Ajali za barabarani Dar zapungua, 62 wapoteza maisha ndani ya miezi sita
Muktasari:
- Licha ya kupungua kwa idadi ya ajali za barabarani katika nusu ya kwanza ya mwaka 2026, watu 62 wamefariki dunia jijini Dar es Salaam. Jeshi la Polisi linasema makosa ya kibinadamu bado ndiyo chanzo kikuu cha ajali na limeeleza mikakati inayotekelezwa kudhibiti hali hiyo.
Dar es Salaam. Jumla ya watu 62 wamefariki dunia katika ajali 58 za barabarani zilizotokea jijini Dar es Salaam kati ya Januari na Juni 2026, licha ya idadi ya ajali kupungua ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana.
Takwimu hizo zimetolewa leo Julai 3, 2026 na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Boniface Mbao, wakati wa hafla ya Kamati ya Usalama Barabarani Kanda Maalum ya Dar es Salaam kukabidhi vitendea kazi kwa Jeshi la Polisi.
Mbao amesema katika kipindi hicho jumla ya ajali 124 ziliripotiwa, huku ajali 57 zikisababisha majeruhi 120.
Amesema takwimu hizo zinaonyesha mafanikio ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2025, ambapo ajali zilizoripotiwa zilikuwa 138, hivyo kupungua kwa ajali 14 sawa na asilimia 10.1.
Aidha, amesema mwaka 2025 kulikuwa na ajali za vifo 69, hivyo mwaka huu zimepungua kwa ajali 11. Watu waliofariki mwaka jana walikuwa 80, ikilinganishwa na 62 mwaka huu, ikiwa ni punguzo la watu 18 sawa na asilimia 22.5.
Kwa upande wa ajali za majeruhi, amesema mwaka 2025 zilikuwa 90, lakini mwaka huu ni 57, ikiwa ni punguzo la ajali 33 sawa na asilimia 36.7. Idadi ya waliojeruhiwa imepungua kutoka 142 mwaka jana hadi 120 mwaka huu.
Akizungumzia chanzo cha ajali hizo, Mbao amesema makosa ya kibinadamu bado yanaongoza, yakiwamo ulevi, kuendesha kwa uzembe, mwendokasi, kuyapita magari mengine bila tahadhari pamoja na kutoheshimu alama, ishara na michoro ya barabarani.
Kuhusu mikakati ya kukabiliana na hali hiyo, amesema Jeshi la Polisi linaendelea kutoa elimu ya usalama barabarani kupitia Dawati la Elimu pamoja na kutumia vyombo vya habari, stendi za mabasi, vijiwe vya bodaboda, shule, makanisa na maeneo mengine yenye mikusanyiko ya watu.
Pia amesema ukaguzi wa magari unaendelea kufanywa kupitia Dawati la Ukaguzi wa Magari ili kuhakikisha magari yanayotumika barabarani yanakidhi viwango vya usalama.
"Tunaendelea pia kufanya operesheni za kuwakamata madereva wanaokiuka sheria za usalama barabarani, kuwatoza faini pale inapobidi na kuwafikisha mahakamani kwa makosa mbalimbali," amesema.
Mbao amesema Jeshi linaendelea kutumia mifumo ya Vehicle Tracking System (VTS) na vifaa vya Speed Radar kuwabaini madereva wanaokiuka viwango vya mwendokasi, hususan mabasi yanayofanya safari za mikoani na nchi jirani.
Hata hivyo, amesema kikosi hicho kinakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwamo upungufu wa magari ya kazi, vifaa vya kupima ulevi, taa za kuongeza mwanga wakati wa operesheni za usiku pamoja na vifaa vya ofisi kama kompyuta, skena, printa na spika za kutolea elimu kwa wananchi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, ameipongeza Kamati ya Usalama Barabarani kwa kutoa magari yatakayosaidia shughuli za usimamizi wa sheria.
Amesema magari hayo yanapaswa kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa na si kwa matumizi binafsi.
"Sitegemei kuyaona magari haya yanabeba mkaa Mkuranga au viazi Kariakoo. Yanapaswa kuwa mfano wa kuigwa katika kuzingatia sheria za usalama barabarani," amesema.
Muliro amesema pamoja na elimu inayoendelea kutolewa kwa wananchi, Jeshi la Polisi halitasita kutumia sheria dhidi ya watakaokiuka taratibu za usalama barabarani.
Awali, Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Barabarani Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Mohammed Bahashwan, amesema kamati hiyo imekabidhi gari aina ya Toyota Hilux Double Cab na Toyota Harrier kwa Jeshi la Polisi ili kusaidia shughuli za usimamizi wa usalama barabarani.
Amesema zaidi ya Sh100 milioni zilizotumika kununua magari hayo zimetokana na mapato ya kamati kupitia makusanyo ya makosa ya barabarani, huku fedha nyingine zikichangwa na wadau mbalimbali.
Naye Mwenyekiti wa Wenyeviti wa Kamati za Usalama Barabarani, Idd Azzan, amesema wataendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kutoa elimu kwa wananchi na kuimarisha usalama barabarani nchini.