Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chaumma kuja na mfumo, CSR inufaishe wazawa

Muktasari:

  • Kampuni zinatakiwa kutumia sehemu ya mapato yao kupitia CSR kuwekeza katika maendeleo ya jamii wanakofanyia shughuli zao za kiuchumi, kwa kutambua kuwa mafanikio ya kampuni hayawezi kutenganishwa na ustawi wa jamii inayowazunguka

Geita. Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), kimeahidi kuweka mfumo wa uwazi na kudumu wa usimamizi wa miradi ya Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR) ikiwamo migodi, iwapo kitachaguliwa kuongoza nchi Oktoba 29, mwaka huu.

Kampuni zinatakiwa kutumia sehemu ya mapato yao kupitia CSR kuwekeza katika maendeleo ya jamii wanakofanyia shughuli zao za kiuchumi, kwa kutambua kuwa mafanikio ya kampuni hayawezi kutenganishwa na ustawi wa jamii inayowazunguka.

Kwa mujibu wa Chaumma, ingawa nia ya CSR ni njema,  lakini utekelezaji wake umekumbwa na changamoto kubwa nchini, unanufaisha wachache, badala ya jamii nzima inayolengwa na haizingatii mahitaji halisi ya jamii, bali huchaguliwa kwa misingi ya ushawishi wa watu wachache wenye mamlaka au ukaribu na viongozi wa kampuni.

Akizungumza leo Jumanne Septemba 16, 2025 katika mkutano wa kampeni uliofanyika eneo la Nyankumbu, Geita Mjini, mgombea urais wa Tanzania kupitia Chaumma, Salum Mwalimu amesema fedha nyingi zinazokusanywa kutoka kwa wawekezaji, zinawanufaisha watu wachache huku wananchi wakibaki masikini licha ya kuzungukwa na raslimali nyingi.

 “Mabilioni ya fedha yanayokusanywa kila mwaka yamegeuka kichaka cha baadhi ya wachache kufaidi peke yao. Kila mwaka wanasema wananunua madawati lakini hakuna lolote. Leo Geita haina madawati wala madarasa, wakati mgodi upo pale,” amesema Mwalimu.

Hivyo, amesisitiza kuwa, Serikali ya Chaumma itafumua utaratibu wa sasa wa usimamizi wa rasilimali na kuweka mfumo unaowezesha miradi mikubwa ya kijamii kama hospitali za kisasa zenye wataalamu, vifaatiba vya hali ya juu na huduma bora kwa wananchi.

 “Haiwezekani mtu akiugua Geita aende Hospitali ya Bugando. Tunajivunia nini kama tuna mgodi mkubwa, lakini majisafi hakuna, barabara ni shida na viwanda hakuna?,” amehoji Mwalimu.

Ameahidi kuwa,  ajira katika migodi lazima zianze kuwanufaisha wenyeji wa maeneo husika, akitoa mfano kuwa kati ya ajira 1,000 angalau 300 na ziwe kwa vijana wa Mkoa wa Geita.

“Hili si ubaguzi, bali ni haki. Vijana wakipata ajira Geita, hawatakimbilia Dar es Salaam au Ulaya, watawekeza nyumbani na utajiri utabaki Geita,” ameongeza.

Mwalimu amesisitiza kuwa, rasilimali kama madini zililetwa ili ziwanufaishe wananchi wa maeneo husika na si kuwanufaisha watu wa nje pekee.

Amesema akifanikiwa kuongoza nchi, miradi ya maendeleo kama hospitali kubwa itabeba jina la mgodi huo kama alama ya kudumu kwa vizazi vijavyo.

 “Tusikubali uzembe huu kuendelea. Lazima maeneo yenye migodi yawe na alama ya kudumu kama kumbukumbu ya uwepo wa rasilimali hizo. Hospitali kubwa, vifaa vyote na hata wamiliki wa migodi wakitaka kutibiwa, waje hapa, si kwenda nje ya nchi,” amesema mgombea huyo.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Mawasiliano kwa Umma kupitia chama hicho, John Mrema  amesema Mkoa wa Geita ni miongoni mwa mikoa yenye idadi kubwa ya ng’ombe nchini, lakini hadi sasa hakuna kiwanda hata kimoja cha kusindika maziwa, nyama wala ngozi.

Katika mkutano huo, Mrema amesema hali hiyo ni ushahidi wa kushindwa kwa Serikali iliyopo madarakani kutumia ipasavyo rasilimali zilizopo kwa manufaa ya wananchi.

"Hili ni jambo la kusikitisha. Tuna maelfu ya ng’ombe lakini hakuna kiwanda cha kusindika maziwa, hakuna kiwanda cha ngozi hii inaonesha wazi kuwa waliopo madarakani wameshindwa kuongoza," amesema.

Ameongeza kuwa huu ni wakati wa wananchi kuamka na kuchukua hatua madhubuti kwa kutafuta mabadiliko ya kweli, ikiwa ni pamoja na kukiweka pembeni chama kilichoshindwa kutimiza matarajio ya wananchi.

"Ni wakati wa kuamua. Ni wakati wa kusema imetosha," amesema Mrema.