Idara ya Misitu Zanzibar: Nguzo muhimu ya uhifadhi wa mazingira, kukuza utalii na uchumi
Mkurugenzi wa Idara ya Misitu Zanzibar, Said Juma Ali.
Sekta ndogo ya misitu Zanzibar imeendelea kuwa mhimili muhimu katika kulinda mazingira, kukuza utalii na kuchangia maendeleo ya uchumi wa nchi hiyo.
Katika miaka ya hivi karibuni, juhudi mbalimbali zimefanywa na Idara ya Misitu Zanzibar kuhakikisha rasilimali za misitu zinahifadhiwa kwa uendelevu huku zikitumiwa kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.
Misitu ya Zanzibar si tu hazina ya viumbe hai bali pia ni sehemu muhimu ya historia, utamaduni na uchumi wa wananchi wa visiwa vya Unguja na Pemba. Kupitia juhudi za uhifadhi na usimamizi bora, sekta ndogo ya misitu imeanza kuonekana kama kichocheo kipya cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Afisa Utawala na Mipango wa Idara ya Misitu Zanzibar, Jaala Kesi Miraji anasema sekta ndogo ya misitu Zanzibar inahusisha usimamizi wa misitu ya asili, upandaji miti, uhifadhi wa bioanuwai pamoja na matumizi endelevu ya rasilimali za misitu kwa ajili ya maendeleo ya jamii.
Anasema sekta hii ina mchango mkubwa katika kulinda vyanzo vya maji, kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kutoa malighafi muhimu kama kuni, mbao na bidhaa nyingine za misitu. Aidha, misitu ya Zanzibar imekuwa kivutio kikubwa cha utalii wa ikolojia (ecotourism).
Watalii kutoka sehemu mbalimbali za dunia hutembelea maeneo ya misitu ili kujionea uzuri wa mazingira ya asili, ndege adimu, wanyama na mimea mbalimbali inayopatikana katika visiwa hivyo. Kwa mfano, misitu kadhaa ya Zanzibar imehifadhi spishi za kipekee ambazo hazipatikani mahali pen-gine duniani.
Hali hii imeifanya sekta ya misitu kuwa sehemu muhimu ya juhudi za kimataifa za kuhifadhi bioanuwai.
Historia ya Idara ya Misitu Zanzibar
Jaala anaeleza kuwa, Idara ya Misitu Zanzibar ina historia ndefu inayohusiana na juhudi za kulinda rasilimali za misitu tangu enzi za utawala wa kikoloni. Katika kipindi hicho, misitu mingi ilianza kutambuliwa kama maeneo muhimu ya hifadhi kutokana na umuhimu wake katika kulinda vyanzo vya maji na bioanuwai.
Mnyama aina ya Kimapunju (Red Colobus Monkey) ni miongoni mwa vivutio vikubwa vya utalii vinavyopatikana katika Hifadhi ya Taifa ya Msitu wa Jozani.
Baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, Serikali iliendelea kuimarisha usimamizi wa rasilimali za misitu kwa kuanzisha mifumo ya kisasa ya uhifadhi na matumizi endelevu ya misitu. Hapo ndipo Idara ya Misitu ilipoanza kufanya kazi kwa karibu na jamii katika kulinda na kusimamia misitu.
Kwa sasa Idara ya Misitu Zanzibar inasimamia misitu zaidi ya 74 katika visiwa vya Unguja na Pemba, ikiwemo misitu ya hifadhi na maeneo ya asili yenye thamani kubwa ya kiikolojia.
Misitu hii inahifadhi aina mbalimbali za mimea, wanyama na ndege ambao ni muhimu kwa mfumo wa ikolojia wa visiwa hivyo.
Shughuli zinazofanywa na Idara ya Misitu Zanzibar Jaala anabainisha kuwa, Idara ya Misitu Zanzibar inatekeleza majukumu mbalimbali yenye lengo la kulinda na kuendeleza rasilimali za misitu.
Moja ya shughuli kuu ni usimamizi wa misitu ya hifadhi ili kuhakikisha kuwa maeneo hayo yanabaki salama dhidi ya uharibifu kama ukataji miti holela na uchomaji misitu. Pia idara inahamasisha upandaji miti katika maeneo mbalimbali ya visiwa hivyo.
Kampeni za upandaji miti zimekuwa zikifanyika kwa kushirikiana na shule, taasisi za Serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali pamoja na jamii kwa ujumla. Shughuli nyingine ni kufanya tafiti za kisayansi kuhusu bioanuwai ya misitu.
Tafiti hizi husaidia kutambua aina mpya za viumbe na pia kuelewa namna bora ya kuhifadhi rasilimali zilizopo. Aidha, idara inasimamia shughuli za utalii katika baadhi ya misitu ya hifadhi.
Kupitia utalii wa ikolojia, wageni hupata fursa ya kutembelea misitu, kujifunza kuhusu mazingira na kuchangia mapato ya Serikali pamoja na jamii zinazozunguka maeneo hayo.
Elimu ya mazingira pia ni sehemu muhimu ya kazi za Idara ya Misitu. Kupitia semina, warsha na kampeni za uhamasishaji, wananchi hufundishwa umuhimu wa kulinda misitu na kutumia rasilimali zake kwa njia endelevu.
Mafanikio ya Idara ya Misitu Zanzibar
Katika miaka ya hivi karibuni, Idara ya Misitu Zanzibar imepata mafanikio makubwa katika uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya sekta ya utalii wa ikolojia. Mojawapo ya mafanikio hayo ni kuimarika kwa ulinzi wa misitu ya hifadhi na kupungua kwa vitendo vya uharibifu wa misitu.
Aidha, idara imefanikiwa kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa misitu. Wananchi wengi sasa wanashiriki katika shughuli za upandaji miti na uhifadhi wa mazingira.
Misitu mingi ya Zanzibar imeanza kuvutia watalii wanaopenda kutembelea maeneo ya asili. Watalii hawa hutumia huduma mbalimbali kama waongoza watalii, malazi na usafiri, hali inayochangia kuongeza mapato ya wananchi na Serikali.
Kwa upande wa uchumi, sekta ndogo ya misitu imechangia kuongeza ajira kwa vijana na wanawake kupitia shughuli za utalii, vitalu vya miche ya miti na biashara ndogo ndogo zinazohusiana na misitu.
Jaala anasema kutokana na juhudi hizo, sekta hiyo sasa imeanza kuvutia wawekezaji ambapo mpaka sasa kuna mwamko mkubwa wa uwekezaji kutoka ndani ya nje ya nchi.
“Kwa sasa kuna kampuni kubwa ya Kituruki ambayo imewekeza katika msitu wa Jozani ambapo uwekezaji wake unahusisha ujenzi wa hoteli, njia za kuruka msituni (cable line). Uwekezaji huu utasaidia katika kuzalisha nafasi za ajira na kuongeza mapato ya Serikali,” anasema Jaala.
Mchango wa sekta ndogo ya misitu katika kukuza utalii na uchumi Utalii wa misitu umekuwa sehemu muhimu ya sekta ya utalii Zanzibar. Watalii wanaotembelea misitu hupata fursa ya kuona mandhari ya kipekee, kusikia sauti za ndege na kujifunza kuhusu mimea na wanyama wa asili.
Maeneo ya misitu pia hutumika kwa shughuli za utafiti na elimu. Vyuo vikuu na taasisi mbalimbali za kimataifa hutuma watafiti na wanafunzi kujifunza kuhusu bioanuwai ya Zanzibar. Kwa njia hii, Idara ya Misitu inachangia kwa kiasi kikubwa kuifanya Zanzibar kuwa moja ya vituo muhimu vya utalii wa ikolojia barani Afrika.
“Tumekuwa tukishuhudia idadi ya watalii wakija kwa ajili ya kufanya utalii wa misitu ambapo wanajionea wanyama mbalimbali wanaotunzwa na idara kwa kushirikiana na jamii zinazozunguka misitu wakiwemo Ngedere,” anasema Jaala.
Changamoto zinazoikabili sekta ya misitu
Licha ya mafanikio hayo, sekta ndogo ya misitu Zanzibar bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali. Mojawapo ni ongezeko la mahitaji ya ardhi kutokana na ukuaji wa idadi ya watu.
Hali hii husababisha baadhi ya maeneo ya misitu kuvamiwa kwa ajili ya makazi au kilimo.
Changamoto nyingine ni ukataji miti holela kwa ajili ya kuni na mkaa. Ingawa serikali imeweka sheria za kudhibiti shughuli hizi, bado kuna baadhi ya watu wanaokiuka sheria na kusababisha uharibifu wa misitu. Mabadiliko ya tabianchi pia ni tishio kwa misitu ya Zanzibar.
Mabadiliko ya hali ya hewa yanaathiri ukuaji wa miti na bioanuwai ya maeneo ya misitu. Aidha, rasilimali fedha na vifaa kwa ajili ya ulinzi wa misitu bado ni changamoto kwa Idara ya Misitu. Upungufu wa askari wa misitu na vifaa vya doria kwa kiasi fulani unaathiri ufanisi wa usimamizi wa misitu.
Mikakati ya kukabiliana na changamoto
Ili kukabiliana na changamoto hizo, Idara ya Misitu Zanzibar imeweka mika-kati mbalimbali. Moja ya mikakati hiyo ni kuimarisha ushirikiano na jamii katika kulinda misitu. Wananchi wanahusishwa moja kwa moja katika uhifadhi huwa na motisha kubwa ya kulinda rasilimali hizo.
Pia Serikali inaendelea kuimarisha sheria na kanuni za uhifadhi wa misitu pamo-ja na kuongeza doria katika maeneo ya hifadhi. Mikakati mingine ni pamoja na kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala ili kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, pamoja na kupanua programu za upandaji miti katika maeneo yaliyoharibika.
Aidha, Idara ya Misitu inaendelea kushirikiana na mashirika ya kimataifa na taasisi za utafiti ili kupata teknolojia na mbinu bora za uhifadhi wa misitu ikiwemo ulinzi wa misitu kwa kutumia kamera.
Wananchi wazungumza Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, wananchi wamezungumzia kuhusu juhudi za Idara ya Misitu Zanzibar katika kulinda mazingira na kukuza uchumi.
Baadhi ya wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya misitu wanasema kuwa juhudi za idara hiyo zimeongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kulinda misitu.
“Ni kweli sasa hivi tunaona Serikali ikifanya juhudi katika kulinda misitu japokuwa bado baadhi ya watu wanavamia kwa ajili ya kulima kutokana na kukosa maeneo ya kufanya hivyo," anasema Mahamudu Salimu Badru mkazi wa Michenzani Zanzibar.
Naye mmoja miongoni mwa wanavijiji wanaoishi karibu na Hifadhi ya Msitu wa Jozani Mohammed Ali Mchobwa anasema kuwa kwa sasa wanafaidika na hifadhi hiyo kwa kupokea fedha kutoka katika mgao wa kila mwaka na kufanikiwa kujenga skuli kwa maendeleo ya watoto wao.
“Zamani walikuwa watoto wanapata tabu sana maana wanatembea masafa marefu kufuata elimu kwenye vijiji vya mbali kama vile Kitogani na Muyuni, lakini hivi sasa tumefanikiwa kujenga skuli kutokana na mgao wa fedha zinazotokana na ulinzi wa msitu,” anasema Mchobwa.
Idara ya Misitu Zanzibar imeendelea kuwa na mchango mkubwa katika kulinda rasilimali za misitu, kukuza utalii na kuchangia maendeleo ya uchumi wa visiwa hivyo.
Licha ya changamoto zinazokabili sekta ndogo ya misitu, juhudi za Serikali, ushirikiano wa wadau na uhamasishaji wa jamii vinaweza kuhakikisha kuwa misitu ya Zanzibar inaendelea kuhifadhiwa na kutumika kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa kuendelea kuimarisha mikakati ya uhifadhi na matumizi endelevu ya mis-itu, Zanzibar inaweza kuwa mfano bora wa namna rasilimali za asili zinavyoweza kulindwa huku zikichangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.