Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ADC yajifungia kujadili kutenguliwa mgombea urais

Dar es Salaam. Uongozi wa Chama cha Alliance Democratic for Change (ADC) umejifungia kwenye kikao cha dharura kujadili barua kutoka Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ya kutenguliwa kwa uteuzi wa mgombea wao wa urais wa Tanzania, Wilson Elias.

Uamuzi huo wa Msajili umetolewa jana Jumanne, Agosti 26, 2025, ambapo pamoja na Elias, pia alitenguliwa Luhaga Mpina wa chama cha ACT-Wazalendo, kwa tuhuma za ukiukwaji wa sheria na kanuni katika mchakato wa uteuzi ndani ya vyama vyao.

Katika mazungumzo na Mwananchi, leo Jumatano, Agosti 27, 2025, Katibu Mkuu wa ADC, Mwalimu Aziz, amethibitisha kupokea barua hiyo rasmi kutoka kwa Msajili na kueleza chama kipo kwenye kikao maalumu cha ndani kabla ya kutoa msimamo kwa umma.

“Ni kweli tumepokea barua kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuhusu kutenguliwa kwa mgombea wetu wa urais. Kwa sasa tunaendelea na kikao cha dharura cha viongozi ili kujadili barua hiyo,” amesema Mwalimu.

Chama hicho kimepokea uamuzi huo katika kipindi ambacho mgombea wao, Wilson Elias, alikuwa tayari ameshatembelea zaidi ya mikoa 10 ikiwemo miwili kutoka Zanzibar kukusanya wadhamini zaidi ya 200 kwa kila mkoa, kama inavyotakiwa na sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).

Uteuzi wa Elias ulifanyika Julai 29, 2025, katika ukumbi wa mikutano wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam, ambapo alipitishwa kwa kishindo na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa chama hicho akiwa mgombea pekee.

Hata hivyo, mchakato huo ulilalamikiwa na aliyekuwa anatarajiwa kuwa mpinzani wake, Mutamwenga Mgaywa, ambaye aliondolewa awali kwa madai ya kutojaza fomu kwa usahihi.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya Msajili, iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano na Elimu ya Uraia, Abuu Kimario, wagombea waliotenguliwa walikiuka masharti ya Kifungu cha 4(5)(a) na (b) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, Sura ya 258.

Kimario alieleza kuwa mchakato wa uteuzi ndani ya vyama hivyo haukufuata misingi ya sheria, katiba na kanuni za vyama husika, jambo linalotishia utawala wa sheria na mshikamano wa kitaifa.


Malalamiko ya Mgaywa yaivuruga ADC

Madai ya Mutamwenga Mgaywa, aliyewahi kuwa Mbunge wa Mwibara kwa miaka 10, ndio yanaelezwa kuchochea uamuzi wa Msajili.

Mgaywa alilalamikia kile alichokiita hujuma dhidi yake, akidai taarifa zake ziliondolewa makusudi kwenye fomu na kuwekwa nyingine zisizo sahihi ili kumwondoa kwenye mchakato wa kugombea.

Siku ya uchaguzi ndani ya chama, Mgaywa aliondolewa kwenye ukumbi wa mkutano kwa madai ya kutokuwa mjumbe halali, licha ya kuwa alikuwa mtiania wa nafasi ya urais.

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa chama hicho, Mtoro Mvunye, alieleza kuwa Mgaywa aliondolewa kwa kushindwa kujaza sehemu muhimu za fomu ikiwemo picha na wadhamini 100, hivyo kumpitisha mgombea mmoja pekee, Elias.

Mwenyekiti wa chama hicho, Shabani Itutu, alitetea hatua hiyo akisema chama hakiwezi kuruhusu mtu asiyejaza fomu ipasavyo kugombea nafasi nyeti kama ya urais.

“Huyu mgombea tukimpitisha anaweza kutupeleka pabaya. Hatuwezi kumruhusu mtu ambaye hajajaza fomu vizuri kugombea nafasi ya juu kama hiyo,” alisema Itutu.

Kwa mujibu wa Kifungu cha 6A(2) cha Sheria ya Vyama vya Siasa, vyama vinapaswa kuendeshwa kwa mujibu wa Katiba ya nchi na kanuni zao wenyewe, na Msajili amesisitiza kuwa uteuzi wa wagombea lazima uwe halali na wa kidemokrasia ili kulinda misingi ya kitaifa.

Ofisi ya Msajili imekabidhi barua rasmi za uamuzi huo kwa vyama husika, pamoja na maelezo ya mchakato wa kushughulikia malalamiko yaliyowasilishwa.