Yanga yawahi Zanzibar kuiandalia kipigo AS FAR
Muktasari:
- Yanga imepangwa katika kundi B la Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa pamoja na timu za Al Ahly, AS FAR na JS Kabylie.
Dar es Salaam. Yanga imepanga kusafiri kesho Jumanne, Novemba 18, 2025 kwenda Visiwani Zanzibar kuanza maandalizi ya mchezo wake wa kwanza wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS FAR mwishoni mwa wiki hii.
Mechi hiyo imepangwa kuchezwa katika Uwanja wa New Amaan Complex, Jumamosi, Novemba 22, 2025 kuanzia saa 10:00 jioni. Taarifa ya safari hiyo ya Yanga imetolewa leo na Ofisa Habari na Mawasiliano wa timu hiyo, Ally Kamwe.
"Yanga SC itaelekea Zanzibar hapo kesho kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya FAR Rabat. Timu itaondoka saa tatu asubuhi kwa njia ya boti.
“Baadhi ya wachezaji kama Prince Dube, Celestine Ecua, Lassine Kouma waliokuwa bado kwenye majukumu ya timu zao za taifa hawatakuwepo kwenye safari hii ya kesho lakini tayari uongozi umeshaweka taratibu zote vizuri ili wachezaji hawa wasafiri na kuungana na timu Zanzibar moja kwa moja.
"Wachezaji waliokuwa kwenye timu ya Tanzania wamesharejea na ni sehemu ya safari ya kesho. Niwaombe Wazanzibar kujitokeza kwa wingi kuipokea timu kesho na kuwaonyesha wachezaji wetu ni kwa kiasi gani mko tayari kwa ajili ya mchezo huu mkubwa wa Kihistoria. Zinakwenda kukutana timu mbili bora Afrika kwa sasa,” amesema Kamwe.
Awali Yanga ilikuwa inautumia Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam ambao sasa utatumiwa na Simba pekee kwenye hatua
hiyo ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kamwe aliwahi kunukuliwa akisema kuwa uamuzi huo umekuja baada ya tathmini ambayo uongozi wa klabu hiyo umeifanya baada ya kupangwa kwa makundi ya mashindano hayo.
"Sio kundi jepesi na sio kundi lelemama na sisi uongozi wa Young Africans tunakiri kwamba hili ni kundi gumu na ni kundi ambalo halitabiri hadi sasa hivi na yoyote anaweza kuwa na nafasi ya kuelekea kwenye hatua ya robo fainali.
"Na sisi kama klabu tunaanza mipango yetu sasa hivi kuhakikisha tunakuwa timu moja katika mbili ambazo zitafuzu kuelekea hatua ya robo fainali.
“Tayari ratiba imeshatangazwa kwa maana mechi zitakavyokuwa. Young Africans tutaanzia mchezo wa kwanza nyumbani dhidi ya FAR
Rabat, baada ya hapo tutasafiri kwenda Algeria kucheza na JS Kabylie," alinukuliwa Kamwe.