Yanga yabanwa mbavu Kwa Mkapa, Pacome aokoa jahazi
Dar es Salaam. Yanga imeondoka na pointi moja baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Al Ahly kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam mchezo wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Huu ni mchezo wa pili wa hatua ya makundi kwa Yanga iliyo Kundi D baada ya ule wa kwanza kupoteza jijini Algers, Algeria kwa mabao 3-0 kutoka kwa CR Belzoudad.
Kwa matokeo hayo, Yanga inasalia nafasi ya nne kwenye msimamo na alama moja na ina kibarua kigumu kwenye kuwania kufuzu hatua ya robo fainali.
Yanga yenye historia ya kufuzu hatua ya makundi ya ligi hiyo mara ya mwisho mwaka 1998, ilipata bao la kusawazisha dakika ya 91 lilifungwa na Kiungo Pacome Zouzoua baada ya lile la Al Ahly la dakika ya 87 lilifungwa na Percy Tau.
Yanga haijapata ushindi mpaka sasa katika mechi mbili walizocheza na ina kibarua kizito kwani mechi inayofuata watakutana na Medeama ambayo iliwafunga bao 2-1 CR Belzoudad.
Kwa matokeo hayo, Al Ahly inaendelea kusalia kileleni ikiwa na alama nne, ikifuatiwa na Medeama yenye tatu sawa na Belzoudad na Yanga ya mwisho na pointi moja.