Yanga yapata faili la Rivers United

Muktasari:

  • YANGA tayari wapo Port Harcourt, Nigeria kwa mchezo wao marudiano wa raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku ikiwa imenasa faili la wapinzani wao, River United juu ya walivyo kwenye mechi zao za uwanjani wa nyumbani na Kocha Nasreddine Nabi akitamba watapindua meza.

YANGA tayari wapo Port Harcourt, Nigeria kwa mchezo wao marudiano wa raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku ikiwa imenasa faili la wapinzani wao, River United juu ya walivyo kwenye mechi zao za uwanjani wa nyumbani na Kocha Nasreddine Nabi akitamba watapindua meza.

Yanga itarudiana na Rivers Jumapili hii kwenye Uwanja wa Yakubu Gowon, jijini Port Harcourt, huku nikiwa na deni la kipigo cha bao 1-0 walilofungwa katika mechi ya mkondo wa kwanza iliyopiga wikiendi iliyopita kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kwa sasa kilichobaki ni safu ya ulinzi ya Yanga inapaswa kuchanga vyema karata zake katika kipindi cha kwanza cha mechi ya marudiano ugenini dhidi ya Rivers kesho Jumapili ili iweze kutimiza lengo lake la kupindua meza baada ya kupoteza mechi ya kwanza nyumbani kwa bao 1-0

Kwa mujibu wa takwimu zilizopo za timu hiyo kwa mechi 10 za mwisho ambazo Rivers imecheza Uwanja wake wa nyumbani wa Yakubu Gowon uliopo mjini Port Harcourt zinaonyesha safu ya ushambuliaji ya timu hiyo imekuwa tishio zaidi kipindi cha kwanza kulinganisha na inavyokuwa katika dakika 45 za pili.

Katika mechi 10 zilizopita za mashindano tofauti ambazo Rivers wamecheza katika uwanja huo imefunga jumla ya mabao 17 ambapo kati ya hayo, 10 imepachika kipindi cha kwanza na mengine saba imefunga kipindi cha pili.

Na kudhihirisha kwamba Rivers imekuwa na hulka ya kushambulia kwa nguvu mwanzoni, hata mabao saba iliyofunga katika kipindi cha pili, manne imepachika katika dakika 15 za mwanzoni huku matatu tu ikipachika katika muda unaobakia.

Rivers kushambulia kwa nguvu kubwa mwanzoni na imekuwa ikiwagharimu hasa kipindi chja pili kwani ndio muda huwa inaruhusu sana mabao kwani kati ya matano iliyofungwa katika mechi zake 10 zilizopita uwanjani hapo, matatu imeruhusu katika kipindi hicho na mawili cha kwanza.

Dakika 15 za kwanza na zile za pili, ndizo Rivers imekuwa hatari zaidi katika kufumania nyavu imefunga jumla ya mabao nane.

Kuanzia dakika ya 1-15 imefunga manne na katika dakika ya 46-60 wamefumania nyavu mara nne

Hata hivyo pamoja na kiu ya Yanga kupindua meza ugenini, inapaswa kuingia na tahadhari kubwa katika Uwanja wa Yakubu Gowon kwani Rivers imekuwa ngumu kufungika.

Katika mechi 10 zilizopita ilizocheza hapo, Rivers haijapoteza mechi kwanin imeshinda saba na kutoka sare tatu na mechi mmoja tu iliyocheza bila kufunga bao.

Katika mechi hiyo ya ugenini refa wa kati atakuwa ni Adaari Abdul Latif kutoka Ghana akisaidiwa na Waghana wenzake Paul Atimaka, Patrick Papala na Kwame Sefah atakayekuwa mezani.

Licha ya Rivers kuwa na takwimu nzuri ikiwa nyumbani, kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi alisema wanao uwezo wa kuwatoa.

“Kuna makosa machache yaliyojitokeza katika mechi iliyopita tukiyarekebisha tuna nafasi kubwa ya kushinda ugenini na kusonga mbele kwani Rivers sio timu tishio kiasi hicho.” alisema.

“Muhimu mashabiki wasikate tamaa. Kama wao walipata matokeo mazuri hapa nasi tunaweza kushinda kwao. Wachezaji wako tayari kwa marudiano.”

Mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya Yanga, Rodgers Gumbo alisema wana imani kubwa ya kupata ushindi ugenini.

Yanga inahitaji ushindi wa zaidi ya mabao 2-0 isonge mbele.