ADC yaahidi bucha za nyama pori, huduma za afya bure
Mgombea urais kupitia Chama cha Alliance For Democtratic Change (ADC), Wilson Mulumbe akizungumza na wakazi wa Balili wilayani Bunda akiwa njiani kuelekea katika Kijiji cha Nyamuswa wilayani humo kwaajili ya mkutano wa kampeni wa chama hicho. Picha na Beldina Nyakeke
Muktasari:
- Mgombea urais wa ADC, Wilson Mulumbe, ameahidi endapo chama chake kitaingia madarakani kitaruhusu kuanzishwa bucha za nyama pori ili wananchi wanufaike na rasilimali. Pia ameahidi kutotoza kodi wajasiriamali wadogo chini ya Sh5 milioni na kutoa huduma za afya bure.
Bunda. Mgombea urais wa Tanzania kupitia Chama cha Alliance For Democratic Change (ADC), Wilson Mulumbe, amesema endapo chama chake kitafanikiwa kushika dola, Serikali yao itaruhusu kuanzishwa kwa bucha za nyama pori ili kuwawezesha wananchi kunufaika moja kwa moja na rasilimali za wanyamapori zilizopo nchini.
Akihutubia kwenye mkutano wa kampeni leo Septemba 9, 2025 uliofanyika katika Kijiji cha Nyamuswa, Jimbo la Bunda, Mulumbe amesema kuwa kwa muda mrefu Watanzania, hususan wakazi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa, wamekuwa wakinyimwa fursa ya kufaidika na rasilimali hizo bila sababu za msingi.
“Ni wakati sasa wa kuwapa wananchi fursa ya kweli ya kufaidika na rasilimali za Taifa lao. Tuna rasilimali nyingi, lakini wananchi hawazigusi hata kwa macho,” amesema Mulumbe, huku akishangiliwa na wakazi wa Nyamuswa.
Amesema kwa mujibu wa wataalamu, wanyamapori wanatakiwa kuvunwa mara mbili kwa mwaka, hivyo wawindaji wadogo watanufaika na fursa hiyo kwa ajili ya kujiongezea kipato huku wananchi wakipata kitoweo kwa urahisi.
Kuhusu wajasiriamali, Mulumbe amesema chama hicho hakitatoza kodi kwa wajasiriamali wadogo wenye mtaji chini ya Sh5 milioni na badala yake, wajasiriamali hao watapata fursa ya kukuza mitaji yao ndipo waanze kuchangia pato la nchi kupitia kodi.
“Wajasiriamali wadogo wameumizwa kwa muda mrefu, wametozwa kodi na tozo nyingi. Sisi tunaahidi kuwalea hadi mtakapokuwa na uwezo wa kulipa kodi, na kodi zetu zitakuwa rafiki ili tuweze kuwa na walipakodi wengi wenye uwezo wa kulipa kodi kwa maendeleo ya nchi yetu,” amesema.
Amewaomba wakazi wa Jimbo la Bunda kukichagua chama chake ili kuwaletea maendeleo kutokana na kukosekana kwa maendeleo katika jimbo hilo, ikiwemo ubovu wa miundombinu ya barabara na ukosefu wa huduma za kijamii ikiwemo maji safi na salama.
“Nimepita kwenye barabara za jimbo hili, zote ni mbovu hadi magari yetu yamepata pancha. Hakuna huduma ya maji safi na salama, huduma za afya haziridhishi. Niwaahidi mkituchagua changamoto hizi zitapata suluhisho la kudumu na mtapata huduma bora kwani ni haki yenu,” amesema.
Amesema wananchi hawatakiwi kuwa waoga bali wafanye maamuzi sahihi kwa mustakabali wa ustawi wa nchi yao, na kwamba ni wakati wao wa kukipumzisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoka madarakani.
Akiwa wilayani Bunda, mgombea urais huyo amekabidhiwa fimbo na wazee wa kimila wa kabila la Waikizu wilayani humo ikiwa ni ishara ya kumuunga mkono mgombea huyo pamoja na mgombea ubunge wa Jimbo la Bunda.
Akizungumza kwa niaba ya wazee hao, Phares Muhuku amesema hawajajiunga na chama chochote cha siasa, bali wanachotamani ni kupata kiongozi mwenye kuwajibika na kuweka mbele masilahi ya wananchi kwa ujumla.
“Huyu mgombea ubunge ni sisi ndiyo tulimtaka agombee baada ya kufanya utafiti tukajiridhisha kuwa ataleta maendeleo kwa wananchi. Tukasema tutamuunga mkono kupitia chama chochote, na tunashukuru uongozi wa ADC ukamruhusu agombee. Sisi tunaahidi kumuunga mkono,” amesema.
Mgombea ubunge wa Bunda kupitia ADC, Maxmilian Madoro, amesema ana nia ya dhati ya kuwatumikia wakazi wa jimbo hilo na kwamba nia hiyo amekuwa nayo kutokana na hali duni ya maisha ya wakazi wa Jimbo la Bunda.
“Huduma zote za jamii ni mbovu, mfano barabara, maji na hata uchumi wa mtu mmoja mmoja na wa jimbo kwa ujumla ni mbaya sana. Mkinichagua nitaibana Serikali ili maisha yenu yaakisi uwepo wa rasilimali hizi muhimu tulizobarikiwa kuwa nazo,” amesema.
Kuhusu changamoto ya huduma za Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kuwa mbali na wakazi wa jimbo hilo, Madoro amesema kuwa endapo atachaguliwa kuwa mwakilishi wa Jimbo la Bunda, atahakikisha kunaanzishwa mamlaka ya mji mdogo ndani ya jimbo hilo ili kupunguza utegemezi wa huduma kutoka makao makuu ya Halmashauri ya Bunda Vijijini.
Amesema hali hiyo inawalazimu wakazi wa jimbo hilo kusafiri hadi Kisorya kupitia Halmashauri ya Mji wa Bunda ili kupata huduma mbalimbali, jambo linalowaletea usumbufu na gharama zisizo za lazima.
Madoro ameeleza kuwa, endapo atachaguliwa, atahakikisha huduma hizo zinapatikana kwa ukaribu kupitia uanzishwaji wa mamlaka ya mji mdogo katika Kijiji cha Nyamuswa, ndani ya jimbo hilo.
“Mimi nitatoa jengo ili tuwe na mamlaka ya mji mdogo. Wananateseka sana kutafuta huduma, mtu wa Mugeta kwenda Kisorya kisa anataka muhuri wa halmashauri ni mateso. Niko tayari kutoa jengo ili huduma zipatikane kwa ukaribu,” amesema.
Mwenyekiti wa ADC Taifa, Shaban Itutu, amesema chama chake hakitakubali Mtanzania yeyote kupoteza maisha kutokana na kukosa fedha kwa ajili ya matibabu, bali kifo kitokane na mapenzi ya Mungu.
“Sisi tukipata nafasi tutatoa huduma za afya bure kabisa. Mwananchi hautatoa kiasi chochote cha fedha kutibiwa. Uwezo wa kugharimia matibabu kwa kila Mtanzania tunao kama nchi, kwani tumejaliwa utajiri wa kutosha. Tuna madini, wanyama kwa ajili ya utalii. Nyie tupeni nchi muone,” amesema.