Tanroads: Mizani na mitambo ya kisasa inavyolinda barabara nchini
Meneja wa Uendeshaji wa Mizani wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mussa George.
Serikali inaendelea kuwekeza fedha nyingi kujenga na kuboresha barabara kuu na za mikoa ili kurahisisha usafirishaji wa watu na mizigo, kukuza biashara na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Hata hivyo, uwekezaji huo unaweza kupoteza thamani iwapo barabara hazitalindwa dhidi ya uharibifu unaotokana na magari yenye uzito unaozidi kiwango kilichoruhusiwa.
Meneja wa Uendeshaji wa Mizani wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Mussa George, anasema moja ya sababu kubwa zinazoharibu barabara ni magari yenye mizigo iliyopitiliza uwezo ambao barabara zilisanifiwa kuubeba.
Anasema kila barabara hujengwa kwa kuzingatia kiwango maalumu cha uzito wa magari kinachoweza kupita bila kuiharibu. Hivyo, usimamizi wa uzito wa magari kupitia mizani ni sehemu muhimu ya kulinda uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika sekta ya barabara.
“Serikali inatumia fedha nyingi kujenga barabara. Hivyo ni lazima tuzilinde. Mojawapo ya njia za kuzilinda ni kuhakikisha magari yanayotumia barabara hayazidishi uzito ulioruhusiwa,” anasema.
Kwa mujibu wa Mhandisi George, TANROADS kwa sasa ina jumla ya mizani 105 nchini kote, ambayo imegawanyika katika aina mbili; mizani ya kudumu (fixed au static) na mizani ya kuhamishika (portable au mobile).
Anasema kati ya mizani hiyo, 83 ni ya kudumu ambayo imejengwa katika maeneo maalumu na haihamishiki, huku mizani 22 ikiwa ya kuhamishika, inayoweza kupelekwa katika maeneo mbalimbali kulingana na mahitaji ya usimamizi wa uzito wa magari.
“Mikoa yote nchini ina mizani, hatupangi mizani kwa kuzingatia tu kwamba kila mkoa lazima uwe nayo, bali tunaangalia umuhimu wa shoroba za usafirishaji (transport corridors),” anasema.
Kwa mwaka wa fedha 2026/27 wanatarajia kuongeza mizani mitano yenye mfumo wa kisasa isiyotumia muhudumu kituoni (unmanned way station) na mizani 15 ya kupima gari ikiwa kwenye mwendo,
Upimaji wa magari katika vituo vya mizani hufanyika kwa kufuata utara¬tibu maalumu unaolenga kubaini uzito wa kila mtahimbo (axle) kabla ya kupima uzito wa gari zima na gari linapoingia kwenye mzani, kila mtahimbo hupimwa moja baada ya nyingine ili kujiridhisha kuwa haujazidi kiwango cha uzito kinachoruhusiwa.
Lori likiwa kwenye mzani uliopo Chunya mkoani Mbeya jambo linlaoendelea kulinda barabara.
Anasema utaratibu huu ni muhimu kwa sababu hata kama uzito wa jumla wa gari uko ndani ya kiwango kinachoruhusiwa, mtahimbo mmoja unaweza kuwa umebebeshwa mzigo mkubwa zaidi na hivyo kuongeza hatari ya kuharibu barabara au madaraja.
“Baada ya kukamilisha upimaji wa mitahimbo yote, mfumo wa mizani hukokotoa uzito wa jumla wa gari pamoja na mzigo wake na kulinganisha matokeo hayo na viwango vilivyowekwa kisheria. Endapo uzito wa mtahimbo wowote au uzito wa jumla wa gari utabainika kuzidi kiwango kinachoruhusiwa, mmiliki au dereva huchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria, kwa kutozwa faini, kupunguza mzigo au kupanga vizuri kabla ya kuendelea na safari,”anasema Mhandisi George.
“Lengo la faini si kuongeza mapato, bali kuhakikisha sheria zinafuatwa na kuzuia uharibifu wa barabara unaotokana na magari yenye uzito uliopitiliza,” anasema.
Anasema mfumo huu wa upimaji unasaidia kuhakikisha uzito unasambazwa kwa usahihi kwenye gari, kulinda miundombinu ya barabara na kuongeza usalama kwa watumiaji wote wa barabara.
Hata hivyo, anasema mizani mingi imewekwa kwenye barabara kuu zinazounganisha mikoa au zinazounganisha Tanzania na nchi jirani kutokana na kuwa na msongamano mkubwa wa magari ya mizigo.
Mhandisi George anasema barabara ya TANZAM inayotoka Dar es Salaam kupitia Morogoro, Iringa na Mbeya hadi Tunduma mpakani mwa Zambia, akisema ni moja ya shoroba muhimu zenye magari mengi ya mizigo, hivyo usimamizi wa uzito ni wa lazima.
Anasema kabla ya kufunga mzani katika eneo fulani, TANROADS hufanya tathmini ya shoroba husika na kuangalia kama kuna haja ya kuwepo kituo cha kupimia uzito ili kulinda barabara mpya au iliyoboreshwa.
“Iwapo tunajenga barabara mpya na tunaona hakuna mzani katika shoroba hiyo, tunaweza kuamua kuweka mzani ili kuhakikisha barabara hiyo inalindwa dhidi ya uharibifu unaoweza kusababishwa na magari yenye uzito uliopitiliza,” anasema.
Anasema magari yote ya mizigo yenye uzito wa tani 3.5 na kuendelea yanapaswa kuingia kwenye mizani kwa ajili ya kupimwa kabla ya kuendelea na safari.
Upimaji huo hufanyika kwa kuzingatia Sheria ya Udhibiti Uzito wa magari Afrika Mashariki ya mwaka 2016 pamoja na kanuni zake za mwaka 2018, ambazo zinaelekeza kiwango cha uzito kinachoruhusiwa kwa kila ekseli na jumla ya uzito wa gari.
Mbali na sheria hiyo, TANROADS pia hutumia kanuni ya mwaka 2018 inayotoa mwongozo wa uendeshaji wa mizani, usimamizi wa watumishi, matumizi ya vifaa na taratibu mbalimbali za ndani.
Mhandisi George anasema mwongozo huo unasaidia kuhakikisha vituo vyote vya mizani vinaendeshwa kwa viwango vinavyofanana na watumishi wanazingatia taratibu zilizowekwa.
“Lengo letu si kuwaadhibu watu, bali kuhakikisha sheria zinafuatwa na barabara zinalindwa ili zidumu kwa muda uliokusudiwa wakati wa usanifu wake,” anasema.
Anasema kutokana na kuongezeka kwa shughuli za uchumi na biashara, idadi ya malori yanayotumia barabara kuu imeongezeka kwa kiasi kikubwa, jambo linaloongeza umuhimu wa kuimarisha usimamizi wa mizani.
Kwa mfano, katika shoroba ya TANZAM, mamia ya malori husafirisha mizigo kwenda na kutoka nchi za kusini mwa Afrika kila siku. Bila udhibiti wa uzito, anasema, barabara hiyo ingeweza kuharibika mapema na kuigharimu Serikali fedha nyingi za matengenezo.
Anasema mizani si kikwazo kwa wafanyabiashara wala wasafirishaji, bali ni nyenzo muhimu ya kulinda miundombinu ya Taifa na kuhakikisha barabara zinaendelea kutoa huduma kwa ufanisi kwa miaka mingi ijayo.
Changamoto katika mizani
Licha ya mafanikio yaliyopatikana katika kusimamia uzito wa magari, bado kuna changamoto kadhaa zinazoathiri ufanisi wa upimaji.
Mhandisi George anasema changamoto kubwa ni ongezeko kubwa la idadi ya malori yanayosafirisha mizigo kutokana na kukua kwa shughuli za uchumi na biashara ndani na nje ya nchi, hususani kwenye shoroba kuu za usafirishaji kama TANZAM, ambako magari hupita kwa wingi kila siku.
“Kama tunavyotambua Rais Samia Suluhu Hassan amefungua bandari yetu idadi ya malori inaongezeka, hilo linaongeza shinikizo kwenye vituo vya mizani na wakati mwingine husababisha foleni,” anasema.
Anasema TANROADS imekuwa ikikabiliana na hali hiyo kwa kutumia mizani ya kupima gari ikiwa kwenye mwendo ili kupunguza foleni.
Pia, anasema TANROADS imeweka utaratibu wa kufanya matengenezo ya mara kwa mara pamoja na ukaguzi wa kitaalamu ili kuhakikisha mizani inaendelea kutoa matokeo sahihi na yanayoaminika.
Vilevile usimamizi wa mizani, kuimarisha ushirikiano na wadau wa sekta ya usafirishaji pamoja na kufanya tathmini za mara kwa mara ili kubaini maeneo yanayohitaji vituo vipya vya mizani.
Lori aina ya Fuso likiwa limegonga kibanda cha mlinzi katika mzani wa Vigwaza mkoani Pwani na kusababisha kusimama kwa muda shughuli za upimaji.
Anasema hatua hizo zinalenga kuhakikisha barabara za Taifa zinalindwa, gharama za matengenezo zinapungua na uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika ujenzi wa miundombinu unaendelea kunufaisha wananchi kwa muda mrefu.
Vibali maalumu kwa mizigo
Meneja huyo anasema pamoja na kusimamia uzito wa magari ya mizigo, TANROADS ina utaratibu maalumu kwa magari yanayosafirisha kemikali pamoja na yale yanayobeba mizigo mizito kupita kiwango cha kawaida (abnormal loads).
Anasema magari hayo hayaruhusiwi kuanza safari bila kupata kibali maalumu kutoka Wizara ya Ujenzi, ambapo waombaji hulazimika kuwasilisha taarifa za mzigo, njia watakayotumia pamoja na kulipia ada zinazotakiwa kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
“Magari yanayobeba mizigo ya kemikali au mizigo mizito isiyo ya kawaida yanapaswa kuomba kibali kabla ya kutumia barabara, hii hutuwezesha kujiridhisha safari hiyo haitasababisha uharibifu wa miundombinu na hatua zote za kiusalama zimezingatiwa,” anasema.
Anasema utaratibu huo husaidia kupanga njia salama za kupitisha mizigo hiyo, kulinda madaraja na barabara pamoja na kupunguza athari kwa watumiaji wengine wa barabara.
Mbali na hizo, anasema changamoto nyingine ni kutokea kwa ajili katika mizani kwa magari kushindwa kufunga breki pamoja na uzimikaji wa magari katika mizani.
“Kumeshatokea ajali siku ya hivi karibuni katika kituo cha Vigwaza kwa Fuso kugonga kibanda cha mlinzi pia magari kuzimika kabla na baada ya kupimwa na kusababisha shughuli za upimaji kusimama kwa muda,”anasema Mhandisi huyo.
Anasema hatua ambazo huchukuliwa ni kufanya tathimini kwa gari litakalogonga kituo na kulipishwa huku kwa magari yaliyozimika yakionolewa na magari maalum (Breakdown) kwa gharama za mwenye gari.
Utaratibu wa maegesho ya mizani
Kuhusu magari yanayozuiliwa katika vituo vya mizani, Mhandisi George anasema TANROADS imeweka utaratibu unaowapa waendeshaji muda wa kurekebisha kasoro zilizobainika bila gharama za awali.
Anasema gari linalozuiliwa katika maegesho ya mizani huruhusiwa kukaa kwa siku tatu bila kulipa ada yoyote.
Hata hivyo, iwapo litashindwa kuondolewa ndani ya kipindi hicho, mmiliki au mwendeshaji atalazimika kulipa ada ya dola za Marekani 50 kwa kila siku ya ziada ambalo gari litaendelea kubaki kwenye maegesho hayo.
“Utaratibu huu unalenga kuhakikisha maeneo ya maegesho hayazidiwi na magari yaliyokiuka taratibu, huku ukiwahamasisha wamiliki wa magari kuchukua hatua kwa wakati ili kurekebisha kasoro na kuendelea na safari zao kwa kuzingatia sheria,” anasema.
Matumizi mzani wa Kurasini
Mbali na mizani ya barabra kuu, taasisi hiyo imeweka huduma ya mzani eneo la Kurasini (pre-weighing scale) inayowasaidia madereva na wasafirishaji kujihakikishia uzito wa magari yao kabla ya kuanza safari.
Anasema huduma hiyo hutolewa bila malipo, ikiwa ni sehemu ya jitihada za TANROADS kuwasaidia wasafirishaji kuzingatia sheria na kuepuka adhabu zitakazojitokeza kwa kuzidisha uzito.
“Mzani wa Kurasini hauna malipo yoyote lengo lake ni kumpa dereva nafasi ya kujua uzito wa gari lake mapema kabla hajaanza safari. Endapo ataona amezidisha mzigo, anaweza kuchukua hatua mapema kabla ya kufika vituo vingine.”
Mhandisi George anasema huduma hiyo imekuwa ikisaidia kupunguza migogoro kati ya wasafirishaji na wasimamizi wa mizani, huku ikiongeza uelewa kwa madereva kuhusu umuhimu wa kufuata viwango vya uzito vinavyoruhusiwa.
Anasema madereva wanapaswa kutumia fursa hiyo badala ya kukwepa na kuwa chanzo cha malalamiko wanapokutwa wamezidisha uzito kwa kutumia mizani binafsi ya eneo la bandari kabla ya kujiridhisha na ule wenye viwango mahususi.
“Hatua yetu ni kuwezesha uzingatiaji wa sheria kwa kutoa huduma rafiki, tunawahimiza wasafirishaji wote kutumia mzani wa Kurasini kujihakikishia uzito wa magari yao,” anasema.
Kwa mujibu wake, matumizi ya mzani huo yamechangia kuongeza utii wa sheria kwa baadhi ya kampuni, kupunguza idadi ya magari yanayobainika na uzito uliozidi kiwango kinachoruhusiwa.
Mizani ngao ya kulinda barabara
Msimamizi wa Kituo cha Mingoyo Kaskazini, Godfrey Kallanga anasema kituo hicho ni miongoni mwa vituo muhimu vinavyolinda miundombinu ya barabara kwa kuhakikisha hakuna gari linalopita na mzigo unaoweza kusababisha uharibifu wa barabara.
Anasema kila siku kituo hicho hupokea magari ya mizigo zaidi ya 400 yanayotoka pande zote mbili za barabara, yakiwemo yanayotoka Mkoa wa Lindi kuelekea Mtwara na yale yanayotoka Mtwara kuelekea Lindi, ambapo yote hupimwa kwa kuzingatia taratibu zilizowekwa.
“Kazi yetu kubwa hapa ni kuhakikisha magari yote ya mizigo yanazingatia uzito unaubalika kisheria. Tunafanya ukaguzi huu ili kulinda uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika ujenzi na matengenezo ya barabara, lakini pia kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara,” anasema Kallanga.
Matengenezo ya mizani
Ili kuhakikisha mizani inaendelea kutoa matokeo sahihi, TANROADS hufanya matengenezo ya kinga katika vituo mbalimbali nchini na hufanyika kwa ratiba maalumu ili kuzuia hitilafu na kuhakikisha vifaa vinaendelea kufanya kazi kwa ufanisi.
Katika baadhi ya vituo vya mizani ikiwemo vile vilivyofanyiwa matengenezo katika mkoa wa Morogoro, wataalamu wamekuwa wakifanya usafi na ukaguzi wa vifaa ili kuondoa changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na mazingira. Msimamizi wa mizani Morogoro Rosemary Nsindagi anasema matengenezo hayo ni muhimu zaidi baada ya msimu wa mvua kwa sababu maji, matope na uchafu mwingine vinaweza kuathiri utendaji wa vifaa vya mizani.
“Baada ya mvua huwa kuna uwezekano wa matope na uchafu kujikusanya katika eneo la mizani, tunafanya usafi na matengenezo ya kinga ili kuhakikisha vifaa vinaendelea kutoa vipimo sahihi,” anasema Rosemary.
Anasema matengenezo hayo hayamaanishi huduma kusimama, bali ni sehemu ya kuhakikisha mfumo mzima wa mizani unakuwa bora zaidi.
Rosemary anasema pale ambapo upande mmoja wa mizani unakuwa katika matengenezo, utaratibu huwekwa kutumia upande mwingine ili magari yaendelee kuhudumiwa. “Huduma haiwezi kusimama kwa sababu tunazingatia mahitaji ya wasafirishaji, tunahakikisha ukaguzi unaendelea huku matengenezo yakifanyika,” anasema.
Mitambo ya ukaguzi wa barabara
Mbali na usimamizi wa mizani, TANROADS imeendelea kutumia teknolojia katika ukaguzi wa hali ya barabara ili kubaini changamoto mapema na kupanga matengenezo kwa wakati.
Meneja wa Usimamizi wa Samani za Barabara kutoka TANROADS, Mhandisi Leonard Mombia anasema matumizi ya teknolojia yameongeza kasi na usahihi katika kutathmini hali ya barabara nchini.
Anasema zamani ukaguzi wa barabara ulikuwa ukifanyika kwa njia za kawaida ambazo zilihitaji muda mrefu, lakini sasa teknolojia imerahisisha kazi hiyo.
“Hapo zamani ukaguzi ulikuwa unachukua muda mrefu kwa sababu ulifanyika kwa njia za kawaida, sasa tunaweza kukagua sehemu kubwa ya barabara kwa muda mfupi na kupata taarifa sahihi zaidi,” anasema Mhandisi Mombia.
Anasema teknolojia hiyo husaidia kupata taarifa kuhusu hali ya lami, mashimo, nyufa, upana wa barabara na maeneo mengine yanayohitaji uangalizi.Taarifa hizo huwasaidia wahandisi kufanya maamuzi sahihi kuhusu matengenezo badala ya kusubiri uharibifu uwe mkubwa.
“Faida kubwa ya teknolojia hii ni kupata taarifa kwa wakati, tunapojua tatizo mapema tunaweza kuchukua hatua mapema na kupunguza gharama za matengenezo,” anasema.
Madereva waona mabadiliko
Baadhi ya madereva wa malori wanaotumia barabara mbalimbali nchini wanasema maboresho yanayofanyika katika vituo vya mizani, ikiwemo matumizi ya teknolojia za kisasa, yanaweza kusaidia kupunguza malalamiko yaliyokuwa yakijitokeza kuhusu utofauti wa vipimo vya uzito wa magari.
Wanasema mfumo wa kisasa wa upimaji ukiwa na usahihi na uwazi zaidi utasaidia kuongeza imani kwa madereva na wasafirishaji, kwa kuwa kila gari litapimwa kwa kuzingatia viwango vinavyofanana bila kuibua mabishano kuhusu matokeo ya uzito.
Dereva wa lori, Hassan Msambali anasema maboresho hayo ni muhimu kwa sababu changamoto ya tofauti za vipimo imekuwa ikiwapa usumbufu baadhi ya wasafirishaji, ikiwemo kuchelewa kwa safari na kuongeza gharama za uendeshaji.
“Teknolojia ikitumika vizuri itasaidia kila mmoja kuona matokeo ya kipimo kwa uwazi, sisi tunachotaka ni mfumo ambao unaaminika na kuhakikisha gari linapimwa kwa haki kulingana na uzito halisi wa mzigo,” anasema Msambali.
Dereva mwingine, Mohamed Ali anasema pamoja na kuboreshwa kwa mifumo ya mizani, ni muhimu kuwepo kwa elimu zaidi kwa wasafirishaji kuhusu viwango vya uzito vinavyoruhusiwa ili kuepuka makosa yanayosababisha usumbufu katika safari zao.
“Barabara zikiharibika na kuwa na mashimo zikifanyiwa ukarabati itatusaidia maana sisi madereva pia tunaathirika kwa sababu magari yanapata gharama kubwa za matengenezo na safari zinakuwa ngumu, ni vizuri kila mtu akafuata sheria,” anasema.
Kulinda barabara ni kulinda uchumi
Kwa ujumla, matumizi ya mizani, teknolojia ya kisasa na ukaguzi wa mara kwa mara wa barabara ni sehemu ya jitihada za kuhakikisha miundombinu ya usafiri nchini inadumu na kutoa huduma kwa muda mrefu.
Kadiri magari yanavyozingatia viwango vya uzito na teknolojia inavyosaidia kubaini changamoto mapema, ndivyo Serikali inavyoweza kupunguza gharama za matengenezo na kuhakikisha barabara zinaendelea kuwa salama kwa wananchi na wafanyabiashara.
Barabara salama siyo tu miundombinu ya usafiri, bali ni kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kulinda barabara ni kulinda shughuli za kila siku za Watanzania na mustakabali wa uchumi wa Taifa.