ACT Wazalendo: Tumesimamisha watiania majimbo 272
Muktasari:
- Kwa mujibu wa ratiba ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kesho Agosti 28,2025 ndio uzinduzi wa kampeni za udiwani, ubunge na urais zitakazoihitimishwa Oktoba 28,2025, kisha siku inayofuata ni kupiga kura.
Dar es Salaam. Wakati leo Jumatano Agosti 27,2025 ndio mwisho wa mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu za udiwani na ubunge, Chama cha ACT Wazalendo, kimesema kimesimamisha watiania katika majimbo yote 272.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano, Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mawasiliano wa ACT Wazalendo, Shangwe Ayo amesema kila jimbo la Tanzania bara na Zanzibar wamesimamisha watiania waliochukua fomu na kuzirejesha INEC kwa nyakati tofauti.
“Sasa hivi naendelea kukusanya taarifa za urejeshaji wa fomu na uteuzi kujua wangapi wameshateuliwa na INEC katika majimbo mbalimbali,” amesema Ayo.
Wakati Ayo akieleza Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo (Bara), Isihaka Mchinjita ameiambia Mwananchi kuwa maeneo yote watiania wa chama hicho waliochukua fomu na kuzirejesha wameteuliwa kuanzia udiwani na ubunge.
“Maeneo yote fomu zilizopochukuliwa na kurejeshwa INEC wagombea wetu wameteuliwa wa taarifa nilizonazo, sijapata malalamiko yoyote ya mgombea kutoketeuliwa baada ya kurejesha fomu zake,”
“Hadi sasa hatujapokea kesi ambazo zinamhusu mgombea wa act Wazalendo, kutoteuliwa na INEC, sijui labda baadaye maana tunaendelea kupokea taarifa za mwenendo huu,”amesema Mchinjita ambaye anawania Jimbo la Lindi Mjini.