Yanga yapata hasara ya 1 bilioni

Klabu ya Yanga SC imeweka wazi ripoti yake ya mapato na matumizi kwa msimu wa 2023/2024, ikionyesha uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa fedha za klabu. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, klabu imefanikiwa kupata mapato ya jumla ya shilingi bilioni 21.1.

Usajili na uhamisho wa wachezaji kama kina Pacome Zouzoua, Yao Kouassi, Joseph Guede ni moja ya maeneo yaliyotumia fedha nyingi, ambapo bilioni 3.5 zilitumika kuhakikisha klabu inapata wachezaji bora.

Gharama za mishahara kwa wachezaji na benchi la ufundi zilitumia sehemu kubwa zaidi ya bajeti, ikifikia Sh 7.39 bilioni. Hii inaonyesha nia ya klabu kuboresha viwango vya wachezaji na kuhakikisha wanapata maslahi bora.

Matumizi mengine muhimu ni pamoja na usafiri, chakula na malazi, ambapo klabu ilitumia Sh 2.89 bilioni kuhakikisha wachezaji na benchi la ufundi wanapata huduma bora wakati wa safari na kambi za mazoezi.

Maandalizi ya mechi nayo yaligharimu Sh 1.85 bilioni, fedha hizi zikiwa zimeelekezwa katika kuhakikisha vifaa na maandalizi yote muhimu kwa ajili ya mechi yanakamilika kwa wakati.

Motisha kwa wachezaji na benchi la ufundi imechukua Sh 2.6 bilioni, fedha hizi zikiwa ni kwa ajili ya bonasi na zawadi kwa wachezaji na makocha kutokana na mafanikio mbalimbali. Gharama za kambi zimesimama kwenye Sh 702 milioni, huku compliance ikigharimu Sh 944 milioni. Gharama za kiutawala zimefikia Sh 1.46 bilioni, ikijumuisha matumizi ya ofisi na mishahara ya wafanyakazi wa utawala.

Aidha, Yanga imetumia Sh 424 milioni kwa ajili ya masoko na Sh 503 milioni kwa gharama za kifedha, ambazo ni pamoja na riba za mikopo na huduma za kibenki. Jumla ya matumizi yote kwa msimu huu yamefikia shilingi bilioni 22.29 ikiwa ni ziada ya bilioni moja.

Ripoti hii inaonyesha jinsi klabu imekuwa ikijitahidi kuboresha miundombinu na ustawi wa wachezaji wake kupitia matumizi bora ya fedha. Kwa uwazi huu, Yanga SC inatarajia kuendelea kupata uungwaji mkono kutoka kwa wanachama na wadau mbalimbali ili kuleta mafanikio zaidi katika msimu ujao.