Wagombea 24 Kongwa watakaopenya kuanza kujinadi kwa wajumbe leo
Muktasari:
- Watiania waliojitokeza awali wanatupa karata yao kwa mara nyingine ili kuwashawishi wajumbe kwa ajili kuwachagua siku ya Jumapili.
Dodoma. Jina la nani litarudi kati ya majina 24 ya watiania ya kuomba kuwania ubunge katika Jimbo la Kongwa imebaki kitendawili baada ya kifo cha aliyeongoza kura za maoni Job Ndugai kilichotokea Agosti 6, 2025.
Chama cha Mapinduzi (CCM) kilitangaza kurudia mchakato wa uchaguzi kura za maoni ambapo uchaguzi wa ndani kura ya maoni utafanyika Agosti 17, 2025 siku ya Jumapili.
Je waliopendekezwa awali watarudi? Waliokuwa wamekatwa nao watarudi? Sababu za wao kukatwa na kurudishwa zimebadilika?
Hayo ni maswali magumu lakini mepesi kwa asubuhi ya leo Ijumaa Agosti 15, 2025 ambapo watu 24 waliochukua fomu kumrithi Ndugai wanasubiri majibu ili waanze kampeni.
Katibu wa CCM Wilaya ya Kongwa, Joyce Mkaugala amesema kuwa anasubiri majina ya waliopendekezwa ili waanze kampeni kwa kuwatembeza kwenye mikutano ya kata leo.
"Mikutano ipo leo kama kawaida na tunasubiria majina asubuhi hii ili watu walioteuliwa waje kujinadi," amesema Joyce.
Kati ya watu 24 walioomba nafasi hiyo, tisa kati yao walipita kwenye mchujo wa awali na wakagombea ingawa kura zao zilikuwa nyuma ya marehemu Ndugai aliyeongoza kwenye matokeo ya jumla.
Mbali na hao, wapo ambao majina yao hayakupenya katika vikao vya uteuzi wa awali akiwemo Hersi Said ambaye ni Rais wa Klabu ya Yanga, awali alikuwa ameomba Jimbo la Kigamboni na sasa ameibukia Kongwa akijaziwa fomu.