashindano, ikiwemo mashirikisho ya soka na serikali. Mara kwa mara, baadhi ya taratibu za CAF zilihitaji ufafanuzi wa haraka, jambo lililokuwa changamoto kwa mashirika ya ndani katika kuhakikisha kila kitu kinapita kwa utaratibu sahihi.
Pamoja na changamoto hizi, mashindano haya yameonyesha kuwa ni lazima kuimarisha miundombinu, mafunzo na utaratibu wa usalama kwa ajili ya mashindano yajayo. Tanzania na Kenya zinapaswa kuchukua hatua zinazohitajika ili kuhakikisha usalama, utaratibu na ulinganifu katika mashindano makubwa.
Kwa upande mwingine, changamoto hizi ni fursa pia kwa nchi za Afrika Mashariki kujifunza na kuboresha maandalizi. Ni muhimu kutumia uzoefu huu kuongeza ubora wa mashindano yajayo.
Baada ya CHAN
Ili kuhakikisha mafanikio ya mashindano ya AFCON 2027 yanakuwa yenye mafanikio zaidi, Tanzania, Kenya na Uganda zinapaswa kuanza maandalizi mapema. Hii inajumuisha kuboresha viwanja, kuhakikisha miundombinu ya kisasa na kuhakikisha kila kitu kipo kwenye mstari sahihi ikiwemo kuandaa vikosi bora zaidi.
Ni muhimu pia kuweka mkakati wa masoko na mawasiliano ili kuvutia mashabiki wa kimataifa na wadau wa soka. Hii itasaidia kuongeza umaarufu wa mashindano na kuongeza mapato kwa nchi wenyeji.
WENYEJI CHAN
2009- Ivory Coast
2011- Sudan
2014- Afrika Kusini
2016- Rwanda
2018- Morocco
2020- Cameroon
2022- Algeria
2024- TZ, KE, UG
Mabingwa CHAN
2009- DR Congo
2011- Tunisia
2014- Libya
2016- DR Congo
2018- Morocco
2020- Morocco
2022- Senegal
2024- Morocco
90- Idadi ya mabao yote yaliyofungwa katika fainali za CHAN 2024 kupitia mechi 44
13- Jumla ya penalti zilizopigwa katika CHAN 2024 ikiwamo moja iliyokoswa
07- Kadi nyekundu zilizoonyeshwa katika fainali hizo za nane za CHAN 2024
03- Wachezaji pekee waliojifunga katika fainali hizo za CHAN zilizoshirikisha nchi 19