Yanga wakutana Dar kupeana mikakati ya msimu mpya
Muktasari:
- Msimu wa 2024/2025, Yanga ilitwaa mataji matatu ambayo ni Ligi Kuu, Kombe la FA na Ngao ya Jamii.
Dar es Salaam. Uongozi wa Yanga leo unakutana na benchi la ufundi, wachezaji na watendaji wa klabu katika semina maalum inayofanyika kwenye Hoteli ya Rotana, Dar es Salaam.
Semina hiyo ni kwa ajili ya utambulisho, historia, matarajio na majukumu ya kila mmoja ndani ya klabu hiyo.
Kuandaliwa kwa semina hiyo hapana shaka ndio mwanzo rasmi kwa Yanga kujiandaa na msimu mpya wa 2025/2026 ambao itakuwa na kibarua cha kutetea mataji matatu makubwa iliyotwaa msimu uliomalizika.
Mataji hayo ni Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la FA na Ngao ya Jamii.
Yanga itaanza kwa kutetea taji la Ngao ya Jamii kwa kukabiliana na Azam FC katika nusu fainali ya mashindano hayo ambayo yamepangwa kuchezwa kuanzia Septemba 11 hadi 14 mwaka huu.
Siku mbili baada ya mashindano ya Ngao ya Jamii kumalizika, Yanga itaanza kibarua cha kutetea ubingwa wa Ligi Kuu ambayo msimu ujao imepangwa kuanza Septemba 16.
Kwa upande wa Kombe la Shirikisho la CRDB, mashindano hayo yamepangwa kuanza kati ya Novemba 21 na Novemba 23, 2025.
Miongoni mwa wachezaji waliohudhuria semina hiyo ni nyota wa kigeni walionaswa na Yanga katika dirisha linaloendelea la usajili ambao ni Lassine Kouma, Balla Conte, Andy Boyeli na Celestin Ecua.
Wachezaji hao wamesajiliwa na Yanga kuziba nafasi za Khalid Aucho, Clatous Chama, Kennedy Musonda na Stephane Aziz Ki ambao wameachana na timu hiyo.