Yanga yaanza mbinu za Bayern, Mtunisia afunguka...

Muktasari:

MASHABIKI wa Yanga wanafurahia ubora wa timu yao ikiwa imeshinda mechi tano na kutoa sare moja na wako pale juu ya msimamo. Imefichuka kwamba kuna mambo matamu yanatoka klabu za Bayern Munich ya Ujerumani na Atletico Madrid ya Hispania.

MASHABIKI wa Yanga wanafurahia ubora wa timu yao ikiwa imeshinda mechi tano na kutoa sare moja na wako pale juu ya msimamo. Imefichuka kwamba kuna mambo matamu yanatoka klabu za Bayern Munich ya Ujerumani na Atletico Madrid ya Hispania. Kuna Kocha mmoja mzungu ambaye huwa na mzuka sana Yanga akishinda. Huwa anaonekana kwenye kibendera akishangilia na wachezaji.

Huyo ni Kocha wa mazoezi ya viungo wa Yanga, anaitwa Helmy Gueldich. Ni Raia wa Tunisia. Ameliambia Mwanaspoti kwamba amelazimika kutumia programu za mazoezi ya klabu za Bayern ambao ni Mabingwa wa Ujerumani na ile ya Atletico kutokana na aina ya falsafa ya kocha wa Yanga Nesreddine Nabi.

Helmy alisema Bayern ina kocha bora wa viungo, Holger Broich wakati Atletico wakiwa na Oscar Ortega amekuwa akiwasiliana nao kupata mbinu mpya za kuimarisha wachezaji wa Yanga.

Helmy ambaye ana shahada ya uzamivu katika mazoezi ya viungo, alisema; “Hawa ni madaktari kabisa kama mimi katika taaluma ya mazoezi ya viungo nilikuwa nafahamiana nao kabla sijaja Yanga kwasasa duniani hawa pia ndio wako ghali kutokana na mafunzo yao.”

“Huwa nawasiliana nao sana walifurahi kusikia nipo Tanzania wakataka kujua maendeleo yangu na huwa nawatumia kila programu kubwa zinazofanywa kwa wachezaji na wamekuwa wakinipongeza na kuniongezea vitu zaidi.”

Helmy aliongeza kuwa falsafa ya Nabi ambaye soka lake linahitaji wachezaji wanaojua kukaba kwa nguvu amekuwa akinufaika na ushauri wa watalaam hao ambapo sasa ubora mkubwa umekuwa ukiongezeka kwa wachezaji wake.

“Hapa Yanga kocha Nabi anataka timu yake inapopoteza mpira ndani ya sekunde tano tayari mpira uwe umepokonywa kwa timu pinzani,hili linahitaji wachezaji walio tayari hasa katika kukaba kwa nguvu.

“Hizi ni mbinu ambazo zinatumika na Atletico,Bayern,Liverpool na hata Manchester City,ushauri wa Ortega na Broich umekuwa ukisaidia kuongeza ubora huu kwa wachezaji wa Yanga ambao tunazidi kuuona sasa.

“Kwasasa nikiwaangalia wachezaji wangu naona ni kama asilimia 65 tu wako katika kiwango ninachotaka bado kuna kazi ambayo tunaendelea kuhakikisha kiwango kinaongezeka zaidi kama hatutakuwa na kusimama kwa ligi,”aliongeza Kocha huyo ambaye Nabi aliwahi kumsifia hadharani hivikaribuni akisisitiza kuwa ndiye anayehusika na ubora wa Yanga ya sasa haswa kwenye utimamu wa miili ya wachezaji. Yanga imeshinda mechi mbili ugenini na kutoa sare moja kwenye michezo yake mitatu iliyocheza huko mpaka ligi inakwenda kusimama kupisha ratiba za kimataifa