Yanga, Azam TV waelewana

What you need to know:

Habari za kuaminika kutoka kwa mmoja wa viongozi wa klabu hiyo, pande hizo mbili zinatarajiwa kusaini mkataba huo ndani ya wiki mbili.

Dar es Salaam. Mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga wamemaliza tofauti zake na kituo cha runinga cha Azam na sasa iko tayari kupokea fedha za udhamini kwa haki za matangazo kutoka kwa wadhamini hao.

Habari za kuaminika kutoka kwa mmoja wa viongozi wa klabu hiyo, pande hizo mbili zinatarajiwa kusaini mkataba huo ndani ya wiki mbili.

“Kwa sasa tupo katika mazungumzo na AzamTV kuhusu masuala ya haki za televisheni pamoja na kuonyesha kwa vipindi vya Yanga TV katika Azam HD,” alisema kiongozi huyo.

Kwa kusaini mkataba huo, Yanga inatarajia kujipatia zaidi ya Sh600m, ikiwa ni fedha za udhamini wa matangazo ya Ligi Kuu pamoja na kipindi cha Yanga TV kitakachorushwa kupitia kituo hicho cha runinga.

Yanga pekee kati ya timu 16 za Ligi Kuu ndiyo ilikuwa haijachukua fedha za mgawo wa udhamini wa Azam TV kwa miaka miwili unaokadiriwa kufikia Sh300m.

Mkataba uliopo baina ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Azam TV, unaonyesha kuwa kila klabu inatakiwa kupata Sh100 m kwa mwaka na Yanga kwa miaka miwili imekuwa ikigomea kiasi hicho cha fedha kwa madai ni kidogo kulinganisha na ukubwa wa klabu hiyo.

This page might use cookies if your analytics vendor requires them.