ADC waahidi umeme na maji bure ndani ya siku 90
Muktasari:
- Hata hivyo amejitetea kuwa ufinyu wa barabara umesababisha achelewe kiasi hicho hivyo akiapishwa kwenye nafasi hiyo atafumua Sheria za masuala ya Miundombinu.
Dodoma. Hatimaye mtiania wa nafasi ya urais wa chama cha ADC, Wilson Mulumbe, amechukua fomu.
Mulumbe amechukua fomu hiyo leo, Alhamisi, Agosti 14, 2025, baada ya kutoonekana juzi, Jumanne. Hata leo alitarajia kufika ofisi za INEC saa tatu asubuhi, lakini alifika saa 9:10 alasiri.
Hata hivyo, amejitetea kuwa ufinyu wa barabara umesababisha achelewe kiasi hicho, hivyo akiapishwa kwenye nafasi hiyo, atafumua sheria zinazoongoza ujenzi wa miundombinu.
Msafara wa mtinia huyo ulikuja na pikipiki, ngoma ya mdundiko, na gari lililofungwa spika kubwa, akiwa na mshereheshaji.
Kundi la vijana waliosindikiza msafara huo walikuwa ni sura zilezile ambazo zimeonekana kwa wagombea wengine waliotangulia.
Walipofika ofisi za INEC, walipokelewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi, Ramadhan Kailima, na kuingia ndani ya jengo ambako walitumia muda mfupi kabla ya kutoka nje na kuzungumza na waandishi wa habari huku akijinadi kwa kusema; "Tunaamini CCM wanakwenda kutukabidhi nchi baada ya upigaji kura Oktoba 29."
Amesema ADC imewasha moto ambao hauna mtu wa kuuzima na kutaja mambo matano yatakayowezesha chama hicho kuingia madarakani.
Mambo hayo amesema ni pamoja na kutoa elimu bure hadi chuo kikuu na kufuta madeni ya wanafunzi wanaodaiwa na bodi ya mikopo, huduma ya afya bure kwa wote na kuweka fao la uzazi kwa kila mwanamke atakayejifungua ili kukomesha matukip ya wanawake kutupa watoto.
Amesema Serikali yake itahakikisha kila mtoto atakayezaliwa Tanzania anakuwa hadi kufikisha umri wa miaka 18 ndipo ataachwa aanze kujitegemea.
Amesema Serikali yao pia itahakikisha uunganishaji wa umeme na maji unakuwa bure kwa nchi nzima ndani ya siku 90, kwa sababu wanalenga kutoa huduma zisizo na ubaguzi kwa kila Mtanzania.
"Umeme tutaunganisha bure nchi nzima na kazi hiyo itafanyika ndani ya siku 90 mara tutakapoapishwa na kuingia madarakani, lakini itakwenda sambamba na maunganisho ya maji," amesema Mulumbe.
Katika hatua nyingine, Mulumbe ametaja kilichomchelewesha njiani kabla ya kufika ofisi za INEC ni ufinyu wa barabara unaosababisha foleni na ajali nyingi alizosema amezishuhudia.
Mgombea mwenza wa ADC, Shoka Khamis Juma, amesema Serikali watakayoiongoza italinda na kudumisha Muungano, huku vyama vya siasa vyote vikiahidiwa ruzuku.
Hata hivyo, Shoka amevitaka vyama vingine viache kususia uchaguzi badala yake waungane ili kukitoa Chama cha Mapinduzi (CCM) madarakani. Amesema kikiachwa, kitaendelea kuendesha nchi kwa kuwabagua wengine.
"Huu ni ubaguzi mkubwa, haiwezekani wapo madarakani na wanatumia rasilimali za nchi halafu wanaweka sharti kwamba ili upate ruzuku eti lazima ufikishe asilimia tano ya kura, hii hapana," amesema.
Kingine ametaja mpango wa uchangishaji fedha kwa ajili ya kampeni uliofanywa na CCM kwamba nao watafanya hivyo ili kupata nguvu ya kufanya kampeni.
“Hata sisi tutaitisha harambee ya kukichangia chama chetu ili nacho kipate nguvu ya kufanya kampeni,” amesema mgombea mwenza huyo.