Ujenzi wa uhusiano muhimu kati ya maji safi na huduma za kijamii nchini
Miradi ya dharura ya Majisafi, Usafi wa Mazingira na Usafi Binafsi (WASH) inayofadhiliwa na UNICEF katika Wilaya ya Biharamulo wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa Marburg iliimarisha upatikanaji wa maji salama na huduma za usafi katika jamii na vituo vya afya; kusaidia kulinda watoto, familia, na wahudumu wa afya wakati ambapo upatikanaji wa maji safi ulikuwa jambo la muhimu zaidi. (© UNICEF Tanzania /2024).
Upatikanaji wa maji safi ni msingi wa huduma bora za jamii, ukifanya kazi kama kichocheo cha maboresho katika sekta za elimu, afya, na mazingira kote nchini.
UNICEF, kwa kushirikiana na Serikali, inaleta mabadiliko katika sekta hizi kwa kutekeleza miradi ya Majisafi na Usafi wa Mazingira (WASH) inayostahimili mabadiliko ya tabianchi, ambayo inalinda utu wa watoto na kuhakikisha mwendelezo wa huduma muhimu za jamii.
Usambazaji maji shuleni: Kulinda utu na ujifunzaji
Katika mikoa ya Iringa, Mbeya, Njombe, Songwe, na Kigoma pamoja na kule visiwani Zanzibar, huduma bora za maji na usafi wa mazingira shuleni zinaimarisha afya, utu, na ushiriki kamilifu wa watoto kwenye masomo.
Miundombinu ya uhakika husaidia kupunguza utoro na kuhakikisha mazingira salama na rafiki ya kujifunzia hususan kwa wasichana, ambao wanahitaji faragha na vifaa salama vya usafi ili kujistiri kwa kujiamini na amani hususan wakati wa hedhi.
Katika shule nyingi, ukosefu wa maji ya uhakika ulisababisha watoto kuhangaika kupata maji salama ya kunywa, kunawa mikono, au kusafisha miili yao wakati wa masomo.
Kwa wasichana, ilikuwa tofauti, kutokana na usafi duni walilazimika kukosa vipindi vya masomo kila mwezi hususan pale wanapokua katika hedhi, jambo ambalo lilidhoofisha maendeleo yao ya kitaaluma na kuongeza pengo la usawa dhidi ya wavulana.
UNICEF, kwa kushirikiana na Serikali na washirika wengine, imesaidia juhudi za kusogeza maji safi karibu na shule kwa kujenga na kukarabati miundombinu ya maji safi na mazingira inayohimili mabadiliko ya tabianchi na rafiki kwa watoto.
Miundombinu hii ni salama kwa watoto na ina uwezo wa kuhimili changamoto za hali ya hewa kama vile ukame wa muda mrefu au mafuriko.
Uwekezaji huu unakamilishwa na programu za mabadiliko ya tabia shuleni ambazo huwashirikisha watoto katika kujifunza na kushiriki katika shughuli za usafi na kuweza kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Maarifa haya yanazigusa mpaka jamii zao, ambapo watoto wanageuka kuwa mawakala wa mabadiliko.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, huduma na miundombinu bora ya majisafi na usafi wa mazingira imeanzishwa au kukarabatiwa katika zaidi ya shule 110 kote Tanzania, ikiwafikia zaidi ya wanafunzi 92,000, wakiwemo wasichana 48,000.
Mchanganyiko huu wa programu za kubadilisha tabia zinazoendeshwa mashuleni na ujenzi wa miundombinu, unasaidia kuweka mazingira ya kujifunzia yaliyo salama, yenye afya na jumuishi zaidi.
Upatikanaji wa maji salama kwa wasichana balehe, vyoo vya faragha, na maeneo safi ya kujistiri wakati wa hedhi, unawahakikishia fursa ya kuhudhuria masomo kwa kujiamini na heshima. Hiiinathibitisha kuwa maji yanapopatikana shuleni, usawa wa kijinsia nao hustawi.
Paneli ya umeme wa jua inayoendesha mfumo wa maji wa jamii katika Mkoa wa Kigoma inapanua huduma za maji zinazohimili mabadiliko ya tabianchi. Huduma hizi zinasogeza maji salama karibu na familia na kuwaondolea wanawake na watoto adha ya kutembea umbali mrefu (© UNICEF Tanzania /2026/Magari)/2024/Studio 19).
Usambazaji maji katika vituo vya afya: Kulinda akina mama na watoto wachanga
Upatikanaji wa maji wa uhakika ni hitaji la lazima kwa huduma za afya salama na zenye ubora wa hali ya juu. Bila maji, wahudumu wa afya hawawezi kunawa mikono yao, kusafisha vifaa vya matibabu, au kudumisha viwango vya usafi vinavyohitajika ili kusaidia uzazi salama na kutibu wagonjwa. Hali hii inawaweka akina mama, watoto wachanga na jamii nzima katika hatari ya maambukizi ya magonjwa yanayozuilika.
Sabrina, mama kutoka kijiji cha Sasama mkoani Songwe, anasimulia alivyokuwa na hofu kujifungulia katika kituo chake cha afya cha karibu kutokana na ukosefu wa maji na usafi.
“Nilikuwa nasita kujifungulia hapa kituoni kutokana na matatizo haya yote ya maji na usafi wa mazingira. Sikutaka kuhatarisha afya yangu au ya mtoto wangu. Lakini kujifungulia nyumbani bila mkunga mwenye ujuzi kulikuwa na hatari vile vile,” anasema Sabrina.
Hii ndiyo sababu ni muhimu zaidi kuimarisha huduma katika vituo vya afya ili kuboresha udhibiti wa maambukizi na kuhakikisha huduma salama kwa akina mama na watoto wachanga.
Katika mikoa ya Songwe, Mbeya, na Kagera, UNICEF imesaidia kuboresha miundombinu ya majisafi na usafi wa mazingira inayohimili mabadiliko ya tabianchi na mifumo ya udhibiti wa taka za afya, hali inayoongeza ubora wa huduma na kunufaisha zaidi ya watu 100,000, ikiwa ni pamoja na idadi kubwa ya wanawake na watoto.
Vituo hivi sasa vina upatikanaji wa maji wa uhakika, vyoo vilivyoboreshwa, sehemu salama za kunawia mikono, huduma za kufulia, na mifumo sahihi ya udhibiti wa taka.
Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, programu zinazofadhiliwa na UNICEF zimeimarisha huduma hizi katika vituo vya afya zaidi ya 90 kote nchini, zikiwanufaisha akina mama, watoto wachanga, wahudumu wa afya, na wagonjwa zaidi ya 300,000 kwa ujumla.
Maboresho haya yanapunguza maambukizi, yakimlinda mama wakati wa kujifungua na kuhakikisha mtoto mchanga anaanza maisha katika mazingira safi na salama.
Usambazaji maji wakati wa dharura: Kulinda watoto wakati wa uhitaji mkubwa
Wakati wa dharura, upatikanaji wa maji safi na salama ni jambo lisilohitaji mjadala. Iwe ni kukabiliana na milipuko ya magonjwa, mafuriko, au majanga ya asili, huduma za uhakika za majisafi na usafi wa mazingira hulinda watoto na jamii dhidi ya maambukizi na changamoto nyingine za kimaisha.
Wakati wa mlipuko wa virusi vya Marburg mkoani Kagera, UNICEF ikifanya kazi kwa karibu na Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine, ilitekeleza mpango wa dharura katika Wilaya ya Biharamulo. Mpango huo ulisaidia kuboresha upatikanaji wa maji katika Hospitali ya Wilaya ya Biharamulo, ambayo ilitumika kama Kituo Kikuu cha Matibabu ya ugonjwa wa Marburg.
Mpango huo ulihusisha uchimbaji wa kisima kipya, ujenzi wa tanki kubwa la maji la lita 50,000, ujenzi wa kituo cha pampu, na uunganishaji maji kwenye majengo ya hospitali ili kuhakikisha huduma ya saa 24 inakuwepo bila kukatika.
Aidha, katika kijiji cha Katerela, ambacho kilikuwa kitovu cha ugonjwa huo, UNICEF ilisaidia ufungaji wa mfumo wa nishati ya jua, ujenzi wa tanki lingine la lita 50,000, na kuwajengea uwezo wajumbe wa kamati ya maji ya jamii ili kuhakikisha uendelevu wa huduma hizo. Hatua hizi za dharura za mpango wa maji safi na usafi wa mazingira ziliwafikia zaidi ya watu 400,000, wakiwemo watoto zaidi ya 220,000.
Vilevile, juhudi hizi ni muhimu zaidi katika kambi za wakimbizi na maeneo yaliyoathiriwa na majanga ya asili kama maporomoko ya ardhi wilayani Hanang na mafuriko kule Rufiji.
Katika maeneo haya, maji safi na usafi wa mazingira huzuia magonjwa kama kuhara na kipindupindu. Hata baada ya kadhia hizo kupita, uwekezaji huu unaendelea kuhudumia jamii, kusaidia watoto waendelee kubaki salama na wastahimilivu.
Paneli ya umeme wa jua inayoendesha mfumo wa maji wa jamii katika Mkoa wa Kigoma inapanua huduma za maji zinazohimili mabadiliko ya tabianchi. Huduma hizi zinasogeza maji salama karibu na familia na kuwaondolea wanawake na watoto adha ya kutembea umbali mrefu (© UNICEF Tanzania /2026/Magari)/2024/Studio 19).
Huduma himilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi: Kuandaa watoto kwa ajili ya kesho bora ya upatikanaji wa maji
Mabadiliko ya tabianchi tayari yanabadilisha maisha ya watoto nchini kupitia uhaba wa maji, mafuriko, na milipuko ya magonjwa. UNICEF inafanya kazi kwa kushirikiana na Serikali kujenga mifumo thabiti inayolinda ustawi wa watoto na kuhakikisha mwendelezo wa masomo na huduma za afya.
Hii ni pamoja na kuimarisha miundombinu, kukuza shughuli za uhifadhi wa maji kama upandaji miti, na kuwapa vijana ujuzi wa kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi.
Huko Zanzibar, UNICEF inashirikiana na Serikali kuimarisha ushiriki wa vijana katika miradi ya kukabili mabadiliko ya tabianchi katika shule za sekondari 216 katika wilaya zote 11 za Unguja na Pemba.
Uwekezaji huu unajumuisha ujenzi wa vyoo 23 vyenye matundu 190 na mifumo ya maji ya uhakika katika shule 13 kule Pemba. Kupitia klabu za maji safi na usafi wa mazingira mashuleni zijulikanazo kama ‘SWASH Club’, wanafunzi wanajifunza kuwa mabalozi wa uhifadhi wa maji na usafi. Vilabu hivi vinawawezesha watoto kubadili tabia zao na kuwahimiza wazazi wao kulinda vyanzo vya maji. Mbali na hilo, UNICEF inasaidia vijana kushiriki katika mijadala ya kitaifa na kimataifa ya tabianchi ili sauti zao ziweze kuleta masuluhisho ya siku za usoni.
Uimarishaji mifumo: Msingi wa maji endelevu na usawa
Nyuma ya kila kituo cha maji kinachofanya kazi, choo salama cha shule, au sehemu ya kunawia mikono katika kituo cha afya, kuna mfumo imara, unaowajibika, na wenye rasilimali za kutosha. Tanzania imepiga hatua kubwa katika kupanua upatikanaji wa maji safi; kulingana na Mpango wa Pamoja wa Ufuatiliaji wa WHO/UNICEF (JMP), idadi ya watu wanaotumia huduma za msingi za maji iliongezeka kutoka asilimia 50 mwaka 2015 hadi asilimia 64 mwaka 2024.
Hata hivyo, kudumisha mafanikio haya kunahitaji sera madhubuti, taasisi zenye uwezo, na mifumo imara ya ufuatiliaji.
UNICEF inasaidia juhudi za Serikali katika kuimarisha mifumo ya kitaifa na ya mikoani kwa ajili ya kupanga bajeti na kusimamia uwajibikaji. Mifumo ya ufuatiliaji inaboreshwa kupitia majukwaa ya kidijitali na miongozo ya takwimu ili kuhakikisha huduma zinadumu muda mrefu baada ya miradi kukamilika.
Vilevile, UNICEF inasaidia hatua za kisekta kuhusu mahitaji ya wasichana balehe kupitia miongozo ya kitaifa ya hedhi salama pamoja na nyenzo zake za kuetendea kazi. Juhudi hizi za kimfumo ni muhimu kwa sababu maji na usawa wa kijinsia haviwezi kutenganishwa.
Ukosefu wa usawa wa kimfumo huamua nani anapata huduma, nani anapata kwa uchache, na nani anashiriki katika kufanya maamuzi. Kwa kuimarisha mifumo na kujumuisha viwango vinavyozingatia jinsia, UNICEF inahakikisha maendeleo yanawafikia wale walioachwa nyuma zaidi, hususan wasichana.
Paneli ya umeme wa jua inayoendesha mfumo wa maji wa jamii katika Mkoa wa Kigoma inapanua huduma za maji zinazohimili mabadiliko ya tabianchi. Huduma hizi zinasogeza maji salama karibu na familia na kuwaondolea wanawake na watoto adha ya kutembea umbali mrefu (© UNICEF Tanzania /2026/Magari)/2024/Studio 19).
Ushirikiano: Kufanya kazi pamoja kwa huduma za maji endelevu
Kupanua upatikanaji wa maji safi nchini kunahitaji ushirikiano thabiti na wa kudumu. Maendeleo ya dhati yanategemea hatua zilizoratibiwa na uwekezaji wa muda mrefu kutoka kwa Serikali, washirika wa maendeleo na jamii.
UNICEF inafanya kazi kwa karibu na wizara mbalimbali kama vile Wizara ya Maji, Wakala wa maji vijijini - RUWASA, Wizara ya Afya, Wizara ya Elimu, na TAMISEMI. Kule Zanzibar, inashirikiana na Wizara ya Maji, Nishati na Madini (MoWEM) na Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA). Ushirikiano huu unahakikisha umiliki wa kitaifa wa miradi ya maji na kuimarisha utekelezaji wa sera ili huduma ziwafikie watoto walio hatarini zaidi.
Juhudi hizi zinawezekana kupitia msaada wa wahisani kama Serikali za Uholanzi, Japan, Ireland, Norway, Jamhuri ya Korea, na mashirika kama Grundfos Foundation, Education Above All, Qatar Fund for Development, na CDC ya Marekani. Pia, UNICEF inashirikiana na asasi za kiraia kama Water Mission, Red Cross Tanzania, na nyinginezo ambazo uwepo wao katika jamii unahakikisha masuluhisho ya maji yanadumu. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, zaidi ya watoto na familia milioni 7.5 wamefikiwa na huduma za majisafi na usafi wa mazingira.
Hitimisho: Kesho yenye usawa wa kijinsia unaokua kwa kasi
Maji yanapotiririka karibu na nyumbani, maisha yanabadilika. Msichana anafika shuleni kwa wakati badala ya kutembea umbali mrefu. Mama anajifungua katika kituo safi na salama. Familia zinakunywa maji salama, zinafanya usafi, na zinajiweka mbali na magonjwa ya maambukizi. Jamii zinaimarika zaidi pale ambapo muda, usalama, na fursa vinarudishwa kwa wanawake na wasichana.
Lakini usawa wa kweli unahitaji zaidi ya upatikanaji wa uhakika wa maji salama. Inahitaji kuhakikisha kuwa wanawake na wasichana siyo tu wapokeaji wa huduma za maji, bali ni washiriki hai katika kuzianzisha.
Wanawake na wasichana wanaposhirikishwa kikamilifu katika kupanga, kufanya maamuzi, na usimamizi wa maji, masuluhisho yanakidhi mahitaji ya watu vizuri zaidi, yanakuwa endelevu, na yenye usawa zaidi.
Kwa sababu, mahali ambapo maji yanatiririka, na mahali ambapo wanawake na wasichana wanapewa fursa ya kuongoza, usawa wa kijinsia hustawi.