Dk Nchimbi: Tunashughulika na matatizo ya Watanzania, CCM itaisimamia Serikali
Muktasari:
- Mgombea mwenza wa urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi ameendelea kuzisaka kura za chama hicho kwa Rais, wabunge na madiwani katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano, Oktoba 29, 2025.
Sumbawanga. Mgombea mwenza wa urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amesema chama hicho kimejikita kugusa sekta zitakazokwenda kukuza uchumi wa wananchi hususan vijana.
Amesema katika miaka mitano iliyopita Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imewekeza katika nyanja mbalimbali za afya, elimu, miundombinu ya barabara za lami mjini na vijijini kutoka kilomita 39.4 hadi 46.5 pamoja na sekta ya uvuvi.
Dk Nchimbi amesema hayo leo Jumanne, Septemba 9, 2025, katika mkutano wa kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika uwanjani, kwenye ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Majengo, Manispaa ya Sumbawanga Mjini, Mkoa wa Rukwa. Ni mkutano wa mwisho mkoani humo baada ya kuanza jana Jumatatu.
Amesema malengo ya CCM ni kuboresha maisha ya Watanzania na kuwa na Taifa lenye kujitegemea, na hilo litafanikiwa ikiwa Samia atachaguliwa kuendelea kubaki madarakani.
Dk Nchimbi amezungumzia maendeleo yaliyofanywa na Samia ikiwemo uboreshaji wa Bandari ya Kasanga, Uwanja wa Ndege wa Sumbawanga na utoaji mikopo kwa makundi maalumu.
Amesema chama kimejipanga kusimamia na kuimarisha huduma za afya kwa wajawazito na watoto, ili kudhibiti na kumaliza vifo vya kinamama wakati wa kujifungua kutoka asilimia 9 hadi 4.
Pia, amesema watapunguza udumavu kwa watoto wa chini ya miaka mitano na kuongeza huduma za lishe kwa makundi yanayoathirika zaidi, ikiwa ni pamoja na watoto, wajawazito na vijana balehe.
“Licha ya Mkoa wa Rukwa kulima mazao ya chakula na biashara, changamoto ya udumavu ni kwa asilimia 49.8, na tutahakikisha tunapunguza tatizo,” amesema Dk Nchimbi.
Awali, Mwenyekiti mstaafu wa CCM Wilaya ya Songea Mjini, Mkoa wa Ruvuma, Hamis Ally amesema chama hicho kina mikakati ya kudhibiti ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto, wasichana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.
Sambamba na hilo, amesema chama kitaimarisha makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto pamoja na kuhakikisha mifumo ya malezi inazingatia uwajibikaji na utunzaji wa familia katika jamii.
Akimkaribisha Dk Nchimbi, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Rukwa, Siraf Maufi amesema wataimarisha huduma za ustawi kwa wazee, ikiwemo huduma za afya, matunzo na ushirikishwaji katika uamuzi na shughuli mbalimbali za maendeleo.
Kwa upande wake, Agnes Lyoba, aliyekuwapo mkutanoni, akizungumza na Mwananchi amesema anawaomba wagombea kutimiza wanayoyaahidi ili waendelee kuaminika.
“Niombe tu wagombea kutimiza ahadi zao, sio kuongea tu ili wapate kura, bali tunatamani kuona utekelezaji wake,” amesema Agnes.
CCM: Tutaisimamia Serikali
Jana Jumatatu, Septemba 8, 2025, Dk Nchimbi alifanya mkutano wa kampeni katika Jimbo la Kalambo mkoani humo, na amesema chama hicho kitaisimamia Serikali kumalizia uunganishaji wa umeme kwenye vitongoji vyote vilivyobakia.
Amesema wataisimamia Serikali kukamilisha mradi wa TAZA unaohusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 400 kutoka Iringa hadi Sumbawanga na kuunganisha nchi za Tanzania na Zambia.
“Mradi huu pia utahusisha ujenzi wa vituo vya kupooza umeme katika Wilaya ya Sumbawanga, Kalambo na Nkasi,” amesema Dk Nchimbi.
Amesema wataimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kuhamasisha matumizi ya nishati mbadala na kuongeza upatikanaji wa gesi asilia katika viwanda, taasisi, majumbani na kwenye magari.
Baadaye leo Jumanne, Dk Nchimbi ataendelea na mikutano mkoani Katavi.
Endelea kufuatilia Mwananchi.