Yanga ikafanye haya Nigeria

Muktasari:

  • MASHABIKI wa Yanga wamepewa somo na watalamu wa soka kwamba, mchezaji anatakiwa ajipambanue asilimia 75 uwanjani na 25 zinakuwa za maarifa aliyoongezewa na kocha.

MASHABIKI wa Yanga wamepewa somo na watalamu wa soka kwamba, mchezaji anatakiwa ajipambanue asilimia 75 uwanjani na 25 zinakuwa za maarifa aliyoongezewa na kocha.

Wametoa kauli hiyo, wakati wanauchambua mchezo wao dhidi ya Rivers United, kwamba siyo kila kitu cha kumtupia mawe kocha, kiufundi kuna vitu vingi vinahitaji muda ili Yanga ifikie kiwango wanachokitaka.

Mchezaji wa zamani wa Mecco ya Mbeya, Abeid Kasabalala amesema asilimia 25 za kocha ndani yake kuna ufundi, mbinu na plani, wakati za mchezaji anatakiwa awe fiti, maamuzi, ushapu, kubadili mchezo kulingana na wanachokutana nacho uwanjani na mambo mbalimbali yanayohusiana na kipaji chake.

"Yanga  walipoteza kwa sababu hawana koneksheni, ila wamesajili timu nzuri inayohitaji utulivu mkubwa wakati wa matengenezo na siyo kelele ambazo zitamtoa kocha mchezoni," amesema Kasabalala na ameongeza kuwa;

"Hata akija kocha mwingine bila kumpa utulivu haiwezi kuwasaidia kitu, kwani hata Simba ilichukua muda mrefu kukijenga kikosi chao,"amesema.

Naye mchambuzi wa soka, Ally Mayay amesema kinachotakiwa ni Yanga kujua ni namna gani ya kushinda mechi ya ugenini sio kutafuta mchawi, wakati inajulikana maandalizi ya timu hayakuwa mazuri.

"Siyo wakati wa nani kafanya nini, wanatakiwa kujua nini kifanyike kwa ajili ya mchezo wa marudiano, hilo ndilo litakaloleta furaha ya kweli kwa mashabiki," amesema.