Absa yatoa Sh20 milioni kusaidia watoto wenye magonjwa ya moyo
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Obedi Laiser (wa pili kushoto), na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Peter Kisenge, wakibadilishana Hati ya Makubaliano (MoU) katika hafla iliyofanyika katika JKCI, Dar es Salaam jana. Kushoto ni Katibu wa Kampuni wa Benki ya Absa Tanzania, Desmond Malyi, na kulia ni Meneja Mkuu wa Global Medicare, Daniel Lazaro.
Dar es Salaam. Benki ya Absa Tanzania imetoa Sh20 milioni kwa ajili ya kusaidia matibabu ya watoto wanaoishi na magonjwa ya moyo, hatua inayolenga kuongeza fursa ya watoto kutoka familia zenye uhitaji kupata huduma za matibabu zinazookoa maisha.
Msaada huo umetolewa kupitia Heart Team Africa Foundation (HTAF), taasisi isiyo ya kiserikali iliyoanzishwa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), inayosaidia watoto wanaohitaji matibabu ya moyo nchini.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Absa Tanzania, Obedi Laiser, alisema msaada huo unaonyesha dhamira ya benki hiyo ya kuchangia maendeleo ya jamii kupitia sekta ya afya.
Alisema watoto wote wanapaswa kupata nafasi ya kuishi maisha yenye afya, hivyo benki imeamua kushirikiana na JKCI ili kusaidia kuongeza upatikanaji wa matibabu kwa watoto wanaokabiliwa na magonjwa ya moyo.
"Dhamira yetu ni kuwa chachu ya maendeleo mema katika kila tunachofanya. Kupitia ushirikiano huu tunaongeza fursa kwa watoto wanaoishi na magonjwa ya moyo kupata matibabu yanayookoa maisha na kuzipa matumaini familia zinazokabiliwa na changamoto za kiafya na kifedha," alisema Laiser.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge, alisema mchango huo umekuja wakati ambao watoto wengi wanahitaji huduma maalumu za matibabu ya moyo.
Alisema magonjwa ya moyo yanaendelea kuongezeka duniani na Tanzania, huku zaidi ya asilimia 70 ya watoto wenye matatizo hayo wakizaliwa nayo, wakati wengine huyapata baada ya kuzaliwa.
"Msaada huu utatusaidia kuongeza upatikanaji wa huduma za matibabu ya moyo kwa watoto wenye uhitaji. Pia unaonyesha umuhimu wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na taasisi za afya katika kuboresha huduma za matibabu nchini," alisema Dk Kisenge.
Aliishukuru Benki ya Absa kwa mchango huo na kueleza kuwa unakwenda sambamba na juhudi za Serikali za kuboresha huduma za afya na kupunguza mzigo wa gharama za matibabu kwa wananchi.
Baadhi ya wazazi wa watoto wanaonufaika na huduma hizo, akiwemo Mariam Athumani ambaye mtoto wake Lightness tayari amefanyiwa upasuaji wa moyo, pamoja na Adam Nuhu ambaye mtoto wake Ajmalbey anasubiri kufanyiwa upasuaji, waliishukuru benki hiyo kwa msaada huo huku wakizitaka taasisi nyingine kujitokeza kusaidia watoto wenye changamoto kama hizo.
Absa Tanzania imesema mchango huo ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wake wa uwajibikaji kwa jamii unaolenga kuboresha upatikanaji wa huduma za afya, kupunguza mzigo wa kifedha kwa familia zenye watoto wanaohitaji matibabu ya moyo na kuchangia ujenzi wa jamii yenye afya bora nchini.