Biteko: Kura yako ni dhamana ya maendeleo ya Bukombe
Muktasari:
- Biteko awahimiza wakazi wa Busonzo kujitokeza Oktoba 29, 2025 kuwachagua wagombea wa CCM, akiahidi kuendeleza miradi ya maji, umeme na elimu chini ya uongozi wa Samia.
Geita. Mgombea ubunge wa Jimbo la Bukombe kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Doto Biteko, amewahimiza wananchi wa Kata ya Busonzo, Wilaya ya Bukombe, mkoani Geita, kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025, na kuwachagua kwa kura za kishindo wagombea wa chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao.
Akizungumza jana, Septemba 9, 2025, wakati akiendelea na kampeni zake katika kata hiyo, Dk Biteko amesema ushindi wa CCM utatoa fursa ya kuendeleza miradi ya maendeleo ambayo tayari imeanzishwa chini ya uongozi wa mgombea urais wa chama Samia Suluhu Hassan, anayetetea nafasi hiyo.
Ameeleza kuwa Kata ya Busonzo, hususan eneo la Idoselo, lilikuwa likikabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo upungufu wa miundombinu ya barabara, shule na huduma za afya.
“Hapa Idoselo tumejenga kituo kikubwa cha kuzalisha umeme megawati tano ili wananchi wapate umeme. Tunataka kuongeza upatikanaji wa maji, na baada ya uchaguzi tutapanua chanzo cha maji ili kuhakikisha kunakuwa na maji ya uhakika,” amesema Dk Biteko.
Ametaja vipaumbele vya CCM ni kujenga shule nyingine ya sekondari Idoselo ili kupunguza adha ya wanafunzi kwenda kusoma Busonzo.
Pia, Dk Biteko amewahimiza wananchi pamoja na wajumbe wa CCM kujitokeza kwa wingi siku ya upigaji kura, Oktoba 29, na kumpigia kura mgombea wa urais, Samia, sambamba na kumchagua yeye kwa nafasi ya ubunge wa Jimbo la Bukombe, pamoja na John Merikiori kwa nafasi ya udiwani wa Kata ya Busonzo.
Akizungumza wakati wa kumnadi mgombea huyo wa udiwani, Dk Biteko amesema Merikiori ni kiongozi mchapakazi, mwenye dira ya maendeleo, na nia thabiti ya kuwatumikia wananchi kwa uadilifu.
Ametoa wito kwa wakazi wa Busonzo kuhakikisha wanamchagua kupitia sanduku la kura ifikapo Oktoba 29.
Pia, amesisitiza kuwa, ili CCM ipate ushindi wa kishindo, ni muhimu wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga kura na kuwachagua wagombea wa chama hicho katika ngazi zote.
Kwa upande wake, mgombea udiwani wa Kata ya Busonzo, John Merikiori, amesema ni wajibu wa kila mwananchi kutumia haki yake ya kupiga kura na kuwachagua wagombea wa CCM, ambao wakipewa dhamana ya uongozi, watahakikisha wanatekeleza miradi ya maendeleo kwa maslahi ya wananchi wote.