Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

AAFP: Tutatengeneza vinu vya nyuklia

Muktasari:

  • Kwa sasa duniani, nchi kumi bora zenye vinu vya nyuklia imo Marekani yenye vinu 94 vinazalisha umeme 781,945 Gwh sawa na asilimia 18.2 ya nishati yote inayozalishwa kwa ajili ya Marekani

Moshi. Inawezekana ni moja ya ahadi itakayohitaji utaalamu na gharama kubwa kuitekeleza lakini Chama cha Alliance for Africa Farmers Party (AAFP), kimeahidi kutengeneza vinu vya nyuklia endapo kitapewa ridhaa ya kuongoza nchi.

Kwa sasa duniani, nchi kumi bora zenye vinu vya nyuklia ni pamoja na Marekani yenye vinu 94 vinazalisha umeme 781,945 Gwh sawa na asilimia 18.2 ya nishati yote inayozalishwa kwa ajili ya  Marekani.

Nchi nyingine zenye vinu vya nyuklia inavyovitumia kuzalisha umeme ni Ufaransa ina vinu 57 China vinu 57, Urusi yenye vinu 37, Japan vinu 33, Korea Kusini, Canada yenye vinu 19 India yenye vinu 20 na Uingereza yenye vinu 9.

Kwa nchi za Afrika ni Afrika Kusini na Misri ndio zinatajwa kuwa na vinu vya nyuklia huku Ghana, Kenya, Uganda, Morocco, Nigeria, Algeria na Rwanda zikiwa katika mipango ya awali ya kutengeneza vinu vya nyuklia.

Nchi zenye silaha za nyuklia ni  Russia, Marekani, China, Ufaransa, Uingereza, India, Pakistan, Israel na Korea Kaskazini huku Iran, Kazakhstan na Syria zina maeneo yenye vinu vya siri vya kuzalisha silaha hizo.

Hata hivyo, mchambuzi huru wa siasa safi, uongozi na usalama, Sam Temu anatahadharisha juu ya ahadi hiyo akisema Tanzania bado haina uwezo wa ndani kisayansi, kiteknolojia na kifedha kuweza kujenga kinu cha nuklia kwa sasa.


Ahadi ya vinu vya nyuklia

Katika ilani yake ya miaka mitano (2025/30) kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani utakaofanyika Oktoba 29,2025, AAFP imekuja na ahadi ya kuiagiza Serikali itakayoundwa na chama chake, kutengeneza vinu vya nyuklia.

“Kwa kuwa nchi nyingi za majirani na duniani kote kumekuwa na migogoro au vurugu za kidiplomasia, hivyo ilani ya chama chetu cha AAFP inaitaka Serikali yake kutengeneza vinu vya nyuklia na kutengeneza ndege zisizo na marubani.”

Mbali na ahadi hiyo lakini imeahidi kuzungusha ukuta katika mipaka nchi nzima.


Itakavyoligawa JWTZ

Katika ilani yake hiyo, AAFP imeahidi kulifanyia mabadiliko makubwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na litagawanywa katika makundi makubwa mawili.

Kutakuwa na Jeshi la Ulinzi na vita, ambalo kazi zake kubwa itakuwa ni ulinzi wa mipaka ya nchi na mambo ya vita na kwamba wataalamu wote wa mambo ya kivita na ulinzi wa mipaka watajiunga na jeshi namba moja.

Kundi la pili ni jeshi la maendeleo Tanzania na sera ya AAFP inakusudia Serikali kuweka utaratibu wa kisheri kwamba, kazi na miradi yote ya maendeleo ndani ya nchi kama vile ujenzi wa barabara na majengo utasimamiwa na jeshi hili.

“Miradi yote kama hiyo ikiwamo utengenezaji wa madawati inatekelezwa, kufanywa na kusimamiwa na Jeshi maalum la maendeleo,” inasema ilani hiyo.

“Wataalamu wote wa jeshi kwa viwango tofauti watajiunga katika jeshi la maendeleo ili kuhakikisha tunakomesha wizi uliozoeleka katika kutekeleza miradi ya maendeleo,”inasisitiza AAFP katika ilani yao hiyo.

“Vile vile ilani inakusudia kuweka nidhamu katika shughuli za maendeleo na kuongeza ajira kwa vijana. Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) linafutwa na kuchanganywa katika jeshi la maendeleo Tanzania ambalo litaitwa jeshi namba mbili.”

Kwa upande wa idara ya usalama wa Taifa, Jeshi la Polisi, Magereza, Zimamoto, Uhamiaji na idara zingine kama hizo, AAFP inasema katika ilani yake hiyo ya 2025/30 zitabaki zilivyo na au zitafanyiwa mabadiliko pale itakapohitajika.


Mtaalamu afunguka mazito

Akizungumza na gazeti hili, mchambuzi wa siasa na masuala ya usalama, Sam Temu anasema Tanzania bado haina uwezo wa ndani wa kisayansi, kiteknolojia na kifedha wa kujenga kinu cha nyuklia kwa sasa.

“Vinu vya nyuklia vinahitaji utaalamu wa hali ya juu kwa maana ya wanasayansi wa nyuklia, wahandisi wa nyuklia, mifumo ya usalama, miundombinu ya gharama kubwa, na usimamizi IAEA (Shirika la Kimataifa la Nguvu za Atomiki),”anasema.

“Kuhusu madini ya nyuklia, ndiyo, Tanzania ina uranium katika maeneo ya Mkuju River (Namtumbo – Ruvuma), Manyoni (Singida) na Bahi (Dodoma),” anaeleza.

Anasema miradi ya uchimbaji ilishawahi kufanyiwa utafiti na Kampuni ya Mantra Resources kwa kushirikiana na Serikali, lakini hadi sasa hakuna mgodi unaozalisha kibiashara uchimbaji wa urani.

“Hata tukizalisha uranium, bado mchakato wa kubadilisha madini ghafi (yellowcake) hadi fuel rods za nyuklia unahitaji teknolojia ya juu mno ambayo ipo tu kwenye nchi chache kama Marekani, Russia, Ufaransa, China na zingine.”

“Kwa hiyo tuna malighafi (uranium) lakini hatuna teknolojia wala miundombinu ya kuibadilisha kuwa nishati ya nyuklia kwa sasa,”anasisitiza mchambuzi huyo.

Kuhusu drones, anasema hilo lina uwezekano mkubwa zaidi hasa katika uzalishaji wa drones kwa ajili ya ulinzi, ufuatiliaji, kilimo au miradi ya maendeleo unaweza kufikiwa kwa haraka kuliko nyuklia.

“Tanzania ina wahandisi wa umeme na ICT na tukipata uwekezaji na mafunzo, tunaweza kuanzisha viwanda vidogo vya kuunganisha na kutengeneza drones. mataifa madogo mengi kama Ethiopia, Rwanda, Afrika Kusini tayari yana program za drones. kwa hiyo hili siyo jambo lisilowezekana,”anasema mtaalamu huyo.


Kuligawa JTWZ

Kuhusu ahadi ya kuligawa JWTZ kuwa majeshi mawili, anasema ni wazo zuri kuwa na Jeshi la Ulinzi wa mipaka kwa ajili ya kulinda mipaka dhidi ya uhalifu wa kimataifa, uhamiaji haramu, ugaidi na hata chokochoko zitakazojitokeza.

“Jeshi la Maendeleo na Mafunzo ya Uzalendo linaweza kufanana na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), likipewa jukumu zaidi la kushiriki moja kwa moja kwenye miradi mikubwa ya kitaifa kama umeme, barabara, kilimo cha umma, viwanda.”  anasema.

Hata hivyo, mtaalamu huyo anasema  changamoto ni kwamba, kuigawanya JWTZ katika majeshi mawili rasmi kunaweza kuhitaji mabadiliko ya Kikatiba na kisheria, kwa kuwa JWTZ kwa sasa ni jeshi moja lenye vitengo mbalimbali.

“Kwa kuhitimisha niseme kuwa hili la vinu vya  nyuklia ni kweli tuna uranium lakini hatuna uwezo wa teknolojia, hivyo ni ahadi ya muda mrefu sana inaweza kuwa ya kisiasa zaidi kuliko kiutekelezaji,” anatahadharisha mtaalamu huyo.

Kuhusu drones, anasema hilo linawezekana kwa muda mfupi na wa kati, na linaweza kuchochea ajira, teknolojia na usalama.

Kuhusu Jeshi la Ulinzi na la maendeleo, anasema linaweza kuundwa kwa kuongeza nguvu kwenye JKT na JWTZ bila kuvunja misingi ya sasa.

“Kwa hivyo ahadi hii ina vipengele vya ndoto za muda mrefu (nyuklia) na vipengele vya uhalisia vinavyoweza kuanza kutekelezeka drones na jeshi la maendeleo,” anasema huku akitahadharisha kuwa, hilo litahitaji mabadiliko madogo ya Katiba ya Tanzania.