Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ACT Wazalendo na muundo wa Serikali tatu

Muktasari:

  • Hoja ya muundo wa muungano wa Serikali tatu ulijitokeza kwa nguvu wakati wa ukusanyaji wa maoni ya Katiba mpya uliofanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uenyekiti wa Jaji Joseph Warioba na kuliingiza katika Rasimu ya Katiba.

Moshi. Chama cha ACT Wazalendo kimeahidi kuimarisha Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa mwaka 1964 kwa misingi ya usawa na heshima ya pande zote, na ili kutekeleza hayo, Muungano utakuwa ni wa Serikali tatu.

Wadau waliozungumzia ahadi hiyo wametofautiana kimtazamo, huku baadhi wakisema hoja hiyo inaakisi maoni ya Watanzania waliyoyatoa katika mchakato wa Katiba mpya inayopendekezwa, na wengine wakidai itaongeza gharama za kuendesha Serikali.

Wakili Stephen Mduma anasema, ili kutekeleza ahadi hiyo, itawalazimu kwanza kubadili sheria mama, ambayo ni Katiba, huku Askofu mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Stephen Munga, akisema lengo ni kuvutia kura.

Hoja ya muundo wa muungano wa Serikali tatu ulijitokeza kwa nguvu wakati wa ukusanyaji wa maoni ya Katiba mpya uliofanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uenyekiti wa Jaji Joseph Warioba, na kuliingiza katika Rasimu ya Katiba.

Chini ya rasimu hiyo, ambayo hata hivyo suala la Serikali tatu lilifumuliwa na wajumbe wengi katika Bunge Maalum la Katiba, ilipendekeza uwepo wa Serikali ya Shirikisho, Serikali ya Tanganyika na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Wananchi wengi waliotoa maoni kuhusu Muungano walijikita kwenye muundo wake. Kwa Tanzania Bara, wananchi zaidi ya 39,000 walitoa maoni kuhusu Muungano, na kati ya hao, karibu wananchi 27,000 walizungumzia muundo.

Ripoti ya Jaji Warioba ilieleza, kwa Zanzibar, wananchi karibu wote waliotoa maoni walijikita kwenye suala la Muungano. Kati ya wananchi karibu 38,000, wananchi 19,000 walitoa maoni kuhusu muundo wa Muungano.

Mchanganuo wa takwimu hizi unaonesha, wananchi waliotoa maoni kuhusu muundo wa Muungano kwa upande wa Tanzania Bara, asilimia 13 walipendelea Serikali moja, asilimia 24 walitaka Serikali mbili na asilimia 61 Serikali tatu.

Kwa upande wa Zanzibar, asilimia 34 walipendekeza Serikali mbili, asilimia 60 walipendekeza Muungano wa Mkataba, na asilimia 0.1 sawa na watu 25 walipendekeza Serikali moja. Taasisi nyingi zilipendekeza Serikali tatu.

ACT Wazalendo, kupitia ilani yake ya uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani ya 2025–2030, imeahidi kuimarisha Muungano kwa misingi ya usawa na heshima ya pande zote mbili kupitia mfumo wa Serikali tatu.

Kinasema kitafufua mchakato wa kuandaa Katiba mpya ya Muungano inayoendana na mahitaji ya wakati, chini ya msingi wa haki, heshima na usawa kama nchi mbili huru zilizoungana kwa hiari, ili kuwa na Muungano wa haki.

Katika kipindi hicho cha miaka mitano, kimeahidi kuanzisha Akaunti ya Pamoja ya Fedha za Muungano kama ilivyoelekezwa na Ibara ya 133 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kulipa malimbikizo ya madeni ya Zanzibar.

Halikadhalika, kitahakikisha Zanzibar inanufaika na mamlaka yake kwa mambo yasiyo ya Muungano, ndani na nje ya nchi.

Mbali na hilo, kama kitapata ridhaa ya kushika dola, ACT Wazalendo kimeahidi kujenga diplomasia ya kimshikamano wa kisiasa, kijamii na kiuchumi kwa watu wa Afrika; kitasimama na kushikamana kupinga uonevu na ukandamizaji duniani kote.


Wadau na muundo wa Serikali tatu

Askofu Munga anasema: “Nadhani ACT Wazalendo wameweka ahadi hiyo katika ilani yao wakiakisi maoni ya raia wengi waliyoyatoa wakati wa mchakato wa Katiba mpya chini ya Tume ya Jaji Warioba (Joseph — mwenyekiti wa Tume).”


“Lengo lao ni kuvuta wale wenye mtazamo huo. Ilani ni mkakati wa kisiasa wa kuvuta wapigakura kuwachagua. Kwenye uchaguzi, ilani ni kama chambo kwenye ndoano ambapo kila anayevutiwa nacho hukimiza,” amesema Askofu Munga.

Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Ruaha (RUCU), Dk Rwezaura Kaijage, anasema muundo wa Serikali tatu hauna ubaya, bali kinachowasumbua Watanzania ni tafsiri ya Serikali tatu, akisisitiza ni mzuri.

Kwa upande wake, Wakili Mduma anasema, ili kutekeleza ahadi hiyo, itawataka kubadili sheria mama ya nchi yetu, ambayo ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kama ilivyofanyiwa marejeo mara kwa mara

“Lakini itawalazimu kuwashawishi wananchi kukubaliana na mabadiliko hayo, sababu sio mfumo rahisi, kwani kwa kiasi fulani utaongeza gharama za uendeshaji wa Serikali, kwani kuna nafasi za viongozi nyingi mpya zitaibuka,” anasema.

Wakili Peter Mshikilwa anasema, ahadi hiyo ni wazo ambalo limekuwepo kwa muda mrefu. Hata katika tume zilizopita za Jaji Kisanga na Nyalali, suala hilo liliongelewa, na kwamba muundo huo ndio mwarobaini wa kero za Muungano.

Mkazi wa Moshi na Dar es Salaam, Aman Ngowi, anasema: “Ningetamani kama ACT Wazalendo wangeanza na mabadiliko ya Katiba, maana huo ndio msingi wa yote. Unaanzishaje muundo wa Serikali tatu wakati zipo kikatiba?”


Huduma bora

Kupitia ilani yake hiyo, pia kimeahidi kuja na mkakati madhubuti wa kutoa huduma bora za afya, elimu, maji, nishati na hifadhi ya jamii, na kitahakikisha upatikanaji wa bima ya afya kwa wote kupitia mfumo wa hifadhi ya jamii.

Pia kitatoa elimu bure hadi chuo kikuu isiyokuwa na michango ya aina yoyote, na kimeahidi pia kusimamia usambazaji na upatikanaji wa maji na umeme kwenye kila kaya, upatikanaji na unafuu wa gesi ya kupikia na hifadhi ya jamii kwa wote.

Akizungumzia ahadi hiyo ya ACT Wazalendo, Anna Emmanuel, ambaye ni mwanafunzi wa stashahada ya ualimu wa shule ya awali (chekechea), anasema ahadi hizo zinavutia na zinatia matumaini kama chama kitapata ridhaa hiyo.

“Hili la elimu bure hadi chuo kikuu nimelipenda kwa sababu Serikali inasema sasa hivi inatoa elimu bure hadi sekondari, lakini kiuhalisia sio kweli. Wanacholipa ni ada tu kwa shule za umma. Kuna michango kibao shuleni,” anasema.

Kwa upande wake, Magdalena Johnson, ambaye ni mjasiriamali muuzaji bidhaa za mitumba, anasema amefurahishwa na ahadi ya kutoa bima ya afya kwa wote, akisema itapunguza mzigo wa matibabu kutokana na gharama hizo kuwa juu

Akizungumza kutoka Marekani, Hussein Mfinanga, mtaalamu wa Teknolojia ya Mawasiliano ya Habari (ICT), anasema elimu bure isiishie shule za umma pekee, bali waangalie watakavyotoa ruzuku katika shule binafsi.


Miundombinu bora

Chama hicho, kupitia ilani yake, pia kimeahidi kuwekeza kwenye miundombinu ya kisasa kwa lengo la kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

“Tutatekeleza ujenzi wa reli mpya ya Kusini (SGR), kufufua reli za kanda, kujenga barabara za kimkakati kama Cashew Ring Road, kununua vivuko, na kuimarisha bandari zote muhimu ikiwemo Mtwara, Tanga, Bagamoyo na Kigoma.

“Tutasambaza miundombinu ya nishati, maji, mawasiliano na huduma za usafirishaji hadi ngazi ya vijiji kwa ajili ya ustawi wa watu wote,” inaeleza sehemu ya ilani hiyo

Kulinda na kusimamia rasilimali za Taifa

ACT inaeeza kuwa endapo kitashika dola, kitahakikisha rasilimali na utajiri wa Taifa unawanufaisha Watanzania wote.

“Kupitia ilani hii, tutarejesha ardhi zote za wananchi zilizoporwa na kuhakikisha usimamizi wa rasilimali unakuwa chini ya mamlaka kamili ya wananchi, kwa kuanzisha mifumo ya kitaifa ya umiliki na ushiriki wa wananchi kwenye rasilimali.”

Inataja rasilimali hizo kuwa ni za sekta ya madini, gesi, misitu na ardhi, na kwamba ACT Wazalendo itarejea na kuweka wazi mikataba yote inayohusisha rasilimali za nchi, kilio ambacho ni cha muda mrefu cha Watanzania na wabunge.


Mazingira, tabianchi na nishati mbadala

Kuhusu mazingira, tabianchi na nishati mbadala, ACT Wazalendo kimeahidi kujenga uchumi utakaokuza matumizi ya nishati jadidifu, kuboresha mifumo ya uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

“Tutaongeza uzalishaji wa umeme hadi megawati 9,365 kufikia mwaka 2030 kwa vyanzo vya maji, gesi na jua, huku tukipunguza bei ya umeme kwa asilimia 50,” kinaeleza chama hicho kupitia muhtasari wa ilani yake ya uchaguzi 2025–2030.