Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga na karata ya tahadhari Algeria

Dar es Salaam. Itakapotimu saa 4:00 usiku kwa saa za hapa Tanzania (wakati kule Algers ikiwa ni saa 2:00 usiku) wapenda soka wengi watavutika kujua kitakachojiri kule mjini Algiers wakati mabingwa wa soka nchini, Yanga, watakaposhuka kwenye Uwanja wa Stade 5 Juillet 1962 kuvaana na wenyeji wao CR Belouizdad katika mchezo wa kwanza wa kundi D la Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga itaanza mechi hiyo ikiwa na kumbukumbu kwamba mara ya mwisho kucheza hatua kama hii ilikuwa miaka 25 iliyopita na sasa inarudi ikiwa na kikosi imara zaidi ambacho msimu uliopita kilishtua kwa kucheza fainali ya ya Kombe la Shirikisho la Caf.

Ilibaki hatua moja tu Yanga kuchukua taji hilo lililochukuliwa na USM Alger ya hapo hapo Algeria na sasa mabingwa hao wa Tanzania leo watashuka uwanja ule ule wa ile fainali kujiuliza kwa Belouizdad.

Mara ya mwisho Yanga kucheza kwenye uwanja huo ilikuwa Juni 3, 2023 ambapo iliwashtua mashabiki wa USM Alger ikishinda bao 1-0 huku ikicheza soka la nguvu lililowalazimu Waarabu hao kuwafanyia vurugu nyingi wakihofia kuaibika nyumbani lakini kwa ugumu wakalichukua taji hilo.

Yanga itarudi kupambana na Belouizdad ambao hawana rekodi za kutisha kwenye michuano ya CAF kulinganisha na USM Alger.

Yanga haikuwahi kukutana na Belouizdad hapo kabla ambapo timu zote mbili zitakwenda kuandika historia ya kwanza kwenye mechi hiyo kabla ya kurudiana baadaye.

Mabingwa hao wa Tanzania tayari wapo nchini Algeria kwa siku tatu kabla ya mchezo huo wakitua kwa mafungu matatu kutokana na wachezaji wengine kuwa kwenye timu za taifa.

Hali ya hewa ya jijini Algers ni ya baridi kiasi inayoambatana na mvua za vipindi tofauti ambapo, tayari kikosi hicho kimeonyesha kuanza kuzoea mazingira hayo tayari kwa mchezo.

Belouizdad hawako vizuri sana kwenye ligi ya ndani ambapo kwenye mechi zao tano zilizopita imeshinda tatu ikipoteza mbili, lakini ina matokeo mazuri kwenye mechi zao mbili za Ligi ya Mabingwa ilipoitupa nje BO Rangers ya Sierra Leone kwa jumla ya mabao 6-1.

Yanga inatakiwa kumchunga mshambuliaji Leone Wamba, raia wa Cameroon aliyefunga hat-trick wakati inatinga makundi.

Mbali na Wamba ambaye anaongoza kwa ufungaji ligi ya kwao sambamba na Boussouf Ishak wenye mabao mawili kwenye ligi, Yanga inatakiwa kuwa makini na Darfalou Oussama, kiungo Benguit Abdelraouf wenye bao moja kila mmoja.

Yanga itakutana pia na mshambuliaji Meziane Bentahar ambaye atakutana na Yanga kwa mara ya tatu baada ya kuhamia hapo akitokea USM Alger ambayo Wananchi walikabili kwenye mechi mbili za fainali ya Kombe la Shirikisho msimu uliopita.

Yanga iko vizuri kwani kwenye mechi zake tano zilizopita haijaangusha alama yoyote kwenye ligi ikiringia safu yao ya kiungo iliyopewa jina la MAP (ikimaanisha Maxi Nzengeli, Aziz KI Stephanie na Pacome Zouzoua) ambao wako kwenye moto mkali msimu huu tangu uanze.

Yanga itahitaji ushindi au sare kwenye mechi hiyo ikitambua kwamba inapaswa kujenga kujiamini kabla ya kurudi nyumbani kucheza dhidi ya Al Ahly ya Misri ambao ndio mabingwa watetezi wa taji hilo.

Kocha mkuu wa Yanga, Miguel Gamond amesema anawaheshimu wapinzani wake na lengo lake kubwa ni kuhakikisha wanapata matokeo mazuri leo.