Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Gavana BoT: Benki ya CRDB endeleeni kuwezesha maendeleo ya jamii na uchumi

Ni ngumu kutenganisha safari ya ukuaji wa Benki ya CRDB ndani ya miaka 30 iliyopita na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambaye ndiye msimamizi wataasisi zote za fedha nchini. BoT amekuwa mzazi mwema aliyetimiza majukumu yake ya malezi na
sasa anasherehekea ukuaji wa mtoto wake ndani ya kipindi hicho chote.

Gazeti hili limefanya mahojiano maalumu na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba kuhusiana na safari ya miaka 30 ya ukuaji wa Benki ya CRDB na mchango wa BoT katika safari hiyo. Fuatana nasi katika mahojiano haya:

Swali: Kwa kifupi, unaielezeaje miaka 30 ya Benki ya CRDB?
Gavana: Miaka 30 ya Benki ya CRDB imekuwa ni safari ya mafanikio makubwa katika kuendeleza na kuimarisha sekta ya benki nchini. Katika kipindi hiki, Benki ya CRDB imejidhihirisha kama benki bunifu na jumuishi kwa kutoa huduma mbalimbali za kifedha zinazowagusa wananchi wengi zaidi.

Huduma hizo ni pamoja na huduma za kibenki kwa njia ya kidijitali, kupitia mawakala wa benki, uwakala wa bima, huduma za mikopo, na huduma katika soko la mitaji. Hadi kufikia Aprili 2025, Benki ya CRDB ilikuwa na zaidi ya matawi 260 nchini, sambamba na uwepo wake katika nchi jirani kupitia kampuni tanzu nchini Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Mafanikio haya yanadhihirisha dhamira ya benki hii kutoa huduma jumuishi na kuwa chombo muhimu cha maendeleo ya kiuchumi nchini. Kwa mtazamo wako, upi umekuwa mchango wa Benki ya CRDB katika kukuza sekta ya benki nchini? Benki ya CRDB imekuwa chachu ya maendeleo ya sekta ya benki kwa
kuanzisha huduma bunifu na kuhakikisha zinawafikia Watanzania wengi.

Benki ya CRDB imeleta mchango mkubwa katika upatanisho na ujumuishi wa kifedha kwa kuwafikia wananchi wengi. Hadi Mei 2025 Benki ya CRDB ilikuwa na jumla ya akaunti za wateja milioni 6.22 na amana za wateja kiasi cha Sh11.33 trilioni.

Aidha, benki hiyo imetoa mikopo yenye jumla ya thamani ya Sh11.64 trilioni katika sekta mbalimbali muhimu za uchumi, ikijumuisha Sh2.7 trilioni katika sekta ya kilimo, Sh1.63 trilioni katika sekta ya biashara, Sh817.99 bilioni katika sekta ya viwanda na uzalishaji, Sh517.05 bilioni katika sekta ya
ujenzi, Sh168.68 bilioni katika sekta ya usafirishaji na mawasiliano na jumla ya Sh5.78 trillioni katika sekta nyinginezo kwa ujumla wake.

Benki ya CRDB imeendelea kujikita katika kutoa huduma mbalimbali ikiwemo kwa njia ya kidijitali, huduma za uwakala wa bima, huduma za mikopo kwa taasisi na watu binafsi na huduma za soko la mitaji. Benki ya CRDB ilikuwa benki ya kwanza kuanzisha huduma ya wakala wa benki (agency banking).

Hadi Mei 2025 benki hiyo ina mawakala 38,763, hatua inayochochea ujumuishaji wa kifedha hasa katika maeneo yasiyofikiwa na matawi ya benki.

Pia, Benki ya CRDB ilitangulia kutoa huduma kama ‘mobile banking’, ATM, ‘diaspora account’, na matawi yanayotembea. Huduma hizi zimeongeza sana urahisi wa upatikanaji wa huduma za fedha nchini. Aidha, Benki ya CRDB imekuwa benki ya kwanza ya ndani kuvuka mipaka ya Tanzania kwa kuwekeza katika nchi jirani, hatua ambayo si tu imepanua wigo wake
wa kibiashara bali imechangia kukuza utandawazi wa huduma za fedha kutoka Tanzania.

Kwa kushirikiana na Serikali, Benki ya CRDB imesaidia kuzinusuru benki zenye changamoto kama vile Benki ya Wananchi Tandahimba (TCB) na Benki ya Ushirika Kilimanjaro (KCBL), zoezi lililofanikisha kuanzishwa kwa Benki ya Taifa ya Ushirika yaani Cooperative Bank of Tanzania (CBT), Benki ya CRDB ikiwa mwanahisa, hatua inayodhihirisha dhamira ya benki
hiyo kuimarisha ustawi wa sekta ya fedha nchini.

Vilevile, kupitia kampuni yake tanzu yake ya CRDB Bank Foundation, Benki ya CRDB imeendelea kuwawezesha wanawake wajasiriamali pamoja na vijana kupitia Programu ya Imbeju ambapo hadi Machi 2025 imetoa elimu ya ujasiriamali na mafunzo ya elimu ya fedha kwa watu takribani milioni 1.25 na mitaji wezeshi kwa wajasiriamali wadogo 520,149 huku jumla ya fedha zilizotolewa kama mitaji zikifikia Sh10.25 bilioni.

Mchango wa Benki Kuu ya Tanzania kwenye safari ya miaka 30 ya Benki ya CRDB ni upi? Benki Kuu ya Tanzania, kama msimamizi wa sekta ya fedha nchini, imetoa mchango mkubwa katika mafanikio ya Benki ya CRDB, kama ilivyo kwa benki nyingine zote hapa nchini kwa kuweka mazingira rafiki ya kibiashara, kutoa miongozo na kanuni muhimu, na kuruhusu ubunifu katika utoaji wa huduma mpya.

Kwa mfano, Benki Kuu iliidhinisha huduma ya wakala wa benki
iliyoanzishwa na Benki ya CRDB, ambayo imeleta mageuzi makubwa katika upatikanaji wa huduma za fedha nchini.

Aidha, Benki Kuu imeendelea kuwa msikivu na mshirika wa karibu kwa taasisi zote za fedha, ikiwemo Benki ya CRDB, kwa kuzipa vibali vya kuanzisha bidhaa mpya na kuziwezesha kufanikisha jitihada za ujumuishaji wa kifedha kwa wananchi.

Mchango huu wa Benki Kuu umeimarisha uthabiti wa sekta na kuchochea ushindani na ubunifu miongoni mwa benki. Aidha, Benki Kuu imeendelea kuziwezesha benki za biashara nchini, ikiwemo Benki ya CRDB, kwa kuzipa ukwasi pale inapohitajika ili kuwezesha shughuli mbalimbali za uendeshaji wa benki husika kufanyika kama kawaida. Unaiona wapi benki hii katika miaka 30 ijayo na una ujumbe gani kwa uongozi wa benki hiyo?
Katika kipindi cha miaka 30 iliyopita benki ilikuza mali zake kutoka kiasi cha Sh 54 bilioni mwaka 1996 hadi Sh 17.14 trilioni Mei 2025.

Naiona benki ambayo itaendelea kujikita kuwa benki ya kimkakati na kuwa kiongozi wa huduma za kibenki katika ukanda wa Afrika, kusini mwa Jangwa la Sahara. Benki itaendelea kupanua huduma zake kwa kuingia masoko mapya ya
kikanda, kuimarisha teknolojia za kidijitali, na kuongeza upatikanaji wa huduma kwa wateja wa makundi mbalimbali.
Uongozi wa Benki ya CRDB unashauriwa kuendeleza uwekezaji katika teknolojia bunifu, kuchochea ujumuishaji wa kifedha, kuboresha uzoefu wa mteja, na kuongeza ufanisi wa ndani wa uendeshaji.

Pia, benki iendelee kuwa mdau mkubwa katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kufadhili miradi ya nishati safi, miundombinu ya kimkakati, na biashara baina ya Tanzania na mataifa mengine.

Uimarishaji wa mizania na mahusiano ya kimkakati na wadau wote, zikiwemo taasisi za Serikali, utakuwa msingi imara wa mafanikio ya baadaye ya benki hii.Hata hivyo, katika kufanya hayo yote Benki ya CRDB iendelee kuimarisha uzingatiaji na utekelezaji wa sheria, kanuni na miongozo mbalimbali inayotolewa na Benki Kuu ikiwa ni pamoja na kuzingatia misingi ya utawala bora kama inavyoelekezwa kupitia kanuni za utawala bora kama zilivyoainishwa na

“Banking and Financial Institutions (CorporateGovernance) Regulations 2021” na kuimarisha mifumo na sera za usimamizi wa vihatarishi.