Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CCM yaahidi kumaliza migogoro ya ardhi

Mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan

Muktasari:

  • Samia aaahidi programu ya Tutunzane kupelekwa wilayani Kilosa ili kumaliza migogoro ya ardhi iliyopo, wananchi waishi kwa amani.

Kilosa. Mgombea urais wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Samia Suluhu Hassan ameahidi kuongeza maeneo ya wafugaji katika Wilaya ya Kilosa kutoka ekari milioni 3.46 hadi kufikia milioni sita ili kumaliza migogoro kati ya wakulima na wafugaji.

Amesema hayo leo Agosti 30, 2025 kwenye mkutano uliofanyika Kilosa, akiendelea na kampeni mkoani Morogoro alizoanza jana, Agosti 29.

Mkoa wa Morogoro hususani wilaya za Mvomero na Kilosa, zimekuwa zikikabiliwa na migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji, jambo ambalo limekuwa likihatarisha maisha ya watu na kurudisha nyuma maendeleo.

Samia amesema Wilaya ya Mvomero imefanikiwa kutatua migogoro baina ya wakulima na wafugaji kupitia programu ya Tutunzane, akiahidi kupeleka programu hiyo Kilosa ili kumaliza migogoro ya ardhi iliyopo, wananchi waishi kwa amani, huku wakiendelea na shughuli za maendeleo.

"Tutakuja na mpango wa kuongeza maeneo ya wafugaji, tuna ekari milioni 3.46, tunakwenda kuongeza hadi ekari milioni sita kwa ajili ya wafugaji. Hii ni kwa ajili ya kupunguza migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji," amesema.

Samia ameeleza mashamba yenye ekari 53,475 ambayo yalikuwa hayajaendelezwa yalifutwa na kupimwa ekari 21,872 ambazo ziligawiwa kwa wananchi kwa ajili ya kilimo, makazi na uwekezaji.

Amesema wananchi 8,557 kutoka kwenye vikundi 186 vilivyopo katika vijiji 11, walifaidika na mpango huo na sasa kazi ya kupima inaendelea. Ameeleza kazi ya ugawaji wanakwenda kuimaliza wakichaguliwa kuendelea kuongoza.

"Niwahakikishie kwamba, tutagawa mashamba bila kuonea mtu, bila dhuluma. Na wale wenye matatizo tunatambua, watapata vipande vya ardhi," amesema akiwaomba kura wakazi wa Kilosa.

Awali, mgombea ubunge Jimbo la Kilosa, Profesa Palamagamba Kabudi alieleza kuhusu mafanikio ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwamo ujenzi wa bwawa la Kidete ambalo limekamilika na kusaidia shughuli za kilimo cha umwagiliaji na kuzuia mafuriko.

Profesa Kabudi amesema Samia alipoingia madarakani, vijiji 16 pekee kati ya vijiji 82 vilivyopo Kilosa ndivyo vilikuwa na umeme, lakini hadi kufikia sasa, vyote vimeunganishwa na nishati hiyo.

"Tunashukuru kwa uamuzi wako wa kuifufua reli ya Kilosa - Kidatu, itasaidia kuchochea shughuli za kiuchumi kwa watu wetu katika ukanda huu," amesema.

Akiwa Gairo, Samia amewahimiza wananchi kukipigia kura chama hicho ili kiendeleze kazi iliyofanyika miaka mitano iliyopita, ikiwamo utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye sekta za afya, elimu, maji na miundombinu.

Ameahidi akichaguliwa miaka mitano ijayo, atahakikisha Serikali inakamilisha miradi ikiwamo ya barabara kutoka Robeho hadi Kisihi. Pia, kuongeza vituo vitano vya afya katika eneo hilo.

Mgombea ubunge wa CCM, Gairo, Ahmed Shabiby amebainisha kuwa changamoto kubwa katika jimbo hilo ni maji, inayosababishwa na kukosekana kwa umeme wa kutosha kusukuma kiwango kikubwa cha maji.

Hata hivyo, amesema kazi ya ujenzi wa kituo cha kupoza umeme inaendelea na kwamba ikikamilika, tatizo la maji pia litapungua kwa wakazi wa eneo hilo.

"Tulikuwa na changamoto ya soko la mbaazi zilizokuwa ghalani, lakini tulizungumza na Waziri wa Kilimo, mbaazi zote zilizokuwa ghalani zimenunuliwa," amesema.