13 wapenya ubunge Kongwa, Hersi akwama
Muktasari:
- Inakuwa mara ya pili jina la Hersi kukatwa katika mbio za kutafuta ubunge baada ya awali kuenguliwa Jimbo la Kigamboni jijini Dar es Salaam
Dodoma. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimefanya mchujo wa watiania 24 waliochukua fomu kwa mara ya pili kuomba ridhaa ya chama kuteuliwa kugombea ubunge wa Jimbo la Kongwa.
Kwa mujibu wa taarifa kwenye tovuti ya CCM Wilaya ya Kongwa, watiania 13 wamepitishwa kwenda kupigiwa kura na wajumbe kwa ajili ya kumpata mgombea ubunge katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025.
Miongoni mwa majina yaliyokatwa yumo Rais wa Yanga, Hersi Said ambaye awali aliomba kuteuliwa kugombea ubunge wa Jimbo la Kigamboni mkoani Dar es Salaam, lakini jina lake lilienguliwa na vikao vya CCM.
Mchakato wa kupata mgombea wa CCM Jimbo la Kongwa umerejewa upya kufuatia kifo cha Job Ndugai, Spika mstaafu na mbunge aliyemaliza muda wake jimboni humo, ambaye alikuwa ameongoza kwenye kura za maoni.
Ndugai alifariki dunia Agosti 6, 2025 na baada ya mazishi yake Agosti 10, 2025, CCM ikatangaza mchakato wa kumtafuta mgombea kuanza upya ambapo watu 24 walijitokeza.
Katika orodha ya sasa ya majina 13, majina ya wagombea saba yalikuwepo awali, kabla ya kurejea upya mchakato huo.
Kati ya watiania 10 wa awali walioshindana na Ndugai, saba pekee wamerejeshwa ambao ni Isaya Mungurumi, Dk Samora Mshang'aa, Dk Simon Ngatunga, Elias Mdao, Philipo Chiwanga, Profesa Emmanuel Mbenah na Ngaya Mazanda.
Wawili yaliopenya kwenye mchujo wa awali ambara safari hii hawakurudi, ni Mwalimu Deus Seif aliyeshika nafasi ya tatu na Paschal Mahinyila aliyekuwa nafasi ya nane.
Wengine ambao hawakuwepo kwenye orodha ya awali, na wamepenya ni Fadhili Bwagakilo, Rodi Gairigi, Baraka Mkanwa, Michael Chigada, Henry Msunga na Dk Rose Mbijima.
Waliopenya kwenye mchujo wa sasa kwa mujibu wa ukurasa rasmi wa CCM, Kongwa ni Dk Rose Mbijima, Isaya Mungurumi, Henry Msunga, Elias Mdao, Dk Samora Mshang'aa, Profesa Emmanuel Mbenah na Philip Chiwanga.
Wengine ni Ngaya Mazanda, Michael Chidaga, Dk Simon Ngatunga, Baraka Mkanwa, Rodi Gairigi na Fadhili Bwagakilo.
Kwa mujibu wa Katibu wa Wilaya, leo Ijumaa na kesho Jumamosi wawaombaji hao wanajinadi kwa pamoja kwenye mikutano ya kata 22 za jimbo hilo na kura za maoni zitapigwa siku ya Jumapili ya Agosti 17, 2025.
Amesema mchakato wa kumpata mgombea katika Jimbo la Kongwa unapaswa kwenda kwa haraka ili kuendana na kalenda ya INEC kwa kuwa mwisho wa uteuzi wa wagombea ni Agosti 27, 2025.