Barrick yang'ara tuzo ya Rais ya walipa kodi wakubwa
Meneja Mkazi wa Barrick nchini, Dk. Melkiory Ngido, akipokea Tuzo ya Rais ya Mlipa Kodi Kinara kwa niaba ya Barrick Mining Corporation wakati wa hafla ya kuwatunuku walipa kodi bora, iliyofanyika katika maadhimisho ya miaka 30 ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
- Tuzo hiyo ilitolewa wakati wa hafla ya kuwapongeza walipa kodi bora iliyofanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 30 ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, chini ya mgeni rasmi Rais Samia Suluhu Hassan.
Dar es es Salaam. Kampuni ya Barrick Mining Corporation, yenye ubia na Serikali kupitia Twiga Minerals Corporation, imeendelea kudhihirisha nafasi yake kama mmoja wa walipa kodi wakubwa nchini baada ya kutunukiwa Tuzo ya Rais ya Mlipa Kodi Mkubwa kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Tuzo hiyo ilitolewa wakati wa hafla ya kuwapongeza walipa kodi bora iliyofanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 30 ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam, chini ya mgeni rasmi Rais Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Samia aliwapongeza walipa kodi kwa mchango wao katika kuongeza mapato ya Serikali, akisema fedha zinazokusanywa kupitia kodi zimeendelea kuiwezesha Serikali kutekeleza miradi ya maendeleo na kuboresha huduma za kijamii.
Kutunukiwa kwa Barrick ni mwendelezo wa kutambuliwa kwa mchango wake katika uchumi wa Tanzania kupitia ulipaji wa kodi. Kampuni hiyo imekuwa ikishinda tuzo kama hiyo katika miaka iliyopita kutokana na mchango wake mkubwa katika mapato ya Serikali.
Meneja Mkazi wa Barrick nchini, Dk. Melkiory Ngido (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na Rais Samia Suluhu Hassan na viongozi wa baadhi ya kampuni zilizotunukiwa tuzo za walipa kodi wakubwa, baada ya hafla ya maadhimisho ya miaka 30 ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Mbali na tuzo hiyo, Barrick-Twiga pia imeendelea kuwa kinara wa kutoa gawio kwa Serikali baada ya kutoa Sh221.9 bilioni mwaka huu, hatua inayoonyesha mafanikio ya ubia kati ya Serikali na kampuni hiyo katika sekta ya madini.
Migodi inayosimamiwa chini ya ubia huo ni North Mara, Bulyanhulu na Buzwagi, ambapo mgodi wa Buzwagi kwa sasa uko katika hatua za kufungwa na umeanza kubadilishwa kuwa Kongani Maalumu ya Kimataifa ya Sekta ya Madini (Buzwagi Economic Special Zone).
Mbali na ulipaji wa kodi, Barrick imeendelea kuchangia uchumi wa taifa kupitia malipo ya mrabaha, gawio, tozo mbalimbali na kuimarisha mnyororo wa thamani kupitia biashara zinazohusiana na shughuli zake za uchimbaji madini.
Akizungumzia mafanikio hayo, Meneja Mkazi wa Barrick nchini, Dk Melkiory Ngido, alisema ushirikiano kati ya Barrick na Serikali unaendelea kuzaa matokeo chanya kwa kuongeza mapato ya Serikali na kuhakikisha Watanzania wananufaika zaidi na rasilimali za madini.
Alisema kampuni hiyo itaendelea kutekeleza mikakati yake ya uwekezaji endelevu sambamba na kuimarisha ushirikiano na Serikali kwa lengo la kuchochea maendeleo ya sekta ya madini na uchumi wa nchi.
Pia alisema Barrick imeendelea kutekeleza kwa ufanisi programu za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), kupitia uwekezaji katika sekta za elimu, afya, maji safi na salama pamoja na ujenzi na uboreshaji wa miundombinu katika jamii zinazozunguka migodi yake.