Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ujumbe kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi

Wadau wenzangu wa Benki ya CRDB,Kwa heshima kubwa na shukrani, ninayo furaha kuungana nanyi

kusherehekea miaka 30 tangu kuanzishwa kwa Benki yetu ya CRDB. Katika kipindi hiki, tunatafakari safari ya mafanikio, changamoto tulizokabiliana nazo na fursa zilizotufikisha hapa tulipo leo kama taasisi imara ya kuaminika na inayoleta chachu ya maendeleo ya kiuchumi nchini Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.

Tulipoanza mwaka 1996, Benki ya CRDB ilikuwa taasisi changa ya fedha iliyojengwa katika msingi wa kuwahudumia Watanzania kwa ufanisi, uwazi na uadilifu. Leo hii, miaka 30 baadaye, tumekuwa moja ya benki kubwa zaidi nchini, tukitoa huduma bunifu kwa sekta zote za uchumi ikiwamo ya kilimo, biashara ndogondogo na za kati, miundombinu, pamoja na wateja binafsi.

Tunapoadhimisha miongo hii mitatu ya kugusa na kubadili maisha ya Watanzania na Taifa kwa ujumla, hatusherehekei tu mafanikio tuliyoyapata, bali maono na misingi iliyoongoza safari yetu tangu mwanzo hadi hapa tulipofika. Safari yetu ni hadithi ya uongozi makini, maono ya kimkakati na imani ya kufanikiwa kujenga taasisi kubwa ya kikanda na kimataifa. Hii siyo hadithi ya mtu mmoja bali ya pamoja, ukomavu wa taasisi na nguvu ya bodi iliyo imara.

Uamuzi wa kuibinafsisha benki hii mwanzoni mwa miaka ya 1990 haukulenga tu kuujenga upya uchumi, bali ilikuwa ni hatua ya mabadiliko yaliyofungua ukurasa mpya katika historia ya sekta ya benki nchini.

Leo hii, tunawashukuru wanahisa waanzilishi ambao imani yao kwa benki hii ndiyo msingi wa kila tulichokijenga. Uwekezaji walioufanya ulionyesha imani kwa biashara ndogo na za kati, ukomavu na uwezo wa Watanzania.

Imani hiyo, pamoja na mwongozo wa Serikali na washirika wa maendeleo, uliiwezesha Benki ya CRDB kufungua ukurasa mpya kutoka kuwa taasisi ya umma hadi kuwa benki imara ya kibiashara inayomilikiwa na watu binafsi. Ukurasa huu ulithibitishwa zaidi mwaka 2009, wakati Benki ya CRDB ilipoorodheshwa kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) ikiwa taasisi ya kwanza ya fedha nchini kufanya hivyo.

Hakika mafanikio yetu katika safari hii ya miongo mitatu, imetufundisha mambo mengi yaliyotusaidia kupiga hatua kubwa ikiwemo kuongeza mtandao wa matawi na mawakala nchi nzima, kutoa huduma katika baadhi ya nchi jirani, kuimarisha mifumo ya kidijitali, kushinda tuzo za kitaifa na kimataifa, kuongeza mchango wetu katika maendeleo ya jamii kupitia miradi ya uwajibikaji na uwekezaji kwa jamii na kuongeza thamani kwa wanahisa wetu na kuendelea kuimarisha ujumuishaji wa wananchi katika huduma za benki.

Maono ya miaka 30 Ijayo Tumepiga hatua kwa ukubwa na hadhi. Kutoka kuwa benki yenye mizania midogo na mtandao mdogo, leo hii Benki ya CRDB ndio taasisi kubwa zaidiya fedha nchini ikwa miongoni mwa zinazoheshimika katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Katika safari hii yote, Bodi ya Wakurugenzi imekuwa ikiongoza kwauthabiti. Majukumu yetu yamekuwa kulinda maono ya taasisi, kuhakikisha uzingatiaji wa sheria na maadili na kuongoza kwa busara katika nyakati zote.

Tumeendelea kuimarisha mifumo ya utawala, kuendeleza mpango mkakati na kukuza utamaduni wa kufikiria mipango ya muda mrefu ujao. Kuanzia kuongoza mabadiliko ya kidijitali nchini hadi kupanua huduma zetu kwenda Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ujumuishi wa kifedha na maendeleo endelevu, sera zetu zimeihakikishia Benki ya CRDB kuendelea kuwa mbele ya mwelekeo wa sekta, huku tukiendeleza misingi tuliyoianzisha.

Maono ya Bodi sio tu kuangalia miaka 30 ijayo kama mwendelezo wa yale tuliyoyafikia, ila kama lango la fursa mpya. Tunaiona Benki ya CRDB ikiwa taasisi ya fedha yenye nguvu kikanda na kimataifa. Ni benki ya kisasa, inayoongozwa kwa takwimu na ubunifu wa hali ya juu. Tunaiona benki inayotumia teknolojia kama akili mnemba, ‘blockchain’ na majukwaa ya kidijitali kuhudumia wateja wake barani Afrika na duniani kote. Benki ambayo ahadi zake katika nyanja za mazingira, uwajibikaji kwa jamii, na uongozi ni jukumu muhimu na moyo wa muundo wa biashara zake.

Katika miaka 30 ijayo, tunalenga kukuza mizania yetu ifike kati ya Shilingi trilioni 60 hadi shilingi trilioni 70, kutoa huduma katika angalau nchi 8 duniani, kutambulika miongoni mwa benki 10 bora barani Afrika kwa ubunifu na uaminifu wa wateja na kuendeleza uongozi wetu katika usimamizi, utawala bora, na miradi endelevu.

Neno la shukrani Kwa niaba ya Bodi, tunatoa shukrani za dhati kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Jamhuri ya Burundi, na Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa kuendelea kutuunga mkono na kwa kuweka mazingira rafiki kwa ajili ya ukuaji wa sekta ya fedha.

Tunawashukuru wanahisa wetu wote, waasisi na viongozi wapya kwa imani yenu ya miongo mingi. Tunawashukuru wasimamizi wa sekta, washirika wa maendeleo, wateja wetu, na wadau wote ambao ushirikiano wao umesaidia kuifanya safari hii kuwa ya mafanikio. Pia, nawapongeza na kuwashukuru wafanyakazi wote wa Benki ya CRDB, waliotufanya kuwa taasisi bora na madhubuti ndani ya miaka 30 tu.

Uwajibikaji wenu umetuwezesha kufika hapa na kwa pamoja tuna Imani miaka ijayo itakuwa ya mafanikio makubwa zaidi. Urithi wa Benki ya CRDB haupimwi kwa ukubwa wake, ila kwa maadili yake. Ni urithi wa Watanzania, Warundi, Wacongo na Waafrika wote wanaoamini katika uwezo wao. Na huu ni mwanzo tu wa hadithi hiyo.

Prof. Neema Munisi Mori, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB.