Palipo na maji, usawa hustawi: UNICEF inavyoshirikiana na wadau kuimarisha upatikanaji wa maji safi kwa kila mtoto nchini
Hakuna tena kutembea kwa miguu umbali mrefu kutafuta maji vijijini: Tabasamu la Tausi linaeleza kila kitu anapofurahia maji yanayotiririka kutoka kwenye bomba la jamii katika kijiji cha Kagalula. Kuleta maji salama karibu na makazi kunaokoa muda kwa wasichana na wanawake, na kufungua fursa zaidi za kujifunza, ustawi, na maisha ya kila siku katika jamii (©UNICEF Tanzania /2024).
Tausi, binti mwenye umri wa miaka 12 anayeishi katika kijiji cha Kaguruka mkoani Kigoma, alikuwa analazimika kuanza siku yake kwa safari ndefu na yenye kuchosha ya kutafuta maji.
Safari hiyo mara nyingi ilimwacha akiwa mchovu, akichelewa darasani, au kushindwa kushiriki kikamilifu katika masomo yake.
Leo hii, maji safi yanatiririka hatua chache tu kutoka nyumbani kwao. Sasa anapata muda wa kutosha kujifunza, kupumzika, na kucheza.
“Maji yapo hapa; tunafurahi; hatuugui tena. Kupatikana kwa maji karibu na nyumbani kumebadilisha maisha yangu. Naweza kuhudhuria shule mara kwa mara, na nimefanya vizuri darasani mwaka huu,” anasema Tausi.
Kama ilivyo kwa Tausi, Ashura anakumbuka alivyokuwa akilazimika kuamla alfajiri ili kutafuta maji katika kijiji hicho hicho cha Kaguruka.
Paneli ya umeme wa jua inayoendesha mfumo wa maji wa jamii katika Mkoa wa Kigoma inapanua huduma za maji zinazohimili mabadiliko ya tabianchi. Huduma hizi zinasogeza maji salama karibu na familia na kuwaondolea wanawake na watoto adha ya kutembea umbali mrefu (© UNICEF Tanzania /2026/Magari)/2024/Studio 19).
Kama ilivyo kwa wanawake wengi vijijini , hapo awali Ashura alitumia muda mwingi kutembea umbali mrefu kwenda kuchota maji kwa ajili ya familia yake. Safari hiyo ilikuwa ya kuchosha, mara nyingi maji hayakuwa salama, na watoto wake walikuwa wakiugua mara kwa mara.
Leo, maji safi yanatiririka kutoka kwenye bomba la jirani, shukrani kwa mifumo ya maji ya jamii inayofadhiliwa na UNICEF kwa ushirikiano na Serikali na wadau.
Watoto wake sasa wanahudhuria shule mara kwa mara, na familia inatumia muda mchache kutafuta maji na badala yake kutumia muda mwingi zaidi kujifunza, kutafuta kipato, na kujenga kesho yao.
Hadithi kama za Tausi na Ashura zinazidi kuwa za kawaida kadiri upatikanaji wa maji safi unavyoongezeka ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jambo linalopunguza mzigo kwa wanawake na wasichana, likiboresha matokeo ya afya, na kuwaruhusu watoto kubaki shuleni.
Kaulimbiu ya Wiki ya Maji duniani mwaka huu ni “Maji na Usawa wa Kijinsia: Palipo na maji, usawa hustawi,” inasisitiza jinsi upatikanaji sawa wa maji safi unavyofungua njia kwa wanawake na wasichana, kusaidia maendeleo ya jamii, na kutengeneza fursa kwa vizazi vijavyo.
Nchini kote, upatikanaji wa maji safi unabadilisha maisha ya wanawake na watoto. Kuanzia vijijini hadi shuleni na vituo vya afya, UNICEF, kwa kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, washirika wa maendeleo, asasi za kiraia, pamoja na jamii, inatoa msaada kwa watoto na familia ili wastawi huku ikikuza usawa wa kijinsia na kujenga mustakabali imara na wenye afya zaidi.
Paneli ya umeme wa jua inayoendesha mfumo wa maji wa jamii katika Mkoa wa Kigoma inapanua huduma za maji zinazohimili mabadiliko ya tabianchi. Huduma hizi zinasogeza maji salama karibu na familia na kuwaondolea wanawake na watoto adha ya kutembea umbali mrefu (© UNICEF Tanzania /2026/Magari)/2024/Studio 19).
Maji katika Jamii: Kusogeza maji karibu na familia
Katika maeneo mengi ya vijijini nchini Tanzania, wanawake na wasichana bado wana jukumu la kutafuta maji kwa ajili ya kaya zao.
Muda unaopotea huzuia fursa za elimu, uzalishaji wa kipato, na mapumziko; hali inayozifanya familia kubaki katika mzunguko wa umaskini na kuzuia fursa kwa wanawake na watoto.
Ili kukabiliana na changamoto hizi, UNICEF inafanya kazi Tanzania Bara na Zanzibar, kwa ushirikiano na Serikali ya Tanzania, na kwa msaada kutoka kwa washirika wa maendeleo ili kupanua mifumo ya usambazaji wa maji inayoweza kuhimili athari za hali ya hewa na kuboresha upatikanaji wa maji safi kwa jamii.
Paneli ya umeme wa jua inayoendesha mfumo wa maji wa jamii katika Mkoa wa Kigoma inapanua huduma za maji zinazohimili mabadiliko ya tabianchi. Huduma hizi zinasogeza maji salama karibu na familia na kuwaondolea wanawake na watoto adha ya kutembea umbali mrefu (© UNICEF Tanzania /2026/Magari)/2024/Studio 19).
Mkoa wa Kigoma ni mfano wa mkakati huu. Kupitia ujenzi wa visima vinavyotumia nishati ya jua, mitandao ya mabomba, na mifumo ya kisasa ya usambazaji maji inayozingatia mabadiliko ya tabianchi, UNICEF inatoa huduma ya uhakika ya maji safi ya kunywa kwa kaya za vijijini, ikiwafikia karibu watu 200,000 katika zaidi ya vijiji 30 na kupunguza kwa kiasi kikubwa mzigo kwa wanawake na watoto.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, programu zinazofadhiliwa na UNICEF zimesaidia kutoa huduma za maji safi kwa zaidi ya watu milioni saba kote Tanzania, ikionyesha nguvu ya ushirikiano madhubuti na uongozi wa ndani.
Maji yanapopatikana karibu na nyumbani, watoto wanakuwa na afya njema na kuhudhuria shule mara kwa mara, huku wanawake wakipata muda wa kujishughulisha na shughuli za kujiingizia kipato na uongozi.